in , , ,

England bado kazi mbichi

*Tatizo kubwa ni beki ya kulia na kati

*Walio wingi ya kushoto wana udhaifu

 

Waingereza wanaweza kuwa na furaha kubwa baada ya kuwafunga Brazil mabao 2-1 kwenye mechi ya kujipima nguvu, lakini kazi bado ni kubwa.

Yapo masuala muhimu ya kuzingatia, ikiwa wanataka kuvuka bila wasiwasi kuziendea fainali za Kombe la Dunia mwakani, na pia kufanya vizuri huko.

Kocha wao, Roy Hodgson alifurahi sana kwa ushindi huu wa Wembley, akawaonesha wapinzani wake kwamba walikosea. Hakuwa chaguo la washabiki Waingereza.

Baada ya kuwafunga ‘Azzuri’ wa Italia kwenye mechi ya kirafiki iliyopita, walau wamepunguza machungu ya Wataliano hao kuwatoa kwenye michuano ya Euro 2012.

Kwa kuangalia yaliyopita, timu hii ya kocha mzalendo Hodgson ina mwelekeo sahihi, lakini zaidi imani inajengeka kwa wachezaji aina ya Jack Wilshere aliyetangazwa kuwa bora katika mechi hiyo.

Huyu ni kiungo wa Arsenal mwenye umri wa miaka 21 tu, lakini siku hadi siku ameonesha umahiri katika kucheza na pia kwenye kuwahamasisha wenzake, licha ya kuwa nje kwa majeraha kwa miezi 15.

Nahodha wa England, Steven Gerrard alisema kabla na baada ya mechi kwamba Wilshere ana nafasi ya kuja kuwa mchezaji bora zaidi England na hata duniani.

Ilikuwa mara ya kwanza wawili hao kuanza mechi pamoja, wakatoa ushindi wa kwanza dhidi ya Brazil tangu 1990, pale Garry Lineker alipowafunga Wabrazili kwa kichwa hapo hapo uwanjani Wembley.

Na hii ilikuwa mara ya kwanza England kuwafunga Wabrazili mabao mawili tangu 1984, kama mtakumbuka John Barnes alikokota mpira toka mbali na kufunga, kabla ya Mark Hateley kuweka bao la pili na Brazil kutoka nunge uwanjani Maracana.

Hata hivyo, ushindi huu dhidi ya Brazil si dhihirisho la ukamilifu wa idara zote za timu ya England, hivyo hata wakifuzu kwenda Brazil mwakani, kuna kazi kubwa ya kufanya.

Tukiangalia golini, licha ya kupangua penati ya Ronaldinho, kipa Joe Hart hajawa mahiri sana golini msimu huu kwa Manchester City, lakini hakuna ubishi kwamba ndiye namba moja England bado.

Anahitaji makali zaidi kwa ushindani ulio mbele yake. Lakini kuibuka kwa makinda Fraser Forster wa Celtic na Jack Butland wa Stoke City ni ishara kwamba katika siku zijazo England watakuwa na hazina ya kutosha ya magolikipa imara, na watapokezana, si kama sasa.

Katika ulinzi hakuna tatizo upande wa kushoto, maana yupo Ashley Cole wa Chelsea, mmoja wa mabeki bora zaidi wa kushoto duniani. Ukitaka mwenye kasi ya kupanda na kushuka, Leighton Baines wa Everton alidhihirisha uwezo huo jioni ile.

Kuna udhafu kidogo beki ya kulia; Glen Johnson wa Liverpool si mzuri katika kupanda na kushuka wala hakabi vyema kama Cole.

Msimu uliopita ilionekana kana kwamba Kyle Walker Tottenham Hotspurs angeichukua nafasi hiyo, lakini mara amepooza.

Watu wanajiuliza nani anafaa pale; labda Adam Smith wa Spurs atajiunga kwa safari ya Brazil, maana ameonesha vitu visivyo vya kawaida Millwall aliko kwa mkopo.

Tatizo kubwa kwa England ni katika ulinzi wa kati, kwani zama za kocha kuchagua nani wa kuchezesha kati ya John Terry, Rio Ferdinand, Ledley King au Jamie Carragher zimeshapita.

Waliopo sasa, akina Gary Cahill, Phil Jagielka, Joleon Lescott na Michael Dawson si wazuri kama hao niliowataja awali, na imedhihirika uwanjani.

Lakini utashangaa, Terry kang’atuka baada ya kuona anaandamwa na FA, Ferdinand haitwi kikosini bila sababu ya msingi na hao wengine wanatundika daluga tayari.

Iliyopo ni kuishi kwa matumaini tu, kwamba kizazi kijacho kitachipua walio bora na kuongeza mazoezi kwa waliopo ili kuepuka kichapo mechi zijazo.

Ukipepesa macho huku na kule, hata hivyo, unaona kwamba Steven Caulker amekuwa mzuri kwa Spurs msimu huu, lakini hajacheza mara nyingi bado. Pale Manchester United, Phil Jones na Chris Smalling ni bora lakini ndio hao wa kuandamwa na majeraha kila mara.

Pale Wembley, kiungo kilionekana kuwa idara bora zaidi, wachezaji wakitawala mpira dhidi ya Wabrazili, Wilshere aking’ara na Gerrard akisumbua kama vile hajafikisha umri wa miaka 32.

Tom Cleverley si mbaya alipocheza chini ya Hodgson, lakini kimsingi anahitajika mtu mwenye mbinu za ukabaji zaidi ili kupata uwiano unaotakiwa. Palikuwapo udhaifu kiasi kwa England, kwani waliruhusu mashambulizi ya kushitukiza kutoka kwa Brazil kupita katikati, japokuwa chini ya Hodgson, Gerrard amekuwa na nidhamu zaidi.

Scott Parker wa Spurs; Michael Carrick wa United na Gareth Barry wa Man City — wote umri unawatupa mkono, maana wamefika 30 tayari.

Huku ikiwa imebaki miezi 18 michuano ya Kombe la Dunia kuanza Rio De Janeiro, lazima kutafuta mwenye umri mdogo zaidi, ikizingatiwa kwamba Gerrard hatakuwa na ‘mapafu ya mbwa’. Si ajabu akaingia James Milner wa Man City.

Kwa upande wa ushambuliaji, Wayne Rooney wa United alionekana kujiamini sana eneo la kati. The Walcott wa Arsenal aliwasababishia matatizo makubwa Brazil kwenye beki yao ya kushoto.

Danny Welbeck alipwaya kiasi kwenye wingi ya kushoto, japokuwa alijaribu kuipigania timu sana. Itabidi Hodgson atafute mtu mwingine aliyezoea pale.

Rooney angefaa pale, lakini Welbeck akirudi kati hatasaidia sana maana si mpachika mabao wa aina ya Rooney, na Hodgson hana sababu ya kumpunguza kasi mpachika mabao wake.

Habari njema kwa England ni kwamba wanao wachezaji wengi wanaoweza kutanua kulia na kushoto, na mmoja wao ni Aaron Lennon anayetisha upande wa kushoto pale Spurs.

Kuna akina Ashley Young na Adam Johnson, ambao japokuwa hawapo fiti sana kwa sasa, wana kipaji. Lakini pia wapo wadogo zao, tena mahiri, akina Alex Oxlade-Chamberlain, Raheem Sterling na Wilfried Zaha.

Ukitazama wachezaji hao, unabaini wazi kwamba nguvu ya England si ajabu ikawa kwenye wingi, sasa unabaki kushangaa kulikoni Welbeck na baadaye Milner wachezeshwe.

Bado kuna majibu mengi yanatakiwa kutafutwa kwa maswali, kwa maana Waingereza wamechoka kukwamia njiani kila mashindano makubwa yanapokuja.

Wanataka kuona wakivuka kwenda Brazil, halafu wabaki huko hadi mwisho, si kurudi nyumbani mapema kila wakati inapokaribia au kufika robo fainali.

Ni juu ya Hodgson kujenga na kuimarisha kikosi chake, ili kiwe na soka ya ushindani na ya kuvutia kwa washabiki kutazama. Wapo wanaosema angepewa kazi hii miaka mingi iliyopita labda England wangekuwa mbali.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

University games get underway in Dar

Gharika Manchester City