in , , ,

Arsenal waangusha moja moja


*Spurs wafurukuta, Wigan wajaribu kufufuka

Hatua za mwisho mwisho za Ligi Kuu ya Uingereza zinazidi mvuto, timu zikijaribu kuwania nafasi tatu zilizobaki juu na nyingine kuepuka kushuka daraja, ambapo Arsenal na Tottenham Hotspurs wameendeleza mchuano.
Wakati Theo Walcott akiiwekea Arsenal rekodi ya goli la mapema zaidi katika ligi hii kwa kuwatungua Queen Park Rangers (QPR) sekunde ya 20, iliwachukua Spurs dakika 87 kufumania nyavu.
Bao la Walcott dhidi ya QPR wanaofundishwa na Harry Redknapp na ambao tayari wameshashuka daraja, limewarejesha Arsenal nafasi ya tatu, Spurs wa nne na Chelsea wa tano, baada ya Arsenal kutupwa kwa muda nafasi ya tano, kutokana na mchezo wa Spurs dhidi ya Southampton kutangulia kuanza na kumalizika. Hata hivyo, Spurs wa Andre Villas-Boas wana mchezo mmoja mkononi, wakati Chelsea wana miwili.
Alikuwa mchezaji bora wa mwaka na mchezaji bora chipukizi, Gareth Bale aliyewabeba Spurs dakika za mwisho dhidi ya timu yake ya zamani kwa bao hilo pekee na kujiwekea matumaini ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, na kuwaacha Southampton katika sintofahamu ya kubaki au kutobaki Ligi Kuu.
Kabla ya bao hilo la Bale, Saints walikuwa wameweka rekodi ya kucheza dakika 367 bila kukubali bao la ugenini na sasa Bale ameweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi nje ya eneo la hatari kuliko wote msimu huu. Amefunga manane ya aina hiyo.
Aston Villa waendelea kujinasua
Jitihada za kocha Paul Lambert kuwaepusha Aston Villa na hatari ya kushuka daraja iliyokuwa dhahiri wiki kadhaa zilizopita zimeonekana kuzaa matunda, baada ya Jumamosi hii kupata ushindi muhimu.
Villa walipata ushindi wa 2-1 lakini wa kuchelewa Carrow Road, walikocheza na Norwich City, na kwa kuwafunga, wamewasogeza kwenye eneo la hatari ya kushuka daraja kwa nafasi moja iliyobaki baada ya QPR na Reading kuwahi tiketi mbili za awali wikiendi iliyopita.
Shujaa wa Villa alikuwa Gabriel Agbonlahor aliyefunga mabao yote, ukiwa ni ushindi uliokuja baada ya ule wa kimbunga wa mabao 6-1 dhidi ya Sunderland katika mechi iliyopita. Lambert hana wasiwasi mkubwa tena, na alionesha hayo kwa jinsi alivyoshangilia kwa nguvu mwisho wa mchezo, lakini Norwich wanabaki kujiuliza.
Wigan wapigana kiume

English: Gabriel Agbonlahor of Aston Villa FC ...
English: Gabriel Agbonlahor of Aston Villa FC Polski: Gabriel Agbonlahor grający dla Aston Villi (Photo credit: Wikipedia)

Wigan wanaoshikilia mkia kati ya timu ambazo hazijatangazwa kushuka daraja, wamefanikiwa kupata pointi tatu muhimu, ambazo zitahitaji nyingine katika mechi zijazo pamoja na kufanya vibaya kwa timu moja au zaidi zinazokaribiana nayo ili wabaki ligi kuu.
Wigan wenye kawaida ya kubaki mkiani hadi mechi chache za mwisho kabla ya kuchomoa, wanaonekana kuwa katika mazingira hayo hayo mwaka huu, na hata Jumamosi hii walikuwa nyuma ya West Bromwich Albion, kabla ya kuwapandia na kutoka na ushindi wa mabao 3-2 mwishoni. Ushindi huo unawatia kashikashi Sunderland, Newcastle United, lakini pia Norwich na Southampton walio nyuma kwenye jedwali.
Reading wakumbuka shuka asubuhi
Kocha wa Reading, Nigel Adkins amepata ushindi wake wa kwanza tangu aajiriwe kuwanoa Reading, lakini kwa bahati mbaya ushindi huo umekuja baada ya timu hiyo kushuka daraja rasmi.
Reading walifanikiwa kuwachapa Fulham 4-2 ambao wana uhakika wa kubaki ligi kuu, lakini hawawezi kupata ushiriki wa michuano ya kimataifa. Reading walikuwa wakicheza kulinda heshima tu, au kwa kila mchezaji kuonesha uwezo wake kwa ajili ya kuchukuliwa na klabu nyingine za ndani na nje ya nchi kwa msimu ujao.
Newcastle hakieleweki, Man City sare
Newcastle ya Alan Pardew inaelekea kuwa katika mazingira tata, kwani licha ya kutumia mamilioni ya fedha kusajili wachezaji wapya wenye asili ya Kifaransa Januari, wameendelea kufanya vibaya.
Jumamosi hii walitoka suluhu na West Ham United, ambapo wenyewe walijisifu, ikiwa ni baada ya kuchambuliwa kwa mabao 6-0 na Liverpool kwenye mchezo uliopita.
Mabingwa wa msimu uliopita, Manchester City wameshindwa kupata bao katika Liberty Stadium, Wales, baada ya kuvimbiwa na Swansea, licha ya kuwa na nafasi nyingi za kufunga, ikiwa ni pamoja na Edin Dzeko kukosa nafasi ya wazi dakika tano kabla ya kipenga cha mwisho.
City wanaonekana kupoteza ari na nguvu ya kucheza tangu walipofungwa na Spurs, na kuweka msingi wa kombe kuchukuliwa na Manchester United waliowapokonya msimu uliopita. Japokuwa wanabaki nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, hawakuonesha cheche uwanjani, wakati Swansea wanaridhika na nafasi salama waliyo nayo.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Arsenal waingia kinamna Afrika

*AZAM FC KUREJEA NYUMBANI KESHO*