in

Azam FC watang’ara mashindano ya Kimataifa?

Azamfc

MABINGWA wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, klabu ya Azam ya jijini Dar es salaam wamerejea kwenye mashindano ya kimataifa baada ya kukosekana kwa misimu kadhaa iliyopita.

Azam maarufu kama Mabwanyenye wa Chamazi wamepania kufanya vizuri kwenye mashindano hayo huku uongozi wa timu hiyo ikijinasibu kuwa hawataki kurudia makosa kama misimu iliyopita kuanzia suala la usajili na viwnago vya wachezaji pamoja na ushiriki wa mashindano ya kimataifa.

Kuonesha nia yao ya kujipanga kwenye mashindano ya kimataifa, Azam hivi karibuni wamekataa ofa ya shilingi bilioni 18 kutoka waarabu wa Pyramids ya Misri ambao wanamtaka mshambuliaji wao Prince Dube raia wa Zimbabwe. Nyota huyo alimaliza msimu uliopita kwa kupachika mabao 14 na kupika mengine matano.

Afisa mtendaji mkuu wa Azam, Abdulkarim Nurdin amenukuliwa na gazeti moja la kila siku la michezo akieleza kuwa nia ya timu yao kwenye mashindano ya kimataifa ni thabiti na kwa kuanzia wamesajili nyota wapya na kwamba wamepania kufika mbali kwenye mashindano hayo na kuhakikisha kikosi chao kinakaa pamoja kwa muda mrefu ili kuleta matunda.

“Hatutaki kurudia makosa, tunahitaji timu itakayokaa pamoja muda mrefu ili kuwa na ushindani ndani na nje, kumbuka tunatarajia kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa kombe la shirikisho,” Abdulkarim aliliambia gazeti hilo.

Katika nukuu hiyo ndipo linapoanzia swali, je Azam wataweza kung’ara katika mashindano ya Kimataifa msimu huu? Je wataweza kurekebisha makosa yao ya misimu ya nyuma waliyoshindwa kufurukuta kwenye mashindano hayo? Maswali hayo yanapaswa kujibiwa msimu huu na Azam ambao wamebainisha nia yao.

Suala la kukataa kumuuza nyota wao,kukiri makosa ya nyuma na dhamira ya kushiriki mashindano ya kimataifa ni jambo la kiungwana lakini liwe zaidi ya hapo. Kimsingi Azam wangeweza kushiriki mashindano ya kimataifa na mafanikio ikiwa wangekubali kubaki na nyota wao ambao wengi walihamia Simba ambako kwa miaka minne wametamba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azam waliachana na Aishi Manula, John Bocco na Erasto Nyoni ambao wamekuwa wachezaji wa kutumainiwa Msimbazi na wamefanya mambo makubwa klabuni hapo kwa kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Endapo Azam wangebakiza msingi wa timu yao bila shaka hata Namungo FC wasingepata nafasi mbele yao. Lakini udhaifu wa Azam miaka kadhaa iliyopita, licha ya uwekezaji mkubwa imekuwa timu inayosua sua na kufukuza makocha mara kwa mara.

Tatizo la kwanza lililojitokeza ni kufumua wachezaji ambao walikuwa wanaunda uti wa mgongo wa timu. Angalau wangeachana na wachezaji hao huku wakiwa wamefanya mambo makubwa kwenye mashindano mbalimbali nje ya ukanda wa Afrika mashariki, lakini hakuna histioia yoyote ya kujivunia na inatia simanzi kushuhudia timu yenye rasilimali inashindwa kupiga hatua na kugeuzwa ‘najikokota Fc’.

Kila msimu wamekuwa wakitema wachezaji ambao hawategemewi kuachwa, hali ambayo inapunguza uimara wao. Kama sababu ingelikuwa kukaa na timu muda mrefu na mipango ya kufanya vizuri kimataifa, bila shaka wangekataa ofa kama za Simba kwa Nyoni,Bocco na Manula.

Walimuuza Manula lakini hadi leo hawana mlinda mlango mwenye sifa za nyota huyo namba moja nchini. Walimuuza John Bocco lakini hadi leo hawana mshambuliaji wa kufikia rekodi zake.

Kuuzwa Erasto Nyoni unaweza kusema nafasi ya kiungo walipata wachezaji wengi wazuri, lakini kufumua timu kwa dhamira isiyo na manufaa ni janga linalowaangusha hadi leo. Kukiri makosa ni sehemu ya maisha, lakini kwao limekuwa suala la kila msimu kusema hay ohayo. Ni marudio yaleyale ya ‘kukiri’ makosa wakati timu inashindwa kupiga hatua.

Naam, sasa mbele yao kuna mashindano ya kimataifa, wamesajili nyota wapya na watanufaika na kanuni mpya za kusajili wachezaji 12 wa kigeni. Pia Azam si kama timu zingine nje ya Yanga na Simba, nao wana uwezo wa kusajili nyota kutoka pembe zote za Afrika, kwahiyo wanapaswa kufahamu kuwa uwezo wao wa matanuzi sokoni uendane na matokea mazuri dimbani.

Azam wanao uwezo wa kuipaisha timu yao kupitia mashindano ya kombe la shirikisho bila kuogopa kilichopo mbele yao. George Lwandamina ni mwalimu mzuri, pia wana kikosi kizuri cha vijana ambao wanajaribu kupenya kwenye kikosi cha kwanza, mfano mshambuliaji wao Peter ni toleo lijalo lenye uwezo mkubwa kwenye kikosi chao.

Aidha, wamefanya mabadiliko kwa kuajiri Mkurugenzi wa michezo, Jonas Tiboroha ambaye amewahi kuwa katibu mkuu wa Yanga. Bila shaka nafasi ya mkurugenzi itasaidia kufanya tathmini mbalimbali katika kikosi chao kwa kushirikiana na benchi la ufundi.

Azam, Simba,Yanga na Baiashara United zinatarajiwa kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya Kimataifa. Hii ni fursa ambayo Azam imepata kutokana na kazi iliyofanywa na wachezaji wake wa zamani Aishi Manula,John Bocco na Erasto Nyoni, kwahiyo ni wakati wao wa kuonesha kuwa wanaweza kufika mbali kwenye mashindano.

Usajili wao wa  wachezaji wa kigeni unaweza kua na mchango mkubwa kwa wazawa, lakini mipango yao na uhodari wa benchi la ufundi ndio chachu ya mafanikio. Ifahamike miaka waliyopo katika Ligi Kuu Tanzania inatosha kusema wao ni timu changa. Sababu kwa hoja ya uchanga hata Namungo FC walikuwa wachanga lakini walifanikiwa kutinga hatua ya makundi kombe la shirikisho viweje wao Azam washindwe?

Pengine tunaweza kusema uchanga wa Namungo ulichangia kuambulia vipigo kombe la shirikisho, lakini Azam ni timu iliyojionesha wazi inamudu mikikimikiki ya kimataifa, kwahiyo wanapaswa kuvunja rekodi ya Namungo. Hiyo ni changamoto yao, kwa sababu wao sio wadogo tena.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Alphonce Simbu

Was the Tanzanian Tokyo Olympics sabotaged?

Liverpool FC

Jurgen Klopp ana kibarua kigumu