in , , ,

BAYERN v. ARSENAL

 

 

Arsenal usiku wa leo watakuwa wageni wa Bayern Munich kwenye dimba la Allianz Arena kwenye mchezo wa Kundi F wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Arsenal ambao waliwafunga wapinzani wao hao kwenye mchezo wa Kundi hili mwezi uliopita wanahitaji kupata alama tatu pia kwenye mchezo huu wa leo ili kuyaweka hai matumaini yao ya kuvuka hatua  za makundi.

Kwa upande mwingine wenyeji Bayern Munich pia wanahitaji alama tatu muhimu kwenye mchezo wa leo baada ya kuteleza kwenye mchezo uliopita. Ikiwa watapoteza mchezo wa leo watajikuta kwenye nafasi itakayowahitaji kushinda michezo yao yote miwili ya mwisho ili kukata tiketi ya kucheza hatua za mtoano.

Itakumbukwa Arsenal hawakupoteza mchezo wowote walipotembelea dimba la Allianz Arena mara mbili za mwisho kwenye msimu wa 2012/13 na 2013/14. Waliibuka na ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa hatua za 16 bora msimu wa 2012/13 kisha kutoa sare ya 1-1 msimu wa 2013/14 walipotembelea tena dimba hilo.

Advertisement
Advertisement

Bayern Munich wao wana kumbukumbu ya kuutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu walipowasambaratisha Dinamo Zagreb mabao matano kwa sifuri kwenye mchezo wa mzunguko wa pili. Pengine hili linawaongezea hali ya kutaka kuwaonyesha Arsenal kuwa wao ni timu bora zaidi.

Hata hivyo wababe hao kwa mara ya kwanza msimu huu walishindwa kushinda mchezo wao wa Ligi Kuu ya Ujerumani Ijumaa wiki iliyopita walipolazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Eintracht Frankfurt wakati Arsenal walipata matokeo ya ushindi kwenye mchezo wao wa mwisho walipowafunga Swansea City 3-0 siku ya Jumamosi.

Kwa upande wa vikosi wenyeji Bayern Munich watawakosa wachezaji kadhaa kutokana na majeraha. Hao ni Frank Ribery, Mario Gotze na Sebastian Rhode. Pia kuna mashaka kuwa Holger Badstuber na Juan Bernat nao hawataweza kupatikana kwa ajili ya mchezo wa leo.

Arsenal wao wanaandamwa na majeruhi wa kutosha kwenye kikosi chao ambapo Ramsey ameungana na majeruhi wengine huku Chamberlain na Walcott ambao wangeweza kucheza kwenye nafasi yake pia wamekumbwa na matatizo ya misuli. Hector Bellerin pia ni majeruhi, hivyo Mathieu Debuchy ataziba nafasi yake. Welbeck, Wilshere na Flamini pia ni majeruhi.

Vikosi vinavyotazamiwa kuanza ni golikipa Manuel Neuer, Philipp Lahm, Jerome Boateng, Javi Martinez na David Alaba, viungo Arturo Vidal, Xabi Alonso na Thiago Alcantara huku Thomas Muller, Robert Lewandowski na Douglas Costa wakisimama kwenye nafasi ya ushambuliaji kwa upande wa wenyeji Bayern Munich.

Arsenal wao wanatazamiwa kuwaanzisha golikipa Petr Cech, walinzi Mathieu Debuchy, Per Mertesacker, Laurent Koscielny na Nancho Monreal, kwenye eneo la kiungo watasimama Francis Coquelin, Santi Cazorla, Mesut Ozil wakisaidiwa na Joel Campbell na Alexis Sanchez huku Olivier Giroud akisimama mbele peke yake.

Nyota wa kutazamwa kwenye mchezo wa leo ni Robert Lewandowski kwa upande wa Bayern Munich. Mshambuliaji huyo kutoka Poland mbaka sasa amefunga mabao 17 kwenye michezo 16 aliyoichezea Bayern msimu huu. Tutarajie mchuano mkali kati yake na beki kisiki wa Arsenal Per Mertesacker.

Kwa upande wa Arsenal nyota wa kutazamwa ni Mesut Ozil. Kiungo huyo wa Kijerumani ndiye aliyefunga bao la pili kwenye mchezo uliopita baina ya timu hizi na anaongoza chati za wachezaji waliopiga pasi nyingi za mabao kwenye ligi tano kubwa za Ulaya msimu huu akiwaamepiga pasi 9 za mabao.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

LIGI YA MABINGWA ULAYA:

Tanzania Sports

Arsenal hali mbaya