in , , ,

EPL inachanua mapema

*Liverpool, Arsenal wamepita vigingi viwili

*Watford, Saints, Newcastle, Villa ni hoi

Washabiki wa soka, hasa wanaofuatilia Ligi Kuu ya England (EPL) wanaanza kufurahia mapema katika raundi mbili za mwanzo tu utamu wake.

Baada ya pilika za usajili kukamilika, zikibaki za wanaoweza kuondoka England kwenda mataifa mengine ambako bado wana ruhusa ya kuendelea kusajili, vionjo vipya vinaonekana EPL.

Timu kubwa zimekutana tayari – yaani zilizo kwenye zile sita bora au hata tuseme nne bora, kwani Jumamosi hii mabingwa watetezi – Manchester City walishindwa kuendeleza libeneke lililozoeleka la kushinda mechi mfululizo.

Ilikuwa kawaida ya Pep Guardiola kusambaratisha timu mchezo mmoja baada ya mwingine, lakini baada ya kushinda mechi yake ya kwanza amekumbana na kigingi cha Mauricio Pochettino na vijana wake wa Tottenham Hotspur.

Kwa kwenda kwao sare, watu wanaanza kujiuliza iwapo msimu huu Spurs wanaweza kuwa washindani wa kweli wa ubingwa wa England na kuwapa tumbo joto Man City ambao wamekuwa wakichukuliwa kwamba wao na Liverpool kombe ni la mmoja wao.

Na Liverpool katangulia kwa kushinda mechi mbili za mwanzo sambamba na Arsenal ambao wameweka rekodi ya kushinda mechi mbili za mwanzo kwa mara ya kwanza katika muongo mmoja. Ilikuwa kawaida yao kufanya maandalizi mazuri kwenye pre-season washabiki wakiwa na matumaini makubwa, lakini mechi ya kwanza wanapigwa.

Msimu huu wakiwa na Unai Emery wamekuja kivingine, wakishinda zote mbili, wachezaji wakionesha kila aina ya jitihada. Moja ya vionjo vizuri vya kuvutia na ambavyo tayari vimeanza kuzungumziwa mitaani ni mchezaji wa Washika Bunduki hao wa London, Dani Ceballos anayecheza kiungo cha kati.

Alianzishwa kwa mara ya kwanza Jumamosi hii kwenye mechi dhidi ya Burnley na akaonesha shoo ya nguvu, washabiki wakaanza kumwimbia na kumpongeza Mhispaniola huyo, wakisema hawajapata kuona kama huyo tangu enzi za Patric Vieira lakini pia wakisema kwamba hawajutii kumpoteza Aaron Ramsey.

Upacha wa Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette umeendelea vyema, wawili hao wakifunga mabao mawili ya Arsenal dhidi ya moja la wapinzani wao, pale Emirates ilipocheka, ikiwa na washabiki zaidi ya 60,000 katika mechi ya mchana.

Frank Lampard, mchezaji wa zamani wa Chelsea aliyerejea Stamford Bridge kama kocha kiangazi hiki, akaanza kwa kichapo kikali kutoka kwa Manchester United, wakilala 4-0 na baada ya kuzinduka, kwenye mchezo wake wa kwanza Stamford Bridge hali ikawa tete.

Wakati jamaa huyu anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya timu hiyo akifikiri kwamba amechukua alama zote tatu, ushindi wa kwanza kwake kama kocha na ujio mwema Stamford Bridge, pilau lake lilitiwa mchanga na mchezaji wa Leicester, Wilfred Ndidi.

Lilikuwa bao la kusawazisha, kufuta lile la mapema dakika ya 20 la Mason Mount. Vijana wa Lampard walianza kwa nia hasa, lakini hawakuwa na pumzi ya kuwazuia hao wa Brendan Rodgers. Timu iliyopanda daraja msimu huu, Sheffield United waliwatandika Crystal Palace 1-0.

Mzunguko wa pili unapoona timu mbili tu zikiwa zimeshinda mechi zote – Liverpool na Arsenal, zipo nne ambazo zimefungwa mechi zote, nazo ni Watford, Southampton, Newcastle na Aston Villa. Nne zimekwenda sare moja na kufungwa moja, moja imekwenda sare zote nan a tatu zimefungwa mechi moja na kushinda moja.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Msimu mpya na usajili mpya

Tanzania Sports

Sanchez: Mshahara pasua kichwa