in

Casemiro ni bora kuliko Neymar?

Casemiro

Real Madrid imetinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya 9 katika kipindi cha miaka 11, safari hii watamenyana na Chelsea ya England katika hatua hiyo. Hii ni nusu fainali ya nne ya kwa kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane, ambaye amewahi kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo akiwa kocha mkuu na mara moja akiwa kocha msaidizi pamoja na mara moja akiwa mchezaji wa Real Madrid. 

Baada ya mchezo wa marudiano kati ya Liverpool na Real Madrid kwenye uwanja wa Anfield, kiungo mkabaji Carlos Casemiro alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo. Lilikuwa jambo la kawaida kutokana na kiwango alichoonesha mchezoni. Mashabiki wa soka wanasema Casemiro kazi yake ni kufanya akzi zote chafu katika eneo la kiungo na safu ya ulinzi. 

Wachezaji wanaocheza nafasi  ya kiungo mkabaji mara nyingi hubeba majukumu makubwa ya timu na wao ndio injini ya timu zao. Majukumu hayo yamesababisha mashabiki wa soka wawe wanawaita jina la Punda. 

Kwa mfano katika klabu ya Simba ya Tanzania, kiungo mkabaji Muzamir Yassin anaitwa jina la Punda. Ni mtu anayebeba mizigo mizito kama mnyama Punda na lazima ifikishwe sehemu sahihi na kuibeba timu kwa dakika zote 90 au 120 za mashindano yoyote. 

Tanzania Sports
Neymar

Kikosi cha Real Madrid kina wachezaji wawili ambao kazi yao ni kufanya kazi chafu na kuwa Punda wa timu hiyo kutokana na majukumu wanayokuwa nayo. Hao ni Carlos Casemiro na Federico Valverde, ambao ni Punda na wanaofanya kazi chafu chafu uwanjani yaani kuwadhibiti wapinzani, kuwakaba kwa nguvu,kuwachapa viatu na pengine kusababisha madhambi kwa lengo la kupunguza kasi zao.

Sasa turudi kwa Casemiro na kazi yake ambayo imezua mjadala kuwa ni mchezaji bora kuliko Neymar Junior wa PSG. Ambao katika mchezo wa nusu fainali watachuana na Manchester City. 

Wengi wanaweza kudhani hilo ni suala la kijinga kulielezea kuwa kiungo mkabaji ni bora kuliko mshambuliaji. Kwanza mshambuliaji anauzwa bei ghali zaidi kuliko kiungo mkabaji. Lakini kwa kuangalia mwenendo wa sasa nyota wa Real Madrid anaibuka kuwa bora kuliko Neymar. Huu sio upendeleo bali namna ninavyotazama uchezaji,majukumu na matokeo ya timu kwa ujumla.

Casemiro anawakilisha mtindo wa kucheza wa viungo wa Real Madrid, ambao kwa takwimu zilizo bayana ni klabu yenye rekodi kubwa kuliko wapinzani wake. Real Madrid imekuwa na rekodi ya kutinga nusu fainali kila baada ya miaka miwili na mkononi wanayo mataji matatu waliyotwaa mfululizo na kuweka historia ya dunia. Ndani ya miaka 8 walichukua mataji matatu, ambapo Casemiro ndiye alikuwa injiani ya mafanikio katika eneo la kiungo. 

Mbrazil huyo ni mchezaji halisi wa ulimwengu wa sasa katika soka la ushindani, ingawa ni ukweli kwamba yeye hafanyi yale ambayo hufanywa na Neymar. Casemiro hachezi kwa kuremba,hapigi chenga nyingi,kupangua ngome ya adui,kasi na ubunifu katika eneo la mwisho linalohitaji ubunifu la kupachika mabao. Viungo wabunifu kama Neymar ni ghali sana katika soka la kisasa. Kila timu inahitaji kiungo mbunifu au mshambuliaji wa pili mwenye ubunifu ambao utasaidia timu kupata matokeo mazuri.

Hata hivyo namna Casemiro anavyoshughulika inashangaza kuona bei yake sokoni haikuwa kubwa wakati ananunuliwa na Real Madrid. Je ni kiasi gani ambacho Real Madrid inaweza kulipa kwa mchezaji huyo anayevaa jezi namba 14? 

Casemiro si mchezaji ghali kama alivyokuwa kiungo Mauro Silva ambaye alikuwa kiungo kabaji mwenye kuifanya timu icheze kwa uwiano mzuri na kuwalinda vema wachezaji wa safu ya ulinzi. 

Mauro Silva aliwapa uhuru viungo washambuliaji, wangeweza kucheza kwa kutamba,madoido na kuwa wabunifu kupindukia. Lakini hayo yote yalichangiwa na uwezo wa Mauro Silva ambaye alileta uwiano mzuri kwenye timu kati ya safu ya ulinzi na kiungo na ushambuliaji.

Casemiro anaipa timu nguvu,uongozi thabiti,uchu wa kusaka ushindi na tabia zote za kubeba mzigo wa timu na kuivusha au kupata mafanikio kama alivyoonesha kwenye mchezo war obo fainali dhidi ya Liverpool, kwenye La Liga dhidi ya Barcrelona.

Katika kikosi cha Real Madrid hakuna mchezaji mbadala au msaidizi wa Casemiro, na kwake uchovu wa mechi ni kitu asichojua-yupo kana kwamba amejitenganisha kama maji na mafuta. Alihitajika katika safu ya ulinzi, alihitajika kwenye safu ya kiungo, alihitajika kwenye kumsaidia Karim Benzema kwenye ushambuliaji, alihitajika kwa beki wa kulia Federico Valverde na Alvaro Odriozola, kote huko alisaidia na kusafisha hatari zote. 

Alitakiwa kuwalinda Nacho Hernandez na Eder Militao, lakini pia alimsaidia Karim Benzema kila alipohitaji kuungwa mkono katika safu ya ushambuliaji. Amefunga mabao sita msimu huu.

Pengine Casemiro si aina ya wachezaji wanaopendwa na watoto kuonwa YouTube au katika michezo ya gemu za aina yoyote kama ilivyo kwa Neymar. Naymar ni kipenzi cha watu mbalimbali kutokana na uchezaji wake, chenga nyingi,madoido,ubunifu na kupachika mabao, lakini hana mafanikio kama yale aliyopata Casemiro.

Wote ni Wabrazil, Casemiro anawakilisha viungo aina ya Mauro Silva, Gilberto Silva, Edmundo, yaani viungo wagumu ambao wamekuwa nguzo ya timu na ndio wanajenga ukuta wa ulinzi kabla ya wapinzani hawajawafikia mabeki. Naymar anawakilisha wabunifu kama Ronaldinho,Denilson,Ricardo Kaka na wengineo. Sasa sijui ni lini Neymar atafikia mafanikio makubwa ndani ya timu ya PSG.

Kwa kikosi cha Real Madrid akiwemo Casemiro anapunguza presha yoyote dhidi ya mabeki na kuwasaidia walinzi kucheza vizuri bila kujali kama baadhi ya wachezaji tegemeo hawapo. Kifupi Casemiro anawakilisha wachezaji bora na wenye mfanikio halisi na viungo wazuri kama Carlos Henrique. Ni viungo maridadi.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
VAR ikitumika kwenye mechi ya Simba, Yanga

VAR ikitumika nini kitatokea Ligi Kuu Tanzania?

Liverpool

Ni wakati wa Liverpool kufanya mabadiliko