in , , ,

Brazil sikio la kufa

Brazil wameshindwa kuwafuta machozi watu wake katika uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2014 kwa kukosa hata nafasi ya tatu.

Badala yake, Brazil waliweka rekodi nyingine mbaya kwa kufungwa mabao 3-0 na Uholanzi kwenye mechi ya kutafuta mshindi wa tatu jijini Brasilia na kuwakatisha tamaa wananchi na washabiki wake ndani na nje ya nchi.

Ndani ya nusu saa ya kwanza tayari Brazil walisharuhusu mabao mawili, kutokana na matatizo waliyo nayo kwenye ushirikiano baina ya beki na viungo wake.

Nahodha Thiago Silva alilambwa kadi ya njano dakika za mwanzo kabisa baada ya kumvuta shati Arjen Robben, ambaye kama kawaida yake alianguka na ikawa penati iliyotiwa kimiani na Robin van Persie. Robben alianguka mara nyingine  nyingi hata baadhi zikionekana za kujirusha mwenyewe.

Bao la pili la Brazil lilitiwa kimiani na Daley Blind Kutokana na kosa kubwa la beki wa kati aliyetoka Chelsea na anayehamia Paris Saint Germain, David Luiz kurudisha uwanjani kwa maadui kwa kichwa mpira wa juu badala ya kuutoa nje kirahisi.

Licha ya kutawala zaidi mchezo, huku wakiwa na kasi katika mashambulizi, Brazil walishindwa kulenga mikwaju mingi golini na ilishindikana kabisa kupata walau bao la kufutia machozi.

Wakati washabiki wakidhani mechi ingemalizika kwa mabao 2-0, Georginio Wijnaldum alifunga bao la tatu katika dakika ya 90, wakati huo washabiki wa Brazil wakiwa wameshaanza kuwazomea wachezaji na kocha Luiz Felipe Scolari waziwazi kwa mchezo dhaifu usio na matunda ya mabao dhidi ya adui bali kwao.

Neymar aliyeumia uti wa mgongo kwenye robo fainali alikuwa ameketi kwenye benchi na beki ambaye hajachezeshwa mechi kadhaa sasa, Dani Alves na wengine sita waliowekwa kando tangu wachakazwe na Ujerumani, akiwamo mshambuliaji Fred ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Jo tangu mwanzo wa mechi.

Hii ni mara ya kwanza tangu 1940 Brazil wanapoteza mechi ya pili mfululizo katika ardhi yao, baada ya kile kichapo cha haja kutoka Ujerumani Jumanne cha mabao 7-1 na kuwafanya waweke rekodi nyingine ya kuwa timu iliyofungwa idadi hiyo ya mabao kwenye nusu fainali.

Kadhalika wameweka rekodi katika mashindano haya kwa kuwa timu iliyofungwa mabao 10 katika mechi mbili tu, tena zikiwa zimefuatana. Washabiki wa Brazil walianza kwa kuishangilia timu yao lakini walichoshwa na kutopewa zawadi ya bao.

Kana kwamba hiyo haitoshi, wapinzani wao wakali kabisa kwenye soka, Argentina wanachuana na Ujerumani katika kile kinachochukuliwa kama madhabahu ya asili ya soka ya Brazil, Maracana Jumapili hii.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Argentina, Ujerumani hapatoshi

Rudisha ashinda mbio Uingereza