in , ,

BUFFON TAZAMA PICHA YA ZIDANE

Kila mtu anamuonea huruma na kuna wakati mwingine huruma hizi zinaenda
sambamba na sifa nyingi kuhusu kipaji chake.

Golikipa aliyedumu kwa muda mrefu tena kwenye kiwango chake bila
kutetereka, miaka 40 inasomeka kwenye paji lake la uso lakini anadaka
mipira ya mashuti ya vijana wa miaka (20-29)

Kuna wakati mwingine mikono yake imekuwa imara zaidi ya mikono ya
makipa wenye umri mdogo. Mikono yake imekomaa ipasavyo na imedumu
ipasavyo langoni

Hapana shaka mikono yake inastahiri kushika kila aina ya taji
aliloshiriki kulipigania akiwa langoni.

Ubingwa mara nane wa Seria A ni kitu ambacho alistahili katika maisha
yake na inawezekana wakati anakutana na Zinedine Zidane katika fainali
ya kombe la dunia 2006 ilikuwa ni siku kubwa ya furaha kwake kwa
sababu mikono yake ilinyanyua kombe la dunia.

Kombe lenye heshima kubwa dunia, kombe ambalo kila mchezaji anatamani
kulichukua lakini bahati mbaya siyo kila mchezaji hufanikiwa kulishika
kombe hili.

Kuna mengi sana ya kujivunia kwenye mpira, unaweza ukajivunia kubeba
kombe la dunia mwenzako akakuuliza una medali ya mshindi wa kwanza ya
kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya?

Ronaldo

Kombe ambalo lina hadhi kubwa kwenye ngazi ya klabu, unaweza
ukafanikiwa kwenye timu ya taifa na ukabeba kombe lenye hadhi kubwa
ngazi ya timu ya timu ya taifa, lakini ukashindwa kufikia mafanikio ya
kubeba kombe lenye hadhi kubwa katika ngazi ya klabu.

Ndipo hapo huzuni lazima ikukamate tena unapogundua mchezaji nyota
anamaliza maisha yake ya mpira wa miguu bila kubeba kombe la klabu
bingwa barani ulaya.

Dunia ilimhurumia Ronaldo De Lima, ikaja kumuongelea kwa huzuni Zlatan
Ibrahimovich leo hii inamuaga kwa huruma Gigi Buffon

Kipa ambaye hakuwahi kupata kadi nyekundu katika michuano ya klabu
bingwa barani ulaya katika mechi 116 lakini mechi ya 117 Michel Oliver
akamuonesha kadi nyekundu

Kadi ambayo ilikuwa na maana kubwa sana katika kuzima ndoto za Gigi
Buffon, kadi ambayo ilikuwa na tafasri moja tu ni ngumu kwako kushinda
kombe la klabu bingwa barani ulaya ukiwa kama mchezaji

Inawezekana ikawa mechi yake ya mwisho katika michuano hii ya klabu
bingwa barani ulaya baada ya kufika fainali kwa mara mbili mfululizo
bila kufanikiwa kushinda kombe

Anaondoka katika uwanja wa Santiago Bernabeu akiwa ameinamisha kichwa
huku swali kubwa linalo muumiza ni lini atashinda kombe la klabu
bingwa barani ulaya?

Moyo wake unatamani sana, mashabiki wengi wa mpira wanataka sana
ashinde lakini muda haumruhusu tena yeye kushinda akiwa kama mchezaji

Kuna njia ambayo anatakiwa kuifikiria wakati huu anapojiuliza maswali
hayo. Siyo muda sahihi kwake kuruhusu kuhurumiwa tena.

Wakati huu anatakiwa atumie mlango wa pili, mlango ambao wengi
wamefanikiwa baada ya kuingia huko.

Jana Zinedine Zidane alikuwa kwenye benchi la RealMadrid, timu ambayo
aliitumikia kama mchezaji.Gigi Buffon anatakiwa akae chumbani kwake
huku akiwa na picha ya Zinedine Zidane.

Picha ambayo itamsaidia kukumbuka matukio ya nyuma ambayo yaliwahi
kutokea kati yake na Zinedine Zidane.

Asilisahau tukio la mwaka 2006 tukio ambalo lilimwezesha kubeba kombe
la dunia mbele ya Zinedine Zidane wote wakiwa wachezaji

Leo hii Zinedine Zidane ni kocha, tena kocha mwenye mafanikio makubwa,
mshindi wa kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya mara mbili mfululizo

Mafanikio haya yamtamanishe Gigi Buffon na kumfanya aone bado ana
nafasi kubwa ya kubeba kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya.

Muda haujamwaacha, nafasi bado anayo, ameshindwa kubeba kombe kama
mchezaji lakini ana nafasi kubwa ya kubeba kama kocha.

Miaka 40 kwake ni mingi, ni wakati mzuri kwake kuvua gloves na kuvaa
suti, ni wakati mzuri kwake yeye kusimama kwenye mstari wa makocha,
siyo muda kwake yeye kusimama tena mbele ya milingoti mitatu

Amefanya kazi na makocha wengi wenye uwezo mkubwa wa kufundisha mpira,
amekuwa nahodha kwa kipindi kirefu akiwaongoza wachezaji wenzake ndani
ya uwanja, ni wakati mzuri kwake yeye kukaa kwenye benchi la ufundi na
kuwaongoza wachezaji wa timu yake kubeba kombe la ligi ya mabingwa
barani ƴulaya ili kutimiza furaha yake.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KIPI WAKIFANYE MANCHESTER CITY WASHINDE DHIDI YA LIVERPOOL?

Tanzania Sports

NATAMANI KUSIKIA LWANDAMINA KARUDI YANGA