in , , ,

Chelsea wawafyatua Palace

*Tottenham sare na Everton*

Ilikuwa ni faraja kwa Chelsea kupata ushindi mzuri wa 3-0 dhidi ya
Crystal Palace, timu ambayo kwa siku za karibuni imekuwa ikifanya
vyema kwenye Ligi Kuu ya England tofauti na The Blues.

Wakiongozwa na kocha wa mpito, Guus Hiddink, Chelsea walipata mabao
yao kupitia kwa Wabrazili Costa, Willian na Diego Costa aliyemaliza
ukame wa mabao wa kitambo sasa. Huu ulikuwa ushindi wa kwanza chini ya
kocha huyo.

Kwa mwenendo wao, baada pia ya kutoshana nguvu na Manchester United
kabla, kocha Hiddink anasema kuna uwezekano kwa kikosi chake kupata
moja ya nafasi nne za juu mwishoni mwa msimu.

Kwa ushindi huo, Chelsea wamevuka ukanda wa kushuka daraja kwa pointi
sita, lakini bado wapo kwenye nafasi ya mbali kutoka juu – 14, baada
ya kuambulia pointi 23 katika mechi 20. Palace waliokosa wachezaji
wake muhimu wapo katika nafasi ya saba na kocha Alan Pardew anaamini
kwamba wanaweza kuimarisha kikosi katika dirisha hili dogo la usajili.

TOTTENHAM SARE NA EVERTON

wachezaji wakitoshana nguvu katika sare hiyo
wachezaji wakitoshana nguvu katika sare hiyo

Tottenham Hotspur wamefanikiwa kujishindilia kwenye nafasi ya nne
katika msimamo wa ligi baada ya kupata sare ya 1-1 na Everton hivyo
kufikisha pointi 36. Wakicheza ugenini, Spurs walifungwa bao la kwanza
na mchezaji wao wa zamani, Aaron Lennon katika dakika ya 22.

Pamoja na bao hilo, Spurs ndio waliokuwa wakicheza vyema na kutawala
katika kipindi cha kwanza ambapo Harry Kane na Ben Davies
wakishambulia kwa kasi mipira yao iligonga mwamba.

Alikuwa ni mchezaji ambaye kiwango chake kinapanda, Dele Alli
aliyedhibiti vyema pasi ndefu ya Toby Alderweireld na kukwamisha mpira
wavuni kwa kiki ya chini chini iliyomshinda nguvu kipa Mmarekani, Tim
Howard katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza.

Everton walianza vyema kipindi cha pili na kulitia shinikizo lango la
Spurs, ambapo kipa wa Spurs, Hugo Lloris alifanya kazi ya ziada kuokoa
kiki ya Muhamed Besic aliyopiga kutoka yadi 25 na baadaye Romelu
Lukaku wa Everton akashindwa kuitendea haki majalo ya Gerard Deulofeu
ambayo alitarajiwa kuiingiza kimiani.

Msimamo wa ligi unaonesha kwamba Arsenal ni vinara kwa pointi 42
wakifuatiwa na Leicester wenye 40, Manchester City 39, Spurs 36, Man
United 33, West Ham 32, Palace 31, Liverpool 30, Watford 29 sawa na
Stoke.

Everton wamefikisha pointi 27, West Bromwich Albion 26, Southampton
24, Chelsea 23 sawa na Norwich; Bournemouth 21, Swansea 19, Newcastle
17, Sunderland 15 na Aston Villa nane.


LEICESTER WAPATA PIGO LA VARDY

Anatakiwa afanyiwe upasuaji
Anatakiwa afanyiwe upasuaji

Leicester waliotesa kwenye uongozi wa ligi wakati wa Krismasi na
kuwashangaza wengi kwa kuwafunga vigogo, wamepata pigo baada ya
mshambuliaji wao hatari, Jamie Vardy kuumia na atakaa nje kwa walau
wiki mbili.

Mshambuliaji huyu wa kimataifa wa England anatarajiwa kufanyiwa
upasuaji mdogo eneo la karibu na paja. Amekuwa katika kiwango kizuri
msimu huu na amewafungia Foxes mabao 15 yaliyowawezesha kuwa wa pili
katika msimamo wa ligi hivi sasa.

Mchezaji huyu wa zamani wa Fleetwood Town mwenye umri wa miaka 28
alicheza dakika zote 95 katika mechi waliyokwenda suluhu na
Bournemouth Jumamosi hii.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Arsenal bado kileleni

Tanzania Sports

Zidane kocha mpya Madrid