in , ,

Fifa kwazidi kufukuta

*Uenyeji Kombe la Dunia 2026 kando

*Qatar hatarini kupoteza uenyeji

*Blatter huenda akang’oka Desemba

Hali ya mambo ndani ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) inazidi kuwa mbaya kwa madai kuibuliwa na sasa mchakato wa kupata mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2026 umesitishwa.

Uamuzi huo umefikiwa kutokana na tuhuma nyingi za uchafu katika mchakato wa kupata uenyeji wa fainali za 2018 na 2022 uliokwenda kwa Urusi na Qatar katika mtiririko huo.

Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke amesema ingekuwa upuuzi kuanza mchakato wa uenyeji huo katika mazingira ya sasa.

Mkutano wa kuchagua mwenyeji umepangwa kufanyika Kuala Lumpur, Malaysia, ambapo wanaopewa nafasi kubwa zaidi ya kuandaa fainali hizo ni Marekani, lakini pia Canada, Mexico na Colombia wanadhaniwa kutaka kuandaa.

Wakati michuano ya 2010 ilifanyika Afrika Kusini, yametokea maneno kwamba mshindi wa uenyeji huo walikuwa Morocco lakini Maofisa wa Fifa wakafanya fitina na kubadili matokeo, na inadaiwa upo ushahidi kuonesha Morocco ndio walikuwa washindi.

Mazingira ya uchunguzi wa sasa yanaashiria uwezekano wa Qatar kuvuliwa uenyeji wa fainali za 2022 lakini Valcke alisema kwamba masuala ya 2018 yanaendelea kama awali, Urusi wakisonga mbele na maandalizi.

Kashfa inayowagusa maofisa wa ngazi za juu wa Fifa imezidi kuwatia pabaya, ambapo saba kati ya wanaohusishwa na mlungula tayari wamekamatwa na wanatarajiwa kupelekwa nchini Marekani kukabiliana na mashitaka ya wizi, rushwa na utakatishaji fedha.

Ofisa wa ngazi za juu wa Fifa, Domenico Scala amesema ikithibitika Qatar na Urusi walinunua kura watapokonywa uenyeji, lakini hali inaelekea kuwa mbaya kwa Qatar.

Katika hatua nyingine, Rais wa Fifa, Sepp Blatter aliyeshinda muhula wa tano kwenye nafasi hiyo majuzi, anatarajiwa kuondoka Desemba 16 mwaka huu.

Aliamua kujiuzulu baada ya ushindi, kwa maelezo kwamba haungwi mkono na ulimwengu wote wa soka, licha ya mashirikisho mengi kumpa kura kwenye uchaguzi.

Blatter (79) anatuhumiwa kuwa kiongozi wa genge la watu wanaojihusisha na mlungula japokuwa yeye binafsi hajatajwa popote.
Huenda mambo yake yakafunuliwa baada ya mamlaka za Uswisi, nchi alikozaliwa na yalipo makao makuu ya Fifa, kuanzisha uchunguzi rasmi juu ya mchakato wa kupata wenyeji wa 2018 na 2022.

Uamuzi wa mwisho juu ya tarehe ya uchaguzi unatarajiwa kutolewa mwezi ujao pale Fifa watakapoitisha mkutano maalumu wa kamati yake ya utendaji.

Hiyo itampa Blatter miezi sita tu ya kubuni na kuanzisha mabadiliko kwenye chombo hicho kikubwa cha soka duniani na ameahidi kufanyia kazi mageuzi kwenye sekta aliyofanyia kazi kwa zaidi ya miaka 40.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

VODACOM KUTOA ZAWADI ZA VPL KESHO

TETESI ZA USAJILI LEO