in , , ,

Benitez abezwa, aanza kwa sare

*Tottenham wawafyatua West Ham

*Southampton wawachapa Newcastle

Rafa Benitez amepokewa vibaya na mashabiki Stamford Bridge, huku timu yake ikitoka suluhu na mabingwa Manchester City.

Mashabiki walionesha wazi hisia zao dhidi ya kocha huyo wa zamani wa Liverpool, aliyekuwa na uhasama mkubwa nao.

Walionesha mabango kuashiria kutomtaka, mengine yakimlilia kocha aliyetimuliwa, Roberto Di Matteo, huku wakimzomea Mhispania huyo katika mechi yake ya kwanza.

Mabango na kelele hizo vilionwa vyema na mmiliki wa klabu, Roman Abramovich aliyekuwa amejichimbia kwenye kizimba chake bila kuonesha kuguswa.

Vinginevyo mchezo dimbani ulijaa kukamiana baina ya wachezaji wa timu mbili hizi kubwa, pakiwa na rafu za hapa na pale, wengi wakimtazama Fernando Torres aliyejaribu kufurukuta.

Mhispania huyu aliyenunuliwa kwa pauni milioni 50 ndiye anadaiwa kuwa sababu ya kufutwa kazi Di Matteo, kwani maagizo yalikuwa lazima acheze mechi ya klabu bingwa Ulaya dhidi ya Juventus, kocha akakaidi.

Benitez aliyeajiriwa kwa miezi saba ya msimu iliyobaki, anadaiwa kuagizwa kumfufua ili awe mpachika mabao, ili hatimaye watwae mataji mengi.

Kwa suluhu hiyo, City wameshindwa kuwashusha Manchester United wenye pointi 30 kileleni mwa ligi, wakiwa nyuma yao kwa pointi moja.

Chelsea wanabaki nafasi ya nne nyuma ya West Bromwich Albion walioanza vyema msimu huu chini ya kocha mpya Steve Clarke.

Katika mchezo mwingine, kocha Andre Villas-Boas amewapaisha Tottenham Hotspur kwa kuwafunga West Ham United mabao 3-1.

Mchezaji Gareth Bale alionyesha ukali wa aina yake mchezoni, akipachika pia bao la tatu, akitanguliwa na Jermain Defoe aliyefunga mawili.

West Ham waliopoteana walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Andy Carroll, na wana kazi ngumu mbeleni kwani wanakabiliana na Manchester United, Chelsea na Liverpool.

Ushindi huo umewapandisha vijana wa Villas-Boas katika nafasi ya saba, wakiwa pointi sawa na Arsenal lakini hawana uwiano bora wa mabao kama jirani zao wa kaskazini mwa London. West Ham wameshuka hadi nafasi ya nane.

Mchezo huo ulishuhudia kurejea kazini kwa mwamuzi Mark Clattenburg, aliyekuwa akituhumiwa na Chelsea kutumia lugha ya kibaguzi dhidi ya John Obi Mikel. Alisafishwa na polisi na chama cha soka na hakufanya kazi kwa karibu mwezi mzima.

Nao Southampton wamefanikiwa kuondoka kwenye eneo la hatari ya kushuka daraja, baada ya kushangaza wengi kwa kuwafunga Newcastle United kwa mabao 2-0.

Wakicheza kwenye uwanja wao wa St Mary’s, Saints wanaofundishwa na Nigel Adkins walifunga kupitia Adam Lallana na Gastom Ramirez.

Walianza vibaya msimu huu kwa kufungwa mfululizo, lakini sasa wamefikisha mechi tatu bila kufungwa, huku Newcastle wakiwa kinyume chao, kwa kuanguka kama jiwe, hii ikiwa mechi ya tatu wakipokea kipigo.

Hawajapata  kupoteza mechi mfululizo kiasi hiki katika miaka minne iliyopita. Ukweli ni kwamba walikuwa na bahati ya kufungwa mabao hayo mawili tu, kwani walicheza hovyo.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Manchester United warejea kileleni

Harry Redknapp atawaokoa QPR?