in , , ,

Arsenal wamewapa somo kubwa Manchester United!

Alidumu kwa muda mrefu sana, yeye ndiye alikuwa nguzo ya mafanikio yote katika kikosi cha Manchester United, alitengeneza utamaduni wa timu kushinda mataji.

Yeye ndiye aliyewaaminisha mashabiki wa Manchester United kuwa, Manchester United iliumbwa kwa ajili ya kuchukua mataji.

Ndiyo maana pale Old Trafford paliwahi kuitwa “Theatre of Dreams”, jina ambalo limeshapotea tangu Sir Alex Ferguson aachane na timu.

Hapaitwi tena ” Theatre of Dreams” na wala Manchester United haiitwi tena “Proud of England”. Kwa kifupi ile alama ya ushindi ilipotea baada ya Sir Alex Ferguson kuondoka.

Inaaminika yeye ndiye aliyeondoka na dawa ya makombe, yamekuwa adimu sana na timu imekuwa siyo ya ushindani tena kama kipindi chake.

Kipindi ambacho kila mwisho wa juma shabiki wa Manchester United alikuwa na uhakika wa kushinda bila kujalisha aina ya timu ambayo wanaenda kukutana nayo.

Kwa sasa imekuwa tofauti sana!, wanaiogopa hata Tottenham Hotspurs. Wanatimu ambayo haina uwezo wa kushindana na vijana wa Mauricio Pochettino.

Mioyo yao haina amani tena hata kama wakikutana na timu ambayo inaonekana ni ndogo. Hawana uhakika tena wa kushinda iwe katika uwanja wao wa nyumbani au ugenini.

Kwa kifupi Manchester United imegeuka kutoka timu ya kuogopwa mpaka kuwa timu ya kuogopa, hawatamani tena mwisho wa juma ufike , kwa sababu roho zao huwa juu mwanzo mpaka mwisho wa mchezo.

Kitu ambacho hakikuwepo kabisa enzi za Sir Alex Ferguson. Kosa ambalo walilifanya ni baada ya Sir. Alex Ferguson kustaafu.

Pamoja na kwamba walichagua kocha ambaye hakuwa wa daraja la Manchester United pia hata aina ya wachezaji ambao walisajili walikuwa ni wachezaji wa daraja la kawaida.

Walimleta Fellain baada ya David Moyes kukabidhiwa timu, mchezaji ambaye alikuwa wa daraja la Kati. Wakamwamini vizuri na kumkabidhi majukumu mazito katika klabu nzito.

David Moyes alianza kuwapeleka Manchester United sehemu ambayo hawakuwa wameizoea katika maisha yao ya soka. Sehemu ambayo haikuwa na furaha hata kidogo.

Taratibu Manchester United wakaanza kuonja ladha ya uchungu baada ya kuzoea kwa muda mrefu ladha ya utamu.

Hawakumvumilia David Moyes, waliamua kuachana naye wakamleta Mholanzi, Louis Van Gaal. Mtu ambaye kwangu mimi nina amini ndiye alikuwa anaijenga Manchester United ambayo ingeweza kuwa na ushindani mkubwa.

Kwa sababu walikuwa bado wanaishi katika pepo la furaha, hawakutaka kabisa kuvumilia maumivu, wakakosa uvumilivu wa kumvumilia Van Gaal.

Jicho lao likamuona Jose Mourinho. Kocha ambaye amezaliwa kushinda tu. Hajazaliwa kutengeneza timu ambayo inaweza kuwasaidia Manchester United kwa muda mrefu.

Ni aina ya makocha ambao wanatumika kwa mipango ya muda mfupi tu. Na kwa sababu Manchester United walikuwa wanataka makombe kwa kipindi hicho ili kurudisha nguvu ya kupigana katika kikosi walimleta Jose Mourinho.

Kwa kiasi fulani walifanikiwa , aliwapa vikombe vitatu. Ukawa Mwanzo mzuri, mwanzo wenye matumaini.

Walianza kupata matumaini kuwa zile siku za neema zikaribu kufika. Lakini ghafla upepo ukabadilika. Manchester United ikakosa ushindani tena.

Yale mategemeo kuwa Jose Mourinho ataifanya Manchester United kuwa ya ushindani yalishindikana. Na tatizo kubwa lilianzia baada ya Sir.Alex Ferguson.

Arsenal walitumia sana busara kumpata mrithi wa Arsene Wenger ambaye alikuwa na uwezo wa kushinda na alikuwa na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya mpira wa sasa.

Unai Emery ameibadilisha sana Arsenal. Hapa ndipo Manchester United walipokosea, baada ya Sir Alex Ferguson kuondoka, kocha ambaye alikuja kuziba pengo lake hakuwa kocha ambaye alikuwa na tabia ya kushinda kitu ambacho kiliifanya Manchester United kuwa timu ya kawaida mpaka sasa.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Arsenal kwa raha zao wanapeta

Tanzania Sports

Miguu ya Modric itamfumbua Neymar