in , ,

AZAM WAMEMCHOMA KISU JICHONI BOCCO, HUKU WAKIWA WAMEMTUMBULIA JICHO.

Kuna vitu ni vigumu kuvitenganisha hata siku moja, na kuna wakati
mwingine unaweza ukakitaja kitu fulani kichwani mwako ikaja taswira ya
kitu kingine ambacho kinamahusiano na hicho kitu.

Unapata picha gani unaposikia Chupa Ombwe ( Thermos)ikitajwa kwenye
masikio yako ? Bila shaka neno chai na uji litakuja kwenye akili yako
kwa sababu ni ngumu kutenganisha chupa ombwe na chaji au uji.

Ndipo ulipo ugumu wa kutenganisha hivi vitu unapoanzia, na kuna wakati
mtu anaweza kukuona kichaa unapoacha kuona umuhimu wa risasi ndani ya
bunduki au umuhimu wa bunduki kwa risasi. Hivi vitu viwili ni tofauti
lakini vina maana moja katika mategemezi.

Huwezi kutenganisha mategemezi ya hivi kitu hata siku moja kwa sababu
vinategemeana kwa kiasi kikubwa. Risasi ndiyo hufanya bunduki kuogopwa
na watu, vivyo hivo bunduki hufanya risasi kuogopwa na watu.

Hii yote inaonesha kwenye maisha tunaishi kwa kutegemeana kila mmoja,
hakuna mwenye bega refu linatosha kujibeba mwenyewe ndiyo maana kuna
wakati mwanadamu hutegemea bega la mwenzake limbembe ili kumfikishwa
sehemu ambayo anaitaka kwenye mafanikio.

Ndiyo hapo mistari ya pamoja inapounganishwa kwa pamoja, ndipo hapo
tunapokutana na mstari wa Musa Hassan Mgosi na Simba au Mstari wa
Charles Boniface Mkwasa na Yanga na hivi karibuni kuna mstari mnene
kati ya John Bocco na Azam FC.

Mstari huu umejengwa tangu Azam FC ikiwa katika ligi daraja la kwanza.
Mstari huu umekaa kwenye vichwa vya watu wengi mpaka kufikia hatua
ambayo ukimtaja John Bocco taswira ya Azam FC inakuja haraka, vivyo
hivo ukiitaja Azam FC taswira ya John Bocco inakuja kwa uharaka.

Hii yote inaonesha kulikuwa na kiunganishi cha heshima kati ya hawa
wawili yani John Bocco na Azam. Kiunganishi ambacho kimeanza tangia
Azam FC ikiwa daraja la kwanza.

Uhusiano huu ulidumishwa maradufu katika mji wa Dodoma mara baada ya
John Bocco kufunga ambalo liliisaidia Azam FC kupanda daraja kutoka
daraja la kwanza mpaka ligi kuu ya Tanzania.

Ndipo hapo heshima yake ilipoanza kujengwa ndani ya kikosi cha Azam,
busara zake pia zikampa nafasi kubwa ya yeye kuwa nahodha wa kikosi
cha Azam Fc.

Nahodha ambaye aligeuka kuwa nembo kubwa ya Azam FC kwa sababu ya
kuiongoza vyema Azam FC katika mashindano mbalimbali.

Alikuwa chachu ya timu kuchukua kombe la Kagame Challenge Cup kwa
kuibuka mfungaji bora katika mashindano hayo. Magoli yake yaliweka
nembo ya heshima ambayo ni vigumu kufutika kiwepesi katika historia ya
klabu ya Azam FC.

Alikuwa mhimili mkubwa wa Azam FC ilipokuwa inachukua ubingwa wa ligi
kuu Tanzania.

Hakuna mchezaji wa Azam FC ambaye alijutia kuwa chini ya uongozi wa
John Bocco kama nahodha. Hii yote inaonesha alikuwa akiiongoza timu
katika misingi ya umoja na ushikamano.

Busara na heshima yake kwa wachezaji na viongozi wa klabu ndivyo
ambavyo vilimpa nafasi ya yeye kuheshimiwa na wachezaji kwa ujumla.

Wachezaji chipukizi walitamani kukaa karibu na John Bocco ili wachume
busara zitakazosababisha wao kufika mbali kwenye mpira.

Huyu ndiye mfungaji bora wa wakati wote wa Azam Fc na ni mmoja wa
wachezaji ambaye ameichezea klabu hii kwa kipindi kirefu sana.

Jasho lake limeanza kutiririka tangia akiwa na timu ligi daraja la
kwanza mpaka ligi kuu msimu ulioisha hivi karibuni.

Pumzi yake , Jasho lake, mbio zake , pasi zake na magoli yake yamekuwa
yakionekana ndani ya Azam Fc kwa takribani miaka 10 bila kuchoka au
kwenda timu yoyote ile.

Hii yote ilitosha kwake yeye kupata heshima nzuri kipindi ambacho muda
wake wa kukaa Azam FC utakavyomalizika.

Ni shujaa wa Azam Fc tangia goli lake moja lililotumika kuipandisha
hii timu mpaka magoli yake yaliyokuja kuipa ubingwa wa ligi kuu ya
Tanzania na kombe la Kagame challenge cup.

Mchango wake ni mkubwa sana ndani ya timu ya Azam Fc , mchango ambao
ungetosha kwa timu kumwandalia mazingira ya mwisho ya kumuaga hata
kama mkataba wake umekwisha na hawana nia ya kuongeza mkataba mwingine
.

Utaratibu mzuri ungewekwa wa kuenzi na kuheshimu mchango wake alioutoa
kwa muda wa miaka 10 ndani ya kikosi cha Azam Fc.

John Bocco hakustahili kuondoka kama alivyoondoka.

Azam Fc bado wanamuda wanatakiwa kukaa chini na kuangalia namna ya
kumuaga vizuri John Bocco kulingana na heshima aliyoiweka ndani ya
kikosi cha Azam FC.

Martin Kiyumbi

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

PESA HAIKUWA CHOCHOTE KWENYE MSIMU WA EPL ULIOMALIZIKA

Tanzania Sports

Arsรจne Wenger – KOCHA WA KUDUMU ARSENAL