in , ,

English Premier League 2015-2016 Kuanza

*Tunaziangalia timu zote zinazoshiriki EPL kwa ufupi*

ARSENAL

Arsene Wenger anaonekana kukiamini kikosi chake. Jina kubwa pekee alilosajili mbaka sasa ni Peter Cech kutoka Chelsea.

 

Rekodi za golikipa huyu zinatosha kabisa kuwaaminisha washabiki wa Arsenal kuwa idadi ya mabao 36 ambayo Arsenal wameruhusu msimu uliopita itapungua msimu huu.

Hata hivyo Wenger anaripotiwa kuwania kuwasajili Sergio Busquets na Karim Benzema ili kuimarisha kikosi chake zaidi. Alexis Sanchez pengine ni nyota ambaye Wenger anamtumainia zaidi kwa sasa kwenye timu yake.

 

Mabao 16 aliyopachika msimu uliopita kwenye EPL huenda akayaongeza msimu huu. Pia uwepo wa Mesut Özil pamoja na Walcott na Carzola waliorefusha mikataba yao wiki iliyopita unaihakikishia Asenal makali yake ya siku zote kwenye eneo la kiungo.

 

ASTON VILLA

Aston Villa haijawahi kumaliza juu ya nafasi ya 15 kwa misimu minne mfululizo sasa huku msimu uliopita ikinusurika kushuka daraja baada ya kumaliza kwenye nafasi ya 17.

 

Kutokana na matokeo mabaya kocha Paul Lambert aliyeteuliwa Juni 2012 alitimuliwa Februari mwaka huu na akateuliwa Tim Sherwood.

 

Kwenye maandalizi ya msimu uliopita Villa ilisajili wachezaji watano na kuuza watano tu lakini kwa ajili ya maandalizi ya msimu huu tayari Sherwood ameshasajili wachezaji 9 mbaka sasa na 12 wametimka wakiwemo nyota wawili muhimu, Christian Benteke na Fabian Delph.

 

Kikosi kinasukwa upya na huenda Idrissa Gueye na Jordan Ayew waliosajiliwa hivi karibuni wataziba mapengo ya Delph na Benteke.

 

BOURNEMOUTH

AFC Bournemouth inashiriki EPL kwa mara ya kwanza msimu huu tangu timu hiyo ilipoanzishwa mwaka 1890. Mtu muhimu zaidi kwenye timu hii ni kocha Eddie Howe wa miaka 37.

 

Howe ameipandisha daraja Bournemouth mara tatu. Aliitoa ‘English League One’ mbaka ‘English League Two’ baadae ‘Football League Championship’, na sasa ameileta EPL.

 

Mafanikio hayo ya kushangaza yamemfanya atajwe kuwa kocha bora wa muongo wa ligi tatu za juu za Uingereza ukiitoa EPL.

 

Changamoto kubwa aliyo nayo ni kukosa uzoefu na EPL yeye mwenyewe na takribani wachezaji wake wote. Hata hivyo ameshasajili nyota kadhaa wazoefu wa ligi hii akiwemo golikipa Artur Boruc aliyetokea Southampton na mlinzi Sylvian Distin aliyetokea Everton.

 

CHELSEA

Timu hii ilishinda taji la EPL msimu uliopita ikiwa bado na michezo mitatu mkononi. Ikaingiza wachezaji sita kwenye kikosi bora cha EPL. Kocha Jose Mourinho akadai kuwa ‘11 ya kwanza’ ya Chelsea yote ilistahili kuwemo kwenye kikosi bora cha ligi hiyo.

 

Hii inaonyesha anajivunia na anakiamni kikosi chake kupita kiasi. Huwezi kutarajia mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Ni wazi kuwa Mourinho anarudi kutetea taji lake la EPL na kikosi kile kile kilichoshinda taji hilo kwa kishindo msimu uliopita.

 

Hata hivyo amewasajili golikipa Asmir Begovic kutoka Stoke City na mshambuliaji Radamel Falcao kutoka Monaco ili kuziba mapengo ya Peter Cech na Didier Drogba walioondoka kikosini.

 

CRYSTAL PALACE

Kwa mara ya kwanza Crystal Palace inashiriki EPL kwa misimu mitatu mfululizo. Kabla ya hapa ilishuka daraja kila ilposhiriki EPL. Alan Pardew alipoichukua timu hii Januari mwaka huu ilikuwa kwenye ukanda wa kushuka daraja ikiwa tayari imeshacheza michezo 21.

 

Akaiwezesha kumaliza kwenye nafasi ya 10 msimu uliomalizika. Huenda kocha huyu atafanya makubwa zaidi msimu huu. Hivi karibuni amefanikiwa kumnasa kiungo Yohan Cabaye kutoka PSG aliyewahi kuwa naye akiifundisha Newcastle United.

 

Huenda wawili hawa wataipeleka Crystal Palace kwenye nafasi tano za juu za EPL kama walivyofanya msimu wa 2011/12 wakiwa Newcastle. Vile vile Pardew amemsajili kwa mkopo mshambuliaj Patrick Bramford kutoka Chelsea ambaye msimu uliopita aliifungia Middlesbrough mabao 17.

 

EVERTON

Msimu uliopita Everton ilishika nafasi ya 11 ikiwa na alama 47 ambazo ni chache zaidi kukusanywa na timu hiyo kwa msimu ndani ya misimu kumi ilyopita ya EPL.

 

Hata hivyo kwenye msimu wa kwanza chini ya Roberto Martinez (2013/14) Everton ilikusanya alama 72 na kuweka rekodi ya alama nyingi zaidi kukusanywa na timu hiyo kwa msimu mmoja kwenye historia yake ndani ya EPL. Ndio maana Martinez anaendelea kuaminiwa.

 

Kikosini Everton imesheheni vipaji kama Jonh Stones, Steven Coleman, Tom Cleverley, Garry Barry, Kevin Mirallas, Romelu Lukaku na wengine. Lukaku aliifungia Everton mabao 16 kwenye msimu wake wa kwanza. Msimu uliopita akatupia 20. Everton chini ya Martinez ipo vizuri.

 

LEICESTER CITY

Msimu uliopita Leicester ilikuwa mkiani kwenye msimamo wa EPL kipindi cha Christmas. Hata hivyo wakamaliza kwenye nafasi ya 14 chini ya Nigel Pearson aliyetimuliwa mwezi Juni kutokana na sababu za kinidhamu.

 

Claudio Ranieri akateuliwa kuwa kocha mpya mwezi Julai. Ranieri amewahi kuzifundisha Chelsea, Valencia, Juventus, Roma, na klabu nyingine kubwa hivyo ana uzoefu uliopitiliza. Amekisifu kikosi cha Leicester kuwa kina wapambanaji baada ya kushiriki nao mazoezi kwa mara ya kwanza.

 

Tutarajie atawatumia vizuri wachezaji tegemeo wa Leicester wakiwemo Wes Morgan, Jeffrey Schulp na Leonardo Ulloa. Pia Leicester imemsajili mshambuliaji Shinji Okazaki anayeshika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji wa muda wote wa timu ya taifa ya Japan.

 

LIVERPOOL

Liverpool wanaingia kwenye msimu wa EPL bila Steven Gerrard aliyekuwa nahodha wao kwa zaidi ya miaka 10. Timu hii inatarajiwa kuingiza sura mpya nyingi kwenye 11 yake ya kwanza.

 

Wachezaji wapya kama Nathaniel Clyne, James Milner, Roberto Firmino na Christian Benteke wanaonekana kuwa na ubora unaotosha kabisa kuwaingiza moja kwa moja kwenye kikosi tegemeo cha Brendan Rodgers. Bado timu hii inahangaika kutafuta mbadala wa Luis Suarez.

 

Kwenye msimu wa mwisho Suarez akiwepo Liverpool ilifunga mabao 101 kwenye EPL huku Suarez akifunga 31 kati ya hayo. Msimu uliopita yakaporomoka hadi kufikia 52 huku kukiwa hakuna mchezaji aliyefikisha mabao 10. Huenda Benteke atakuwa suluhisho na kuipa mafanikio Liverpool.

 

MANCHESTER CITY

Manchester City tayari imewaongeza Raheem Sterling na Fabian Delph kikosini. Hata hivyo sidhani kama wataingia kwenye 11 ya kwanza moja kwa moja. Sterling atarajie changamoto kutoka kwa Nasri, Silva na Navas. Delph atarajie changamoto kutoka kwa Toure, Fernando na Fernandinho.

 

Hii ni ishara kuwa Pellegrini atakuwa na machaguo ya kutosha kumuwezesha kubadili kikosi kadri itakavyohitajika. Kiujumla kikosi cha timu hii ni kizuri hasa kwenye eneo la ushambuliaji linaloongozwa na Sergio Aguero aliyekuwa mfungaji bora wa EPL msimu uliopita akiwa na mabao 26.

 

Msimu uliopita City hawakuweza kutwaa ubingwa ingawa walikuwa ni timu pekee ilyoshinda michezo yake yote sita ya mwisho. Msimu huu wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.

 

MANCHESTER UNITED

United inajipanga kushindania ubingwa wa EPL ambao imeukosa kwa misimu miwili mfululizo kitu ambacho mara ya mwisho kilitokea kwenye misimu ya 2004/05 na 2005/06.

 

Bastian Schwensteiger, Morgan Schneiderlin, Memphis Depay, Matteo Darmian na golikipa Serge Romero ni wachezaji watano wapya kikosini.

 

Usajili huu umesifiwa na wengi lakini United inatakiwa kusajili pia mlinzi wa kati kwa kuwa ukuta wake umekuwa ukisuasua tangu kuondoka kwa Rio Ferdinand na Nemanja Vidic.

 

Pia ingawa Rooney anatarajiwa kucheza kama mshambuliaji wa kati bado kuna umuhimu wa kusajili mshambuliaji mwengine kwa kuwa Van Persie ameondoka. Tutarajie timu hii kuzipa changamoto ya kutosha Chelsea na Man City kwenye ubingwa wa EPL msimu huu.

 

NEWCASTLE UNITED

Newcastle inauanza msimu ikiwa na kocha mpya Steve McLaren aliyewahi kuzifundisha timu nyingi mashuhuri ikiwemo timu ya taifa ya Uingereza. Amewahi pia kushinda taji la ligi kuu ya Uholanzi msimu wa 2009/10 akiwa na FC Twente.

 

Msimu uliopita Newcastle iliishika nafasi ya 15 EPL na kuruhusu mabao 63 ambayo ni mengi kuliko timu yoyote ukiwatoa QPR walioshika mkia. Timu hii imemsajili Chancel Mbemba kutoka Anderletch ili asaidiane na nahodha Coloccini kupunguza idadi hiyo ya mabao msimu huu.

 

Kiungo Georginio Wijnaldum aliyeisadia PSV kushinda ligi kuu ya Uholanzi msimu uliopita na Aleksandar Mitrovic aliyeifungia Anderletch mabao 2o na kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Ubelgiji pia wamejiunga na Newcastle.

 

NORWICH CITY

Alex Neil alijiunga na timu hii Januari mwaka huu na kuirudisha EPL baada ya kukosekana kwa msimu mmoja. Aliiongoza Norwich kushinda michezo 17 na sare 5 kati ya michezo 25 tangu alipoichukua.

 

Ni kocha kijana kuliko wote EPL akiwa na umri wa miaka 34. Norwich ni timu yake ya pili kuifundisha baada ya Hamilton Academical ya Scotland.

 

Ameshasajili wachezaji wanne kwa ajili ya msimu huu akiwemo winga Robbie Brady aliyetua kwa paundi milioni 7 kutoka Hull City.

 

Wachezaji kadhaa wameondoka ila hakuna mchezaji tegemeo kati yao. Cameroon Jerome aliyeifungia timu hiyo mabao 21 msimu uliopita amebakia kikosini pamoja na nyota wengine tegemeo kama Nathan Redmond na Bradley Johnson.

 

SOUTHAMPTON

Southampton inaanza msimu ikiwa imewapoteza Morgan Schneiderlin na Nathaniel Clyne waliouzwa na Toby Alderweireld aliyerejea Atletico Madrid baada ya muda wa mkopo kuisha.

 

Pengine hili si tatizo kwa kocha Ronald Koeman kwani hata msimu uliopita wachezaji wengi tegemeo walikuwa wamehama na timu ikamaliza katika nafasi ya 6 kwenye EPL. Iliruhusu mabao 33 ambayo ni machache kuliko timu yoyote ukiwatoa Chelsea walioruhusu 32.

 

Walinzi wawili walioshiriki kuifanya kazi hiyo wameshaondoka na wamebakia nahodha Jose Fonte na Ryan Betrand.

 

Koeman amejaribu kuziba mapengo kwa kuwasajili walinzi Cedric Soares kutoka Sporting Lisbon na Cuco Martina kutoka FC Twente. Pia amejaribu kuziba pengo la Schneiderlin kwa kumsajili Jordy Classie kutoka Fayenoord.

 

STOKE CITY

Stoke City walikamata nafasi ya 9 EPL msimu uliopita wakiruhusu mabao 45 tu ambayo ni machache kuliko timu yoyote ukizitoa timu nne za juu na Southampton.

 

Hata hivyo golikipa wao mahiri Asmir Begovic ametimkia Chelsea na wamemsajili Shay Given kuziba pengo lake.

 

Pengo kubwa zaidi ni Steven N’zonzi aliyetimkia Sevilla. N’zonzi alitoa mchango mkubwa kwenye mafanikio ya timu hiyo msimu uliopita. Pengo lake huenda likazibwa na Van Ginkel aliyetua kwa mkopo kutoka Chelsea.

 

Glen Johnson na Ibrahim Affellay pia wametua Stoke. Maandalizi ya Mark Hughes yanatosha kuwaaminisha washabiki kuwa kocha huyu ataibakiza timu hii kwenye nafasi kumi za juu kwa mara ya tatu mfululizo msimu huu.

 

SUNDERLAND

Sunderland hawakuwahi kushuka daraja tangu walipopanda mara ya mwisho mwaka 2007. Msimu uliopita walinusurika kushuka daraja. Walikusanya alama 38 ambazo ni alama tatu 3 zaidi ya alama za Hull City walioshuka daraja.

 

Kocha Dick Advocaat anajiandaa kuiepusha timu hii na hatari ya namna hiyo msimu huu. Tayari amesajili wachezaji watano, wanne kati yao ni walinzi na kiungo mmoja. Kocha huyu anaonekana kudhamiria zaidi kwenye kuimarisha safu ya ulinzi.

 

Hata hivyo nadhani timu hii inahitaji mshambuliaji kwa kuwa msimu uliopita ilifunga mabao 31 na kuwazidi kwa mabao Burnley pekee.

 

Muda wa kusajili bado upo huenda Advocaat ataongeza mshambuliaji vinginevyo sioni namna ambavyo timu hii itabakia EPL msimu ujao.

 

SWANSEA CITY

Msimu uliopita ulikuwa wa mafanikio mno kwa Swansea chini ya kocha Garry Monk.

 

Swansea walimaliza kwenye nafasi ya 8 EPL mbayo ni ya juu zaidi kuliko misimu yote tangu walipopanda daraja mwaka 2011 huku wakikusanya alama 56 ambazo zimeweka rekodi ya alama nyingi zaidi kwenye historia ya timu hiyo kwenye EPL .

 

Mafanikio haya yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na usajili wa mlinda mlango Lucas Fabianski kutoka Arsenal, mlinzi Federico Fernandez kutoka Napoli na kiungo Gylfi Sigurdsson kutoka Tottenham.

Mwezi uliopita Monk amesaini mkataba mpya wa miaka mitatu kuendelea kuifundisha timu hiyo na tayari amesajili wachezaji kadhaa akiwemo Andre Ayew kutoka Marseile kwa maandalizi ya msimu huu.

 

TOTTENHAM

Ingawa ilimaliza kwenye nafasi ya 5 EPL msimu uliopita Tottenham haikuwa vizuri kwenye ulinzi.

 

Iliruhusu mabao mengi zaidi kati ya timu 13 za juu. Pochettino ameliona hilo na ameamua kutoa kitita cha paundi milioni 11.5 na kumvuta mlinzi Toby Alderweireld kutoka Atletico Madrid ili ashirikiane na mbelgiji mwenzie Jan Vertonghen kwenye safu ya ulinzi.

 

Alderweireld alionyesha kiwango cha juu akiwa kwa mkopo Southampton msimu uliopita. Kwenye ushambuliaji Harry Kane alionyesha ubora wa kushangaza kwa kutupia mabao 21 na akachaguliwa kwenye timu bora ya EPL.

 

Ni jambo zuri kwa washabiki wa Spurs kuwa dalili za mchezaji huyo kuhama hazipo tena na anajiandaa kwa msimu mwengine akiwa na jezi ile ile.

 

WATFORD

Quique Flores kwa mara ya kwanza anafundisha timu ya EPL. Baadhi ya timu alizowahi kufundisha awali ni Valencia, Benifica na Atletico Madrid ambayo aliiwezesha kushinda taji la ‘Europa League’ msimu wa 2009/10.

 

Safari hii anaifundisha Watford iliyorejea EPL baada ya kukosekana kwa takribani misimu nane. Flores ameshasajili zaidi ya wachezaji 10 mbaka sasa. Hata hivyo miongoni mwa nyota waliong’aa msimu uliopita wakiwa na timu hii na kuipandisha daraja hakuna aliyeondoka mbaka sasa.

 

Nahodha Troy Deeney na Odion Ighalo ambao kwa pamoja walifunga jumla ya mabao 41 wamebakia kikosini tayari kutumika na Flores kwenye kutimiza malengo ya kocha huyo aliyoyataja kuwa ni kuhakikisha timu hii inaendelea kuwepo kwenye EPL.

 

WEST BROMWICH

Said Berahino aliifungia West Brom mabao 21 msimu uliopita yakiwemo 14 ya EPL. Hata hivyo kocha wa timu hii Tony Pulis amemuongeza mshambuliaji Rickie Lambert kwenye kikosi.

 

Amedai kuwa Lambert atakuwa mfano kwa kijana anaechipukia Said Berahino na kumuwezesha mchezaji huyo kukomaa zaidi.  Mbali na Lambert pia Pulis amewasajili James McClean na James Chester.

Inaonekana Pulis hana mpango wa kusajili  wachezaji wengi na anakusudia kukitumia kikosi kilichopo.

Pulis wakati anaichukua timu hii Januari mwaka huu aiikuta kwenye nafasi ya 17 kwenye msimamo wa EPL na akafanikiwa kuifikisha kwenye nafasi ya 13.

Amedai malengo yake ni kupanda zaidi ya nafasi hiyo msimu huu wa EPL.

 

WEST HAM

West Ham msimu huu watautumia uwanja wao ‘Boleyn Ground’ kwa mara ya mwisho kabla ya kuhamia ‘Olympic Stadium’ msimu ujao. Wanaanza msimu wa EPL wakiwa na kocha Slaven Bilić.

 

Bilić ni kwa mara ya kwanza anafundisha timu ya EPL, ila aliwahi kuichezea timu hii mwaka 1996. Mwaka 2007 aliibania timu ya taifa ya England nafasi ya kushiriki michuano ya ‘Uefa Euro 2008’ baada ya kifunga timu hiyo 3-2 katika dimba la Wembley akiwa kocha wa Croatia.

 

Anakikuta kikosi cha West Ham kikiwa na nyota kama Diafra Sakho, Cheikhou Kouyaté, Enner Valencia na wengine. Kipimo chake cha kwanza ni dhidi ya Arsenal kwenye dimba la Emirates Jumapili hii.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Ronaldo ampa wakala kisiwa

Di Maria aelekea PSG