in , , ,

‘De Gea hataki kucheza’

 

*Man U wamsubiri Pedro*

 

 

Kipa namba moja wa Manchester United, ameonesha kwamba hayupo katika hali ya kuchezea timu hiyo, na hayo yamebainishwa nay eye mwenyewe pamoja na kocha wake, Louis van Gaal.

 

Mdachi huyo anatarajiwa pia kumweka kando De Gea katika mechi ya leo watakapokaribishwa Villa Park kukipiga na Aston Villa.

 

De Gea anatakiwa na Real Madrid, timu ya jiji alikozaliwa, lakini United wamekuwa wakimwekea ngumu kuondoka, vinginevyo wakisema wapewe beki wa kati wa Madrid, Sergio Ramos, ambaye hata hivyo anakaribia kusaini mkataba mpya ili abaki Santiago Bernabeu.

 

Aliwaambia wafanyakazi wa klabu ya Manchester United kwamba hakuwa na shauku ya kucheza tangu mechi ya fungua dimba, ambapo waliwafunga kwa tabu Tottenham Hotspur 1-0 wakicheza nyumbani Old Trafford.

 

De Gea, 24, ambaye amekuwa mchezaji bora wa timu hiyo kwa misimu miwili alimwambia pia kocha wa makipa, Frans Hoek hayupo tayari kwa asilimia 100 kucheza. Van Gaal alisema kwamba De Gea anayemwona sasa si yule aliyemjua msimu uliopita, ndio maana hakuwa hata kwenye benchi la timu katika mechi ya kwanza.

 

Kipa wa kimataifa wa Argentina, Sergio Romero ndiye alianza golini, ikiwa ni mara yake ya kwanza. Van Gaal amesema kwamba huchukua uamuzi baada ya kujadiliana na wenzake, kwa sababu hafanyi kazi peke yake.

 

“Sifanyi kila kitu peke yangu. Ninao makocha wawili wasaidizi na kipa wa makocha. Frans (Hoek) alikuwa na kikao na David De Gea na anakubaliana kabisa na uamuzi wangu,” akasema Van Gaal na kuongeza kwamba walimwangalia vyema De Gea kwenye mazoezi na kubaini kipa huyo wa zamani wa Atletico Madrid amebadilika.

 

Anasema Hoek alimuuliza De Gea iwapo alikuwa anataka kucheza naye akamjibu kwamba hakutaka, hivyo hawaoni sababu ya kumweka kikosini. Hata hivyo, baadaye klabu ilitoa ‘ufafanuzi’ juu ya kauli hiyo, ikieleza kwamba De Gea hakusema ‘hapana’ bali kwamba hakuwa tayari kwa asilimia 100.

 

United wanang’ang’ania kutomuuza kipa wao aliyewaokoa msimu uliopita kufungwa mabao mengi lakini kwa kuwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, wanacheza bahati nasibu kwani asiposaini mkataba mpya ataondoka kama mchezaji huru na United hawatapata hata senti tano.

 

Van Gaal ameashiria kwamba atamsajili mshambuliaji wa Barcelona, Pedro, kwa sababu anafaa kwenye kikosi chake kutokana na kuwa na kasi lakini pia anajua kujipenyeza katikati ya wachezaji wa timu pinzani na kufunga mabao.

 

Alisema anahitaji mchezaji wa aina hiyo ili amsajili kabla ya msimu wa usajili kumalizika, japokuwa amepata pia kusema kwamba hawalazimiki kuongeza mshambuliaji kwa vile anao wengi wazuri.

 

Pedro, 28, ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Hispania amewaambia Barcelona angependa kuondoka iwapo hangepata muda mwingi wa kucheza. Anabaniwa fursa ya kucheza kwa sababu Barca wanao Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar katika mstari wao wa ushambuliaji.

 

Hata hivyo, Van Gaal alipoulizwa iwapo Pedro atajiunga nao, aliwataka wanahabari wamuulize Pedro na si yeye kwa sababu hawezi kusema mambo hayo kabla hajasaini mkataba.

 

“Muulizeni Pedro, si mie. Sitaji chochote kabla hajasaini. Akishasaini nitakuja kwenu na kuwaambia; ‘jamani, Pedro huyu hapa’. Hali hiyo bado haijakamilika kwa hiyo hatuna budi kusubiri,” akasema Mholanzi katika hali ya kuwa na matumaini ya kumpata.

 

Van Gaal amesema kwamba angependa kuona Wayne Rooney akifunga mabao zaidi ya 20 msimu huu. Amewaondoa kikosini mwake Robin van Persie aliyemuuza Uturuki na kumrejesha Monaco, Radamel Falcao ambaye hata hivyo ametwaliwa na Chelsea.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Afrika na ushabiki EPL

Man U waangusha moja tena