in , , ,

Hakuna suluhu ubaguzi katika soka England..

*Wachezaji wamewatolea uvivu viongozi wao

*Swansea, Wigan wagomea fulana za kampeni

*Rio, Roberts, Pienaar, Cisse, Lescott vinara


Sakata la ubaguzi wa rangi kwenye soka limeingia hatua mpya, baada ya wachezaji kadhaa weusi kuwatolea uvivu wanafiki.
Mshambuliaji wa Reading, Jason Roberts, Mwingereza mwenye asili ya Grenada alivunja ukimya kwa kukataa kuvaa fulana inayoashiria upigaji vita ubaguzi huo.
Aliungwa mkono na wachezaji zaidi ya 30, akiwamo Rio Ferdinand wa Manchester United, wanaoamini kwamba taasisi ya Kick It Out haijachukua hatua stahili kuukabili ubaguzi. Imekuwa utamaduni kila Oktoba kuadhimishwa wiki ya kupinga ubaguzi, na wachezaji wote walitarajiwa kuvaa fulana hizo kwa wiki moja kuanzia Oktoba 18.
Matukio haya yamekuja baada ya John Terry wa Chelsea kumbagua Anton Ferdinand (mdogowe Rio anayechezea Queen Park Rangers – QPR) na Luis Suarez wa Liverpool kumtolea lugha ya aina hiyo Patrice Evra wa United, kisha kukataa kumpa mkono mara mbili.
wachezaji waliokataa kuvaa fulana hizo kabla ya mechi za mwisho wa wiki ni Victor Anichebe, Sylvain Distin na Steven Pienaar wa Everton waliokuwa wakipambana na QPR.
Wenyeji wao, yaani QPR waliokataa fulana hizo ni
Anton Ferdinand kama alivyotarajiwa, Djibril Cisse, Shaun Wright-Phillips, Nedum Onouha na Junior Hoilett.
Jumamosi wachezaji wengi zaidi waligombea fulana hizo, nao ni Micah Richards na Joleon Lescott wa Manchester City na Rio Ferdinand wa Manchester United.
Mwassi wa mgomo huo alitimiza azma yake katika uwanja wa Anfield, naye ni Jason Roberts wa Reading wakati Kenwyne Jones wa Stoke naye aliitupa mbali fulana hiyo.
Swansea na Wigan walionesha mshikamano wa ajabu kwani wachezaji wao wote hawakuvaa fulana hizo.
Hatua ya wachezaji hao kukacha fulana zenye nembo yenye maneno ya Kiingereza; ‘Mchezo Mmoja Jamii Moja’ imekuja baada ya Ashley Cole wa Chelsea pia kumtetea mshirika wake Terry kortini.
Cole ambaye ni mweusi aliku kubezwa na Chama cha Soka (FA) cha Uingereza kwa vile ushahidi wakeu ulikuwa wa uongo, naye akajibu kwa kuwatusi maofisa wa FA.
Matokeo ya hatua yake ya kiburi na majigambo imeishia kutozwa faini ya Pauni 90,000. Rio amemfananisha Cole na ‘choc ice’, yaani barafu ambayo nje huweza kuwa nyeupe na ndani nyeusi. Rio alipigwa faini ya Pauni 45,000.
Terry aliadhibiwa kulipa faini ya Pauni 220,000 na kukosa mechi nne za ligi, akadai angekata rufaa.
Hata hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita amesema hatakata rufaa, hatua inayoonesha ameridhia adhabu zote na anajua kwamba alifanya makosa ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Anton.
FA ilimwadhibu Suarez kukosa mechi nane na kulipa faini ya Pauni 40,000 kwa makosa yake ya kujirudia rudia. Chelsea nao wamemwongezea Terry adhabu na walisema Cole naye angeadhibiwa, lakini Terry anabaki nahodha wa mabingwa hao wa Ulaya.
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, taasisi ya Kick It Out inachukuliwa na wachezaji weusi kwamba imelemaa na haijakuwa makini kushughulikia tatizo hilo, hivyo wakaamua kuachana na fulana zao, ili walau kufikisha ujumbe.
Wakati makocha wa timu ambazo wachezaji wao waligomea fulana hizo wakionesha upole, Kocha wa Manchester United, Alex Ferguson aligeuka mbogo, akidai Rio angeshughulikiwa.
Lakini ni Rio huyo huyo anayetegemewa na klabu yake katika ulinzi Jumanne hii katika hatua za mtoano za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Jumatatu asubuhi, Rio na Ferguson walionekana mazoezini, wote wakitabasamu na kujenga hisia kwamba hapangekuwa na adhabu yoyote.
Yalichapishwa madai mwishoni mwa wiki, kwamba huenda Rio angeadhibiwa kwa kukatwa mshahara wa wiki mbili, ambao ni Pauni 220,000, na hatima yake Man U kuwa shakani. Si rahis kwa kocha Ferguson kuchukua hatua kama hiyo.
Hata angeadhibiwa Rio ni mtu wa msimamo na katika masahibu ya mdogo wake na mengine ya wanaodhalilishwa, amekuwa nao siku zote, bila kuogopa kitakachompata.
Pengine ni kwa sababu hiyo, Ferguson amekengeuka na kusema kwamba hakuna tatizo kati yake na Rio na kwamba mambo yote yameshawekwa sawa.
Akizunguza na waandishi wa habari Jumatatu alasiri, Ferguson alisema kwamba kilichotokea ni ukosefu wa mawasiliano kutoka kwa Rio, aliyetarajiwa kutoa notisi ya kusudio la kutovaa fulana hiyo.
Ferguson alionekana kuudhika, hasa kwa sababu alikuwa amemshambulia Roberts wa Reading kwa kutangaza kugomea uvaaji fulana, akisema kwamba mshambuliaji huyo hakuwa na hoja.
‘Kick Racism out of Football’ ilianza mwaka 1993 kabla haijabadilika na kuwa ‘Kick It Out’ mwaka 1997.
Katika msimu wa mwaka 2010/11 taasisi hiyo ilikuwa na bajeti ya £453,913. Kati ya hizo, £330,000 zilitolewa na FA, taasisi inayoendesha Ligi Kuu na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA).
Akizungumzia suala la ubaguzi kwenye soka, Mark Hughes – Kocha Mkuu wa QPR anayochezea Anton Ferdinand anasema itachukua muda mrefu kumaliza tatizo hilo.
Kocha wa Everton, David Moyes anawaunga mkono wachezaji wake watatu kwa walilofanya, japokuwa anasema kwamba hiyo haina maana anakubaliana na hoja yao.
Ni vigumu kwa kocha yeyote mweledi kuwaadhibu wachezaji weusi kwa sababu eti wamekataa kuvaa fulana hizo, kwa sababu wapo wanaowatukana mara nyingi wasioadhibiwa. Itachukua muda kupata suluhu katika hili.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Pointi 20 zatenganisha timu EPL

TAVA NATIONAL LEVEL I, IN MAGU – MWANZA