in , , ,

DE BRUYNE NDIYE BORA ZAIDI MPAKA SASA

Ni msimu wa pili wa Pep Guardiola ndani ya Manchester City tangu ajiunge na matajiri hao akitokea Bayern Munich ya Ujerumani. Safari hii timu yake ni moto wa kuotea mbali ikiwa haijapoteza mchezo wowote mbaka sasa kwenye mashindano yoyote. Wapo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England wakiwazidi Manchester United walio kwenye nafasi ya pili kwa alama tano na wanao mchezo mkononi utakaopigwa leo Jumatano dhidi ya Southampton.

Matajiri hawa wa Etihad tayari wana mabao 44 ambayo ni mengi kuliko timu nyingine yoyote ya Ligi Kuu ya England. Orodha ya wachezaji 7 wenye mabao mengi zaidi inayoongozwa na Mohamed Salah wa Liverpool mwenye mabao 10 inao wachezaji watatu wa Manchester City. Hao ni Sergio Aguero mwenye mabao 9, Raheem Sterling mwenye mabao 9 na Gabriel Jesus mwenye 8 pia.

Nini siri kubwa ya uwezo huu mkubwa wa kufunga mabao walio nao Manchester City? Sababu zipo nyingi lakini kubwa na ya muhimu zaidi ni Kevin De Bruyne. Roho ya kikosi cha Pep Guardiola. Mchezaji anayepiga pasi mbili mbaka tatu zisizowezekana kwenye karibu kila mchezo anaocheza. Baadhi ya wachezaji humaliza maisha yao ya soka bila kupiga angalau pasi moja tu ya pasi ngumu anazopiga Kevin De Bruyne.

De Bruyne anayecheza kati zaidi anaifanya kazi ya viungo wa pembeni na washambuliaji wa Manchester City kuwa rahisi mno. Pasi safi ya bao, pasi ya ajabu kabla ya pasi ya bao au pasi nzuri ya hatari ya namna nyingine ndivyo vitu utakavyoviona kutoka kwa Mbelgiji huyu kwenye kila mchezo atakaokuwemo uwanjani. Raheem Sterling, Leroy Sane, Sergio Aguero, David Silva na Gabriel Jesus wanang’arishwa na De Bruyne.

Kwenye orodha ya wachezaji waliopiga pasi nyingi za mabao anazidiwa na David Silva pekee ambaye anazo pasi 8 za mabao mbaka sasa wakati De Bruyne anazo 6. Hata hivyo ukitazama vipengele vingine vya takwimu na namna Kevin De Bruyne anavyorahisisha zaidi mashambulizi ya Manchester City utakubali kuwa Silva ameachwa nyuma mno kiubora msimu huu na De Bruyne.

Kiungo huyu wa zamani wa Chelsea ndiye mchezaji aliyetengeneza nafasi nyingi zaidi msimu huu akiwa ametengeneza nafasi 34 huku 6 pekee zikiwa zimezaa mabao. Ni kinara wa pasi za kupenyeza na kuitangulia safu ya ulinzi ya timu pinzani akiwa amepiga pasi 18 za namna hiyo mbaka sasa ambapo anayemfuatia ni Christian Eriksen wa Spurs mwenye pasi 10 za namna hiyo. Manchester City inang’arishwa na Kevin De Bruyne.

Paundi milioni 55 walizotoa Manchester City kumnyakua nyota huyu wa timu ya taifa ya Ubelgiji kutoka Wolfsburg ya Ujerumani unaweza kuziona ni pesa kidogo mno unapotazama kazi anayoifanya uwanjani msimu huu. Ukirudi nyuma zaidi na kukumbuka kuwa Jose Mourinho akiwa Chelsea alimuuza kwa ada ya paundi milioni 18 pekee unaweza kutokwa na machozi. Pengine kwa wakati huo hakuwa na dalili za kuja kuwa na ubora huu. Lakini jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la msingi.

Wapo wanaomtaja Mohamed Salah kuwa ndiye aliyeonesha kiwango zaidi mbaka sasa. Kuwa kinara wa mabao ndicho kinachowapa ujasiri wa kutamka maneno haya. Hatuwezi kupima kiwango cha kiungo kwa idadi ya mabao na zaidi ya hapo thamani ya mambo aliyofanya nyota huyu wa Manchester City mbaka sasa ni zaidi ya hayo mabao 10. De Bruyne ndiye mchezaji bora zaidi mbaka sasa wa EPL msimu huu. Akiendelea na moto huu hakuna wa kumzuia kunyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa EPL.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

José Mourinho: NI LAZIMA AWATAWALE WABABE ILI KUPATA UBINGWA

Tanzania Sports

MANCHESTER UNITED ILITUONESHA UDHAIFU WA ARSENAL