in , , ,

Arsene Wenger : Maswali magumu

Msimu mpya upo hapa lakini Arsenal ni wale wale. Arsene Wenger
amepeleka jeshi lake vitani likiwa halijaivishwa vyema kimbinu wala
kuwa na fedha za kutosha – wakaangukia pua kwenye mechi ya kwanza ya
Ligi Kuu ya England (EPL).

Washabiki tuliingia uwanjani kuona Arsenal wanakuja na kipi kipya
kutokana na kusuasua kwa usajili na kwa hakika karibu washabiki 60,000
walishuhudia udhaifu ule ule wa kawaida wa Arsenal, wakafunga 4-3 na
kikosi kizuri cha Liverpool chini ya Jurgen Klopp.

Wenger alionekana kulihisi joto kali, hasa baada ya Sadio Mane
alipoweka kimiani bao la nne. Arsenal walishaona mabao yakija hata
kabla ya mechi; ilikuwa suala la muda tu na Arsenal walibaki kwenye
nafasi waliyozoea, ya kuwa nyuma ya washindani wenzao wa kuwania
ubingwa kwa pointi tatu nzima baada ya mechi moja tu.

Wangefanya nini washabiki wale? tulikaa (Nilikuwepo uwanjani) chini kimya lakini wakiumia
baada ya kile kinachoonekana ni uamuzi wa Wenger kukataa kusajili
majina makubwa wakati wenzao kama Manchester United, Chelsea na Man
City wakifanya kweli kujiimarisha.

Sasa wanajionea wenyewe mgogoro ukianza kuwakumba na simanzi
kuzifunika nyuso zao baada ya majeruhi kuanza kujilundika kwenye
vyumba vya uuguzi. Tazama Aaron Ramsey ameumia na haijulikani atarudi
lini, Alex Iwobi kadhalika wakati Jack Wilshere anatarajiwa Agosti 20.

Gabriel aliyeumia enka anatarajiwa uwanjani Oktoba 15, Carl Jenkinson
ni hadi Novemba, Per Mertesacker ni Januari mwakani na Danny Welbeck
hadi Februari na wote hao wameumia magoti yao. Wachezaji saba muhimu
wapo nje na bado watu hawataki kufanya usajili wa maana. Na kwa nini
wawe na majeruhi wengi kiasi hicho? Na kwa nini iwe wao tu kwa wingi
huu?

Liverpool wana majeruhi watano tu, wakati wawania ubingwa wanaopewa
nafasi kubwa – Chelsea na Manchester City watatu kila mmoja,
Manchester United wawili na Tottenham Hotspur wote wapo timamu.

Kutokana na michuano ya Euro 2016 nchini Ufaransa, Arsenal walikosa
huduma za akina Mesut Ozil, Olivier Giroud naLaurent Koscielny –
wachezaji waandamizi, walau kwa viwango vya Arsenal, kwenye mechi
hiyo. Lakini kilichoudhi washabiki wengi ni tamko la Wenger kwamba eti
timu yote haikuwa tayari kwa EPL.

Kwa nini hawakuwa tayari? Bado Mfaransa huyu hajui ni lini watakuwa
tayari. Kwa nini? “Tutakuwa lini tayari? Sijui. Tunatakiwa kuwa tayari
wiki ijayo kwa sababu tunakwenda Leicester,” Wenger alisikika akisema.
Na kweli lazima wawe tayari vinginevyo ni maangamizi.

Tena wangefurahi kwa sababu ratiba imewapangia vyema Arsenal timu
wanazocheza nazo. Wenger anajua walitakiwa kuanza kuwacharaza
wapinzani tangu mwanzo ili ndoto yake ya ubingwa iwe kweli, lakini
anaonekana kutojali kuhakikisha wanafanya hivyo; anazungumza bila
kuchukua hatua za dhati. Kikubw alichoweza kufanya baada ya kufungwa
na kuanzisha sesheni mbili za mazoezi badala ya moja.

Meneja wa Arsenal: Arsène Wenger
Meneja wa Arsenal: Arsène Wenger

Kwa nini yanatokea haya tena na tena? Arsenal waliwapa Liverpool faida
ya kujipigia wakiwa nyumbani Emirates baada ya ‘hang’over’ ya
kiangazi. Miezi 12 iliyopita walikuwa West Ham waliowagonga Arsenal
wakati miaka mitatu iliyopita walikuwa Aston Villa waliowapiga vilivyo
Arsenal hapo hapo nyumbani siku ya kwanza ya msimu wa ligi kuu. Aibu
hii mpaka lini?

Huu ni mwekeleo wa kuogofya lakini Wenger haelekeo kujifunza kwa
makosa ya nyuma na kujipanga upya. Ni kweli kwamba Arsenal
waliondokana na mwelekeo huo miaka iliyopita na kuja kumaliza katika
nafasi nne za juu, lakini hofu ni kwamba safari hii wapinzani wao
wamejipanga vyema zaidi na wanasogea kwa kasi kubwa hivyo kwamba
Arsenal wataachwa mbali huko nyuma wakiwayawaya.

Licha ya kupoteza mechi hiyo, Arsenal walikuwa na wachezaji wazuri
uwanjani; akina Alexis Sanchez, Mohamed Elneny na Theo Walcott wote
walianza mechi wakati Granit Xhaka na Santi Cazorla waliwapa sapoti ya
kilo kutoka kwenye benchi. Pamoja na hayo, ukichanganya majeruhi na
labda wataongezeka, watakuwa na kazi ya ziada, watasubiri hadi lini?

Je, kwa nini hawataki kusajili mlinzi wa kiwango cha kimataifa?
Unapowaweka Calum Chambers na Rob Holding kama mabeki wa kati wakati
hawana uzoefu mkubwa, itakuwaje kwa gemu kubwa? yaani ukiwajumlisha
hao wawili unapata umri wa miaka 41. Holding ni mgeni kabisa kwenye
ligi kuu kama hii yenye mikiki mikiki.

Anahitajika beki mkali wa kimataifa wa kucheza na Laurent Koscielny,
kwa sababu Mertesacker na Gabriel hawajapata kuinesha kiwango kikubwa
kabisa kinachofaa.Tumesikia wanataka kumsajili Skhodran Mustafi kwa
pauni milioni 30 lakini kila baada ya muda unasikia pigo jipya kwa
Arsenal. Je, safari hii watafanikiwa? Kulikoni Wenger hafanyi haraka
kuharakisha dili mapema kama wenzake akina Mourinho anasubiri wiki za
mwisho?

Kwa nini hasajili mshambuliaji mkali wa kupachika mabao mengi mengi
kabisa? Msimu jana Arsenal walifunga jumla ya mabao 65 tu sawa na ya
West Ham ambao walishika nafasi ya saba mwisho wa msimu. Ilishaelezwa
tangu awali kwamba wasimtarajie sana Giroud kwa sababu ameonesha
hawezi kuwa aina hiyo ya mchezaji anayetakiwa. Tetesi zinapigwa tu
huko nje kwamba angekwenda Emirates Alexandre Lacazette lakini lini?
Sanchez labda atakuwa mtamu baada ya muda lakini wanahitaji utamu sasa
na si baadaye, ndege haidandiwi.

Maswali bado yapo mengi; kwa nini Walcott ndiye apige penati? Rejea
mechi dhidi ya Liverpool. Walcott alipiga penati vibaya na mpira
ukaokolewa kirahisi na kipa. Unaweza kuhisi kwamba kama si kuikosa
wangeweza kwenda sare au hata Arsenal kushinda kutokana na morali
ambayo ingejengeka baada ya penati hiyo kuzaa bao.

Lugha ya mwili ya Walcott haimwoneshi kuwa mtu mwenye kujiamini na
ilishangaza kumwona akipiga penati wakati hakupata kuwa mpigaji mzuri
ndiyo maana ilikuwa rahisi kwa golikipa Simon Mignolet kudaka penati
ile.
Wenger anayo madaraka kuteua mpiga penati na anatakiwa kuyatumia
kwa busara si kuacha mambo yajiendee tu kama maji ya mkondo ambayo
lazima yasonge uelekeo wa kushuka na si kupanda.

Je, Wenger amepewa kiasi gani cha fedha kwa ajili ya kutumia kwenye
usajili? Kiangazi kilichopita alisajili mchezaji mmoja tu – Petr Cech.
Yeye anasema tu kwamba akipata mchezaji mwenye kiwango anayewafaa
atazitumia fedha hizo, lakini ni ngapi na amepanga kutumiaje? Wengine
wote wanajiwekea malengo yeye anazibanisha benki tu.

Julai aliwaacha washabiki wakitokwa mate kusubiri vifaa vipya lakini
hadi sasa ndio hao wawili tu katika Holding na Xhaka. Alisema mwenyewe
kwamba hawezi kukubali kufanya makosa kwenye dirisha la usajili lakini
hadi sasa keshafanya kibao tu.

Siku chache baada ya kauli ya Wenger, Mtendaji Mkuu wa Arsenal, Ivan
Gazidis amesikika akisema hawawezi kushindana na wenye kiasi kikubwa
zaidi yao cha fedha kwenye usajili. Nani anasema ukweli au walau aliye
karibu na ukweli? Arsenal walitumia pauni milioni 40 wakampata Ozil na
milioni 35 wakawa naye Sanchez miaka iliyopita lakini sasa inaonekana
mtindo ni kusajili mchezaji mmoja tu mkubwa kwa msimu, naona kama
Xhaka tayari yumo ndani ya nyumba kwa pauni milioni 34 huenda kelele
za washabiki juu ya Mustafi na Lacazette zikawa sawa na zile za
mpangaji kwa mwenye nyumba. Watasubiri hadi lini?

Je, huyu mtaalamu wa kupika mabeki, Steve Bould ameshaimarisha ngome
vya kutosha? Ikiwa mabao manne yametumbukia kwenye nyavu zao katika
siku moja tu tutarajie mengine mengi kiasi gani? Matobo hayo
yatazibwa? Kama ni ndio lini? Kuna maswali juu ya uhusiano wa Wenger
na Bould; kwamba hawaelewani vya kutosha. Bould ameingia kwenye kazi
hiyo tangu kustaafu kwa Pat Rice 2012. Bould ni mzuri na alikuwa beki
mahiri hapo Arsenal. Kufungwa mabao 37 tu msimu jana ni rekodi nzuri,
ya pili kwa ubora EPL lakini msimu huu kuna mtihani ikiwa hali ndiyo
hii tuliyoijadili na iwapo haitabadilishwa.

Fungu la maswali yangu ya mwisho wa Wenger linajumuishwa na hili; je,
Wenger anao mpango wa jinsi ya kuondoka Arsenal? Swali hili huwa
linabaki likielea hewani pasipo Wenger na wenzake kutoa majibu
yanayotakiwa. Miaka 12 bila taji, umri wake ni miaka 66 hivyo ni wazi
kwamba kuna siku mwanzo wa mwisho utajitokeza kwake hapo Emirates.

Kama ilivyo kwa Wenger, Gazidis naye anaupiga ukimya tu asipende
kuzungumza hadharani mpango wa kubadili kocha au walau kumwandaa
mrithi kwa siku zijazo isije ikawa ghafla na kusababisha matatizo kama
yaliyotokea Manchester United. Washabiki hulalamika lakini wamekuwa
wakiishia kulia na kuumia wenyewe, maana bosi anajiamini na waliomweka
wamemwachia kila kitu aamue anakaa hadi lini.

Je, Wenger anayo nguvu ya kuwezesha washabiki wake wafurahi na
kupambana na makocha wengine wa EP sampuli ya Jose Mourinho, Pep
Guardiola, Jurgen Klopp, Mauricio Pochettino, Antonio Conte na
wengineo? Nimalizie hapo kwa leo, labda majibu yatapatikana siku moja.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

SIMBA ina thamani ya Bilioni 20?

Tanzania Sports

EPL na moto wake