in , , ,

CONTE ALIWAZA SEHEMU AMBAYO HATUKUIAMINI AWALI

Kwenye mechi kumi (10) kabla ya jana alikuwa amefanikiwa kufunga
magoli mawili (2)pekee, hapana shaka tangu kifo cha mama yake kiwango
chake kilikuwa cha kupanda na kushuka.

Hakuwahi kusimama kwenye kiwango bora kwa muda mrefu mara baada ya
mama yake kuachana naye na kwenda kwenye makazi yake ya milele.

Alikaa darajani akiwa mpweke sana, ule msaada aliouonesha kwenye msimu
ambao Leicester City ( 2015/2016) ulipungua kwa kasi kubwa sana, msimu
huo alionekana ndiye mwenye msaada mkubwa zaidi kwenye timu mara.

Kwa mara nyingine jana alisimama kama mtu mwenye msaada mkubwa kwenye timu.

Willian Borges da Silva jana alianza kwenye kikosi cha Antonio Conte
ambacho kilirudi kwenye mfumo wake wa msimu uliopita wa 3-4-3, wakati
wapinzani wao Barcelona walicheza mfumo wa 4-3-3.

Lakini kulikuwa na mabadiliko ya kimfumo kwa kila timu kutokana na
hali ilivyokuwa inabadilika ndani ya mchezo.

Mfano, Chelsea walipokuwa wanazuia walikuwa wanatumia mfumo wa 5-4-1.
Ambapo Marcus Alonso na Victor Moses walikuwa wanarudi nyuma kuungana
na mabeki watatu na kuongeza idadi ya watu watano nyuma, huku
wakimwacha Hazard mbele.

Barcelona walikuwa wanatumia mfumo wa 4-3-3 wakati wanashambulia,
lakini walipokuwa hawana mpira Iniesta alikuwa anarudi katikati
kuongeza idadi ya wachezaji na kutengeneza mfumo wa 4-4-2 wenye umbo
la Diamond.

Wapi Chelsea walifanikiwa wakati wakujilinda?

Moja ya silaha kubwa ambayo Barcelona wako nayo kwa muda mrefu na
wanaitumia bila kuisha makali ni Lionel Messi, jana alikuwa anashuka
chini katikati, kushuka kwake chini walikuwa wanatarajia beki mmoja wa
Chelsea kushuka naye kumkaba ili Chelsea watengeneze uwazi eneo la
nyuma , uwazi ambao ungetumiwa na Luiz Suarez, lakini kila Lionel
Messi alipokuwa anashuka katikati hakuna beki wa Chelsea aliyekuwa
anashuka naye.

Hali hii ilisababisha eneo la nyuma la Chelsea kutokuwa na uwazi muda
mwingi mwa mchezo, ndiyo maana wakati Barcelona walipokuwa na mpira
katika eneo la Chelsea ilikuwa ngumu kwao kupenyeza eneo la kumi na
nane kwa sababu hakukuwa na uwazi wa kupitishia mipira.

Kipi kilisababisha Chelsea kusawazishiwa?

Moja ya faida kubwa waliyokuwa nayo Barcelona ni wao kuanzia kukabia
juu, hali ambayo ilisababisha mabeki wa Chelsea kufanya makosa na
kupoteza umiliki mpira.

Mfano goli la Lionel Messi , Chelsea walilazimishwa kufanya makosa
kutokana na Barcelona kukabia juu kitu ambacho kilimpelekea Andreas
Christensen kupoteza umiliki wa mpira na Barcelona kuwaadhibu Chelsea.

Kipi kilisababisha Chelsea kutangulia kufunga goli?

Wakati Barcelona wakinufaika na kukabia juu, Chelsea walikuwa
wananufaika na wao kuwa na wachezaji wenye kasi (pace) kule mbele,
kitu ambacho kilikuwa kinawapa faida ya wao kulazimisha kufanya
mashambulizi kwa kasi.

Eden Hazard ndiye alikuwa funguo la goli la Chelsea , alicheza kama
false 9 mara nyingi alikuwa anakuwa huru kushuka chini na
kuwalazimisha mabeki wa Barcelona kutengeneza uwazi eneo la nyuma,
uwazi ambao mara nyingi ulikuwa unatumiwa na Willian.

Mfano kabla hajafunga goli, alipiga mashuti mawili yaliyogonga mwamba,
wakati anapiga mashuti hayo alikuwa huru kwa sababu alikuwa sehemu
ambayo kulitengenezwa uwazi uliotokana na Hazard kushuka chini, hata
goli la kwanza alilofunga, kafunga akiwa eneo ambalo ni huru na
alitumia uwazi ulioachwa na mabeki wa Barcelona.

Jana Willian alikuwa ndiye nyota wa mchezo na karata ya Conte kuamini
miguu ya Samba aliichanga vyema, wengi wanaweza kuongelea kwa ukubwa
na upana kuhusu Lionel Messi kuvunja mwiko wa kutoifunga Chelsea baada
ya michezo nane , lakini kiwango cha Willian ndicho kitu kizito
kinachostahili kuongelewa lakini kwa sababu kimefanywa na mtu mwepesi
watu watakichukulia kiwepesi

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Singida United, anzeni walipokosea Mbeya City

Tanzania Sports

ZANZIBAR WALIPATA FURAHA CECAFA, AIBU WAMEIPATA CAF