in , , ,

Di Canio akata ngebe


*Awagaragaza Newcastle baada ya miaka 13
*Man City wawaua Chelsea na kutinga fainali

 

Kocha mpya wa Sunderland, Paolo Di Canio amekata ngebe za wapinzani wake, kwa kuibuka na ushindi wa kishindo dhidi ya Newcastle United.
Katika mechi ya watani wa jadi wa kaskazini mashariki mwa England iliyovuta hisia kwa muda mrefu, Sunderland waliparura Newcastle mabao 3-0.
Di Canio kwake ilikuwa mechi ya pili, tangu alipochukua nafasi ya Martin O’Neill aliyefukuzwa kwa mwenendo mbaya wa timu. Hata hivyo, Di Canio alipingwa na baadhi ya washabiki, kutokana na kauli ya zamani kwamba yeye ni fashisti, ambayo hata hivyo ameikana.
Kocha huyo ndiye aliyeonekana kujawa furaha kupita kiasi, ambapo bao la kwanza alishangilia kwa kukimbia na kuruka juu; la pili kwa kurukia wachezaji na la tatu kukimbia na kuteleza kwa magoti uwanjani.
Ilikuwa faraja ya aina yake kwa washabiki wa Sunderland pia, kwani ulikuwa mwaka wa 13 bila kuweza kushinda katika uwanja wa St James’ Park, nyumbani kwa Newcastle.
Ushindi huo umewaweka Sunderland katika nafasi nzuri ya kuepuka kushuka daraja, na kuwavuta Newcastle kwenye vita hiyo.
Bao la kwanza la Sunderland lilifungwa na Stephane Sessegnon dakika ya 27, la pili Adam Johnson dakika ya 74 na la tatu David Vaughan dakika ya 82.
Jitihada za kocha wa Newcastle, Alan Pardew kubadilisha mchezo hazikuzaa matunda, kwani ngome ya Sunderland ilikuwa ngumu kupenya, huku wakiendelea kutafuta mabao, tofauti na mfumo wa zamani ambapo walichelea kushambulia.
Ilionekana kana kwamba ilikuwa sahihi kufukuzwa O’Neill aliyekuwa akilaumiwa kutohangaika uwanjani kubadili mchezo mambo yanapoharibika, kiasi cha kwenda mechi tisa bila ushindi.
Sunderland sasa wanashika nafasi ya 15 wakiwa na pointi 34, wakati Newcastle ni wa 13 na pointi zao 36.

MAN U UBINGWA BADO POINTI SABA

20130414-204138.jpg

Vinara wa Ligi Kuu ya England (EPL), Manchester United wamesogea hatua muhimu kuuelekea ubingwa, ambapo sasa wanatakiwa kupata pointi saba zaidi.
United waliofungwa mechi iliyopita na mahasimu jirani wao, Manchester City, waliamka Jumapili hii kwa kuwafunga Stoke City mabao 2-0 walipocheza katika Uwanja wa Britannia.
Man U wanaotafuta taji la 20 la ubingwa wa England walipata bao la kwanza kupitia kwa Michael Carrick dakika ya nne tu, na lile la pili kwa tuta lililovurumishwa na Robin van Persie aliyekuwa akikabiliwa na ukame wa mabao katika mechi 10.
United sasa wamefikisha pointi 80 wakati Stoke wamejeruhiwa kwa kutupwa eneo la hatari ya kushuka daraja, kwani wanashika nafasi ya 16 kwa pointi zao 34.

MAN CITY FAINALI KOMBE LA FA

ba

Katika nusu fainali ya pili ya Kombe la FA, Manchester City wamewakamua Chelsea mabao 2-1 katika Uwanja wa Wembley.
Katika mechi kali, ya kukamiana na ya kuvutia, City walipata mabao yao kupitia kwa Samir Nasri dakika ya 35 na Sergio Aguero dakika ya 47.
Chelsea wenye ratiba ngumu ya mechi nyingi (za EPL, Ligi ya Europa na FA walikofutwa sasa) hawakuonesha uhai kipindi cha kwanza, tatizo likionekana kwenye kiungo na utengenezaji nafasi za kufunga.
Hata hivyo, baada ya kufungwa bao la kwanza, mabingwa hao watetezi walijaribu kucharuka lakini hawakufurukuta, kwani nahodha wa Man City, Vincent Kompany aliongoza vyema ulinzi.
Hata hivyo, juhudi binafsi za Demba Ba zilizaa matunda kwa kufunga bao zuri la kushitukiza, lakini halikutosha kuusogeza mchezo kwenye dakika za nyongeza.
Man City watavaana na Wigan katika fainali uwanjani Wembley Mei 11. Wigan waliwatoa Milwall katika nusu fainali ya kwanza Jumamosi hii, kwa kuwafunga mabao 2-0.

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

WERE THE FIRST GAMES HELD IN EGYPT?

Arsenal wazuiwa