in , , ,

De Gea, Van Gaal hapakaliki

Karim Benzema, inasemekana yuko njiani kwenda Arsenal....

 

*Terry tumbo joto, Chelsea wamtaka Varane  

 

*Wenger anaendelea kutafuta mshambuliaji

 

Uhusiano wa kipa wa Manchester United, David de Gea na kocha wake, Louis van Gaal unaelezewa kuharibika ka kiasi kikubwa kutokana na kocha huyo kumtupa nje ya kikosi chake.

 

De Gea ametazama mechi zote za tatu za United akiwa jukwaani na hakupewa hata nafasi ya kuwa na wachezaji wa akiba, maelezo yanayotolewa na kocha yakiwa kwamba hawezi kujituma kwa sababu anafikiria mambo ya Real Madrid.

 

Wakati Mhispania huyo akitaka kurudi kwao anakotakiwa na Real, United wanasema kwamba hawatamuuza mchezaji huyo licha ya kubakisha msimu mmoja tu kiasi kwamba anaweza kuondoka kama mchezaji huru kiangazi kijacho.

 

De Gea anaona kwamba hali ilivyo klabuni hapo itakuwa ngumu kufanya kazi na kocha huyo ambaye alimwekea maneno mdomoni kwamba alisema hataki kucheza mechi mbili za kwanza ilhali alikuwa na kiu ya kurejea langoni.

 

Chanzo cha habari kilicho karibu na De Gea kimenukuliwa kikisema: “David haelewani tena kabisa na Van Gaal – uhusiano wake na kipa wa makocha, Frans Hoek ndio umetibuka kabisa.” Van Gaal alidai kwamba De Gea alimwambia kocha huyo wa makipa kwamba hakuwa na shauku ya kucheza, ndipo wakaamua kumpumzisha na nafasi yake kuchukuliwa na Sergio Romero.

 

Pia Victor Valdes aliyesajiliwa akiwa mchezaji huru naye ni kana kwamba ametupiwa virago na hutazama mechi akiwa jukwaani, baada ya kumchefua Van Gaal kwa kukataa kufanya mazoezi na kikosi cha pili. Alimwambia anaweza kuondoka, na anasubiri timu ya kumnunua, lakini ana mkataba mnono hapo, hivyo anakaa bure.

 

Zipo habari kwamba Pedro Rodriguez aliyekuwa ajiunge na Man United kutoka Barcelona alibadilisha mawazo baada ya kushauriwa ama abaki Camp Nou au aende klabu nyingine ya Ligi Kuu ya England, kwani Van Gaal angeweza kumharibia maisha kutokana na hasira na ukali wake.

 

Kipa wa zamani wa Manchester United, Edwin van der Sar, ambaye sasa ni mmoja wa wakurugenzi wa Ajax ya Uholanzi anasema anafahamu fika sintofahamu iliyoibuka baina ya kocha na mchezaji huyo na alikuwa na haya ya kusema kumhusu:

 

“Ni wazi kwamba kuna mengine mengi zaidi yanaendelea chini chini; kuna kitu kati ya Louis na De Gea. “Nina wasiwasi kwamba De Gea atakuwa na kipindi kigumu sana cha miezi 10 ijayo. Nikiwa mwajiriwa na kipa wa zamani wa klabu hiyo, nahisi ni kitu cha kuogofya kuona makipa wazuri watatu – De Gea, Anders Lindegaard na Victor Valdes – wakiwa jukwaani wakiangalia mpira wa Man United.

 

“Huyo Sergio Romero alikuwa mchezaji huru ambaye hajacheza mechi ya ligi kiushindani hasa katika miaka miwili, lakini ndiye anapewa nafasi ya kwanza. Jina la Cillessen linatajwa kama mtu wa kuchukua nafasi ya De Gea, lakini nikiwa mkurugenzi hapa Ajax, najitahidi kuhakikisha kwamba mchezaji wetu bora zaidi anabaki.”

 

TERRY AHOFU..

Raphael
Raphael anatajwa kuwa yuko njiani kwenda Chelsea…..

Nahodha wa Chelsea, John Terry, 34, anahofia hatima yake ndani ya klabu hiyo, baada ya kusikia tetesi kwamba kocha Jose Mourinho anafikiria kumsajili beki wa kati wa Real Madrid, Raphael Varane, 22.

 

Mourinho alimwondosha Terrywakati wa mapumziko  kwenye kikosi chake kilichofungwa na Manchester City 3-0, badala yake akamwingiza Kourt Zouma, na juzi alimtaja kuwa mmoja wa wachezaji sita waandamizi waliochemsha msimu huu.

 

Chelsea wameshapeleka dau mara tatu Everton kwa ajili ya kumsajili beki wa kati, John Stones, lakini pia wametuma barua Real Madrid kuhoji uwezekano wa kumsajili Varane kiangazi hiki. Varane amekuwa kipaumbele cha Mourinho lakini Madrid hawaelekei kumuachia.

 

Terry amekuwa akijifua zaidi, akiamini kwamba anaweza bado kuwika kama msimu uliopita, ambapo alicheza dakika zote za mechi zote za ligi kuu. Makocha waliomtangulia Mourinho, Rafa Benitez na Andre Villas-Boas walikuwa wakimtupa benchi Terry.

 

WENGER: HAWATAKI KUTUUZIA MSHAMBULIAJI NYOTA

Karim Benzema, inasemekana yuko njiani kwenda Arsenal....
Karim Benzema, inasemekana yuko njiani kwenda Arsenal….

 

 

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema uchache wa washambuliaji mahiri wenye viwango vikubwa kimataifa na klabu zenye wachezaji wa aina hiyo kutotaka kuwauza kunawafanya Arsenal kushindwa kusajili jina kubwa hadi sasa.

 

Hata hivyo, amesema uwapo wa vipaji vingi, hasa katika klabu za Barcelona na Real Madrid kiasi cha kutoa ushindani wa namba kwa wachezaji kunaweza kuwanufaisha Arsenal, kama ilivyotokea kwa kuwapata Alexis Sanchez kutoka Barca na Mesut Ozil kutoka Real, na sasa wote wana umri wa miaka 26.

 

Pamekuwapo habari kwamba Arsenal wanataka kumsajili mshambuliaji wa kati wa Real Madrid, Mfaransa Karim Benzema, ambapo baadhi walidai dili lingekamilika wiki iliyopita, wengine wakisema huenda mwanzoni mwa wiki hii, lakini hadi sasa ni kimya.

 

Zilikuwapo taarifa pia kwamba Arsenal walikuwa wakiulizia uwezekano wa kumpata Edinson Cavani wa Paris Saint-Germain (PSG) au hata mshambuliaji mwenzake, Zlatan Ibrahimovic aliyesema angeushangaza ulimwengu juu ya klabu atakayohamia.

 

Alipata kukaribia kucheza Arsenal miaka kadhaa iliyopita, akafanya nao mazoezi akiwa tayari ameshapewa jezi, lakini akatimka baada ya Wenger kumtaka aingie kwenye majaribio halisi kama angefaa, Ibrahimovic akasema yeye si mtu wa maonesho bali alikuwa ameenda kucheza moja kwa moja.

 

Mkongwe wa Arsenal, Ray Parlour ameunga mkono majaribio ya kuwasajili Benzema na Cavani, japokuwa jitihada zikifanyika uwezekano kwa Arsenal ni kupata mmoja wao tu.

advertisement
Advertisement

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Man United wabanwa

Man City safi