in , , ,

GAZETINI ANAONEKANA NEYMAR, UWANJANI ANAONEKANA COUNTINHO

Hapana shaka Brazil ndiye timu ambayo imejibebea mashabiki wengi sana kwa sababu ya aina yao ya mpira ambao wamekuwa wakicheza.

Samba ndiyo imekuwa nguzo na nembo kwao, na samba ndiyo imekuwa kivutio cha watu wengi kuipenda Brazil.

Kwa miaka mingi Samba imekuwa ni chakula chenye mchanganyiko wa virutubisho vingi vinavyohitajika kuimarisha afya ya mpira.

Afya ya mpira ya watu wengi huwa haiimariki ipasavyo kama haijapata magoli, burudani ya vyenga vya maudhi, sanaa ya mpira na mpira wa kuvutia wenye pasi nyingi.

Vyote hivi vilikuwa vinapatikana kwa Brazil, mabingwa mara 5 wa kombe la dunia na hakuna aibu yoyote kama ukisema ndiyo mabingwa wa kihistoria.

Historia yao ilianza kujengwa na vipaji toka enzi za kina Pele, Dunga, Romario, Garincha, Rivaldo, Ronaldo De Rima, Ronaldinho, Kaka mpaka sasa ikiwa na wachezaji wakawaida wanaokuzwa na magazeti.

Hapana shaka gazeti huuzika kipindi ambacho Neymar akiandikwa kwa sababu watu wengi watapenda kufuata habari zake. Hii ni kwa sababu Neymar alijidhatiti nje ya uwanja kwa kutengeneza mazingira mazuri ya kibiashara ndiyo maana ana mvuto mkubwa kuzidi Countinho.

Mvuto ambao unawafanya watu wengi wamwangalie kama mkombozi wa timu ya taifa ya Brazil uwanjani. 

Hii ni tofauti kabisa na tunavyotamani kuwa. Magazeti yanamuona Neymar kama mchezaji bora wa timu ya taifa kwa sasa lakini uhalisia unapingana na kinachoandikwa na magazeti.

Magazeti hayawezi kumuona Philippe Countinho na hayataki kabisa kumuandika katika ukubwa kwa sababu Neymar ana mvuto nje ya uwanja kuliko Philippe Countinho.

Mvuto wa Neymar unaishia nje ya uwanja peke yake lakini tunalazimisha na ndani ya uwanja awe na mvuto, mvuto ambao tunataka tumpeleke katika daraja la mchezaji bora wa timu ya taifa ya Brazil kwa sasa.

Philippe Countinho amekuwa mhimili katika michuano hii. Amekuwa akiichezesha timu vizuri akitengeneza nafasi na kufunga magoli kipindi ambacho timu inahitaji magoli.

Miguu yake imekomaa kuzidi Neymar, kwa sababu anafanya maamuzi ya haraka yenye faida kubwa kwenye timu kuliko Neymar ambaye miguu yake imebeba mambo elfu moja ya kufanya kipindi anapokuwa na mpira.

Hana maamuzi ya haraka na inafikia wakati anaikosesha timu ushindi kutokana na yeye kukaa na mpira muda mrefu.

Kitu ambacho kinamfanya anyang’anywe mpira na wakati mwingine kuishia kujiangusha bila faida yote na hii ni kwa sababu miguu yake bado haijakomaa.

Ukomavu huu unaonekana katika miguu ya Philippe Countinho mtu ambaye haonekani katika kurasa za mbele za magazeti lakini anaonekana katika kurasa za mbele za ndani ya uwanja. Na huyu ndiye mchezaji bora wa Brazil kwa sasa.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TETESI ZA USAJILI:

Tanzania Sports

KIFO CHA TIMU ZA AFRIKA KILIANZIA HAPA