in , ,

Haaland kumwaga hasira kwa Inter Milan

Macho na masikio ya wengi yalisubiri ni lini nyota huyo atatikisa kwenye soka la Ulaya kutokana na kipaji maridhawa..

DAKIKA 180 za mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa zilishuhudia nyota nyota wa Manchester City, Erling Haaland kutoka Norway akishindwa kufurukuta, hivyo akamaliza bila kupachika bao. Mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu ulikuwa wa presha kubwa ambapo Man City walikuwa na lengo la kulipa kisasi cha kutolewa nusu fainali msimu uliopita. 

Dakika 90 zilimalizika huku beki kisiki wa Real Madrid Antonio Rudiger akimdhibiti vilivyo mshambuliaji huyo. Mchezo huo ulimalizika kwa 1-1. Katika mchezo wa marudiano kwenye uwanja wa Etihad, Erling Haaland alikutana na beki kisiki mwingine ambaye mchezo wa kwanza hakucheza, Eder Militao. 

Dakika 90 zilimalizika huku real Madrid ikichapwa mabao 4-0 na kuipa nafasi Man City kutinga fainali ya pili katika historia yao ya Ligi ya Mabingwa. Lilikuwa jambo la ajabu kwa mshambuliaji huyo moto wa kuotea mbali kushindwa kutumbikiza mpira wavuni. 

Lakini Erling Haaland alitinga fainali. Hii ni fainali yake ya kwanza katika maisha yake ya soka. Mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa utakuwa wa 30 kwake tangu alipoanza kuwa mwanasoka wa kulipwa. Leo jumamosi atakiongoza kikosi cha Manchester City kwenye uwanja wa Olimpiki wa Ataturk jijini Istanbul nchini Uturuki. 

Nyota huyo kutoka Norway alijitokeza kwenye kandanda mwaka 2019 wakati akichezea klabu ya Salzburg na kiwango chake kwenye Ligi Kuu kilikuwa cha kusisimua. Alikipeleka kiwango chake kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa akiwa na klabu hiyo, ambapo katika mechi 8 alizocheza alipachika mabao 6 akiwa na kikosi cha Salzburg ya Austria. 

Macho na masikio ya wengi yalisubiri ni lini nyota huyo atatikisa kwenye soka la Ulaya kutokana na kipaji maridhawa. Haaland aliwavutia mabosi wa Borussia Dortmund ambapo mwaka 2020 walimwaga fedha kumsajili kinda huyo ambaye alikuwa akisifika kwa kiwango cha kupachika mabao. 

Aliendeleza tabia ya kucheka na nyavu hadi mwaka 2022 ambapo pesa za Waarabu wa Man City zilitua katika ofisi ya Borussia Dortmund hivyo akasajiliwa kukipiga katika dimba la Etihad. Kusajiliwa kwake Manchester City kulikuwa na maana moja kubwa, nyota huyo alifuata nyayo za baba yake ambaye amewahi kuichezea timu hiyo. 

Pia baba yake ndiye wakala wake, na katika maisha yake ya soka alichezea klabu za Manchester City na Leeds United. Licha ya kufanikiwa kunyakua medali za Ligi Kuu ya Austria na kombe la Ujerumani, ameongeza kiwango cha mataji tangu alipojiunga na Man City. Haaland ametwaa mataji ya Ligi Kuu Engl;and na Kombe la FA akiwa na umri wa miaka 22 tu. Nyota huyu hajawahi kucheza mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa, kwahiyo fainali ya Uturuki itakuwa ya kwanza kwake akiwa chini ya kocha wa dunia Pep Guardiola.

Mtambo wa mabao

Mchezaji huyo toka Norway anasifika kwa upachikaji wa mabao. Katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa amefunga mabao 35 kutokana na mechi 29. Katika klabu aliyochezea amekuwa silaha muhimu ya kupachika mabao na kuibuka na ushindi. 

Akiwa Salzburg katika mechi nane alifunga mabao 6. Katika mechi 15 za Ligi ya Mabingwa alizocheza akiwa Borussia Dortmund alifunga mabao 13. Tangu alipojiunga na Man City msimu huu amepachika mabao 12. Haaland amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao matatu katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa alipokuwa akiichezea klabu ya Salzburg. 

Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 19, na amekuwa mchezaji wa tatu akitanguliwa na Alesandro Del Piero na Diego Costa kufunga mabao kila mechi katika michezo mitano ya kwanza tangu kujitokeza kwenye mashindano hayo. Haaland ni mshambuliaji mwenye  takwimu za juu za ufungaji. Amefunga mabao 10 katika mechi 7. Kufunga mabao 15 katika mechi 12. Kafunga mabao 20 kutokana na mechi 14, amewahi kufunga mabao 25 kutokana na mechi 20. Amewahi kutupia mabao 30 kwa mechi 25 na mabao 35 kwa mechi 27.

Mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa unakuwa wa 29 katika maisha yake ya soka. Katika mechi  28 za Ligi ya Mabingwa alizocheza hadi leo amefunga mabao katika mechi 26, lakini alikwama katika mechi ya 27 na 28 dhidi ya Real Madrid ambako hakufunga bao lolote.  

Silaha ya Guardiola

Akizungumza katika mahojiano na vyombo vya habari jana, kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amebainisha mafanikio yake yanayokana na kikosi chake kuwa na mchezaji bora. Guardiola alisema alipokuwa Barcelona alikuwa na Lionel Messi, na sasa anaye Erling Haaland katika kikosi cha Man City na ndiye silaha yake inayompa mafanikio hadi sasa. Kocha huyo alisema ana uhakika Haaland atafunga mabao katika mchezo wa fainali na kumpa ushindi. Na kwa vile Haaland hakufunga katika dakika 180 za nusu fainali, huenda leo akawa na hasira zaidi mbele yay a Inter Milan.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Magumu sita kwa Chelsea ya Pochettino

Harry Kane

Harry Kane jua linavyomchwea EPL