in , , ,

Arsenal ushindi mwembamba

 

 

Arsenal wamepata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Newcastle waliocheza muda mwingi wa mchezo wakiwa 10 baada ya mshambuliaji wao, Aleksandar Mitrovic kutolewa nje kwa mchezo mbaya dhidi ya kiungo mkabaji Francis Coquelin.

Ushindi huu wa pili mwembamba baada ya ule waliopata dhidi ya Crystal Palace, suluhu na Liverpool na kufungwa na West Ham kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya England, ni msisitizo kwamba Arsenal wanahitaji mshambuliaji mahiri wa kati.

 

Washabiki wa klabu hii ya London pamoja na wachambuzi wa masuala ya soka wamekuwa wakimtaka Arsene Wenger kufanya usajili wa nguvu, walau mshambuliaji mmoja mwenye kiwango cha juu ikiwa kweli anataka Arsenal watoe ushindani katika kuwania ubingwa msimu huu.

 

Hata bao la washindi lilikuwa la kujifunga la beki wa Newcastle, Fabricio Coloccini ambapo wageni Arsenal walimiliki mpira kwa asilimia 74, wakapata nafasi nyingi, wakipiga mashuti 22, tisa langoni na kona tisa tofauti na Newcastle waliokuwa na shuti moja tu.

 

Umiliki huo mzuri wa mpira, sawa na mechi iliyopita, ungewapa ushindi mkubwa iwapo wangekuwa na mshambuliaji sampuli ya Karima Benzema ambaye Arsenal walikuwa wakimuwinda lakini inaelekea jitihada zimeshindikana, zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya dirisha kufungwa.

 

Wenge alimwanzisha Theo Walcott katika ushambuliaji wa kati, nafasi ambayo Mwingereza huyo huililia, lakini alishindwa kucheka na nyavu kwa dakika 70 alizokaa uwanjani, hadi akatolewa na kuingizwa chaguo la kwanza hapo, Olivier Giroud ambaye hakubadilisha matokeo, kwani bao lilifungwa dakika ya 52.

 

Bao hilo lilitokana na mkwaju wa kuchonga wa kiungo Alex Oxlade-Chamberlain uliompiga Coloccini na kutinga wavuni. Hata hivyo, Arsenal wameshikilia rekodi yao ya kutofungwa na Newcastle katika dimba la St James’ Park katika ligi tangu Desemba 2005 na wameshinda mechi nane zilizopita hapo, wakifunga mabao 21 na kuruhusu sita tu.

 

Kocha wa Newcastle, Steve ambaye ni mpya bado hajaonja ushindi tangu msimu huu uanze, lakini alisifiwa kwa jinsi walivyowabana Manchester United kwenye mechi iliyopita Old Trafford na kwenda suluhu.

 

Alishamuonya mchezaji wake huyo mpya, Mitrovic, 20, kwamba lazima aoneshe uvumilivu na kutawala hisia zake, maana alishaonyeshwa kadi mbili za njano kwenye mechi zilizotangulia, akisema kwamba kila wakati unaona kama kadi nyekundu ingetolewa, na leo ikatimia. Alisajiliwa kiangazi hiki kwa pauni milioni 13 kutoka Anderletch.

 

Wenger amewasifu wachezaji wake kwa jinsi walivyocheza, akieleza kwamba walikuwa wakijiamini dimbani, wakionesha akili na kukomaa. Walikuwa wakitawala na kufikisha mipira hadi mstari wa mwisho kwa washambuliaji, lakini wakashindwa kupachika mabao.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

BAYERN MUNICH SI KIKWAZO KWA ARSENAL

Tanzania Sports

Chelsea, Liverpool wapigwa