*Spurs waangushwa na Fulham

*Newcastle wanyolewa na Wigan

 

Chelsea wamebisha hodi nafasi ya tatu Ligi Kuu ya England (EPL), baada ya kupata pointi tatu, huku washindani wao, Tottenham Hotspurs wakipoteza pointi kama hizo muhimu.

Wakicheza nyumbani Stamford Bridge, Chelsea waliwatuliza washabiki wao kwa kuwanyuka West Ham United mabao 2-0.

Ilikuwa siku muhimu kwa Frank Lampard, kwani alifunga bao lake la 200 kwa klabu, alilolisubiri muda mrefu kutokana na ama kushindwa kufunga au kutochezeshwa.

The Blues walitawala mchezo huo, ambapo bao la pili lilifungwa na Mbelgiji Eden Hazard na kumpa furaha Rafa Benitez ili aepuke kelele za maudhi kutoka kwa washabiki wa Chelsea.

Spurs wakicheza nyumbani White Hart Lane, waliwachefua washabiki wao kama ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu, baada ya kukubali kichapo kutoka kwa Fulham.

Alikuwa mchezaji wao wa zamani, Dimitar Berbatov aliyewaua dakika ya 52 na hakushangilia bao hilo kwa heshima yao, huku Spurs wakionekana kuchoka muda mwingi wa mchezo.

Nyota wao Gareth Bale ambaye kocha Andre Villas-Boas anamfananisha na Lionel Messi wa Barcelona, alikosa mabao, kama ilivyokuwa kwa mwenzake, Jermain Defoe.

Kocha Alan Pardew wa Newcastle United amerudi kwenye masahibu baada ya vijana wake kushindwa kupata walau pointi katika safari yao kwa Wigan.

Newcastle wenye wachezaji wengi wa asili ya Kifaransa, walishindwa kufurukuta, kwani walilala kwa 2-1.

Mabao ya wenyeji yalifungwa na Jean Beausejour dakika ya 18 na Arouna Kone dakika ya 90, wakati la Newcastle liliwekwa kimiani na Davide Santon dakika ya 72. Pardew alishajua anarudi kaskazini mashariki mwa England na pointi moja na kukaa pazuri kwenye msimamo wa ligi, lakini Wigan wana kawaida ya kufufuka ligi inapokaribia mwishoni.

Katika mechi ya awali iliyotawaliwa na utata, wachezaji 10 wa Norwich City wakicheza ugenini waliwabana Sunderland kwa dakika 60 kwenda sare ya 1-1.

Baada ya Wes Hoolahan kuunganisha kwa kichwa mpira wa kichwa wa Kei Kamara, Norwich walimpotea golikipa wao, Mark Bunn aliyepewa kadi nyekundu.

Palikuwa na utata iwapo golikipa huyo alishika mpira kwa makusudi nje ya eneo lake, na iwapo alimzuia mchezaji wa timu pinzani kwenda kufunga bao la wazi.

Baada ya golikopa huyo kutolewa, ulipigwa mpira wa adhabu ndogo lakini haukuwa na madhara. Vijana wa Chris Hughton waliingia matatizoni tena, safari hii Sebastien Bassong kudaiwa kuunawa mpira ndani ya eneo la penati.

Mkwaju wa penati ulitiwa kimiani na Craig Gardner na kusawazisha mambo, lakini kipindi cha pili Dany Rose wa Sunderland alipounawa mpira ndani ya eneo la hatari, haikutolewa penati, bali adhabu ndogo kwenye ukingo wa eneo hilo.

Kwa matokeo ya Jumapili hii, Manchester United wanaendelea kuongoza kwa pointi 74 wakifuatiwa na Manchester City wenye pointi 59. Chelsea wamefikisha pointi 55 na Spurs wana 54.

Arsenal wapo nafasi ya tano kwa pointi 50, Everton 40, Liverpool 45, West Bromwish Albion 44, Swansea 40 na Fulham pointi 36.

Nafasi ya 11 inashikwa na Stoke City na Norwich wenye pointi 34, Newcastle na West Ham wenye pointi 33, Sunderland na Southampton wenye pointi 31 na Aston Villa waliojikusanyia pointi 30.

Eneo la hatari ya kushuka daraja wakati huu wa mapumziko ya mechi za kimataifa linawaacha Wigan wenye pointi 27, Reading na Queen Park Rangers wenye pointi 23 kila moja na uwiano wa mabao -22 kila moja pia.

 

 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

WAAMUZI WA ANGOLA KUCHEZESHA MECHI YA STARS DAR!

Uongozi Simba hautambui “Mapinduzi”