in , , ,

Arsenal: Mwamko wao si wa uongo

*Mourinho amepata ahueni, Spurs nao, lakini …

*Huddersfield, Fulham, Cardiff wako pabaya

WENGI walikuwa wakisema kwamba Arsenal wangeanza kushuka kwa kasi, baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Crystal Palace huku wakijiandaa kuwavaa Liverpool wenye kasi kubwa, lakini vijana wameonesha vinginevyo.

Wakicheza kwa kujiamini katika dimba la Emirates, Arsenal walionesha hata dalili za kushinda mechi hiyo, licha ya Liverpool kutangulia kupata bao kupitia kwa James Milner kabla ya Alexandre Lacazette ambaye sasa anajiamini sana kusawazisha dakika nane kabla ya dakika 90 kukamilika.

Kwa hiyo sasa Arsenal wamekwenda jumla ya mechi 13 chini ya kocha Unai Emery pasipo kufungwa, mechi 11 wakiwa wameshinda na wanaweza kujidai kwa hakika kwamba sasa ni timu tofauti, ikizingatiwa aina ya mchezo walioonesha, ukiwa mkali na wakiwa hawaogopi kupanda kushambulia.

Pamoja na kwamba matokeo hayo na mengine yamewashusha kutoka nafasi ya nne hadi ya tano, wakibadilishana na mahasimu wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur waliowashinda Wolves 3-2 ugenini, bado Washika Bunduki wa London watajipa moyo kwamba kuna matumaini makubwa waendako. Lucas Torreira, kiungo wa Arsenal alikuwa mchezaji bora wa mechi.

Msimamo wa EPL baada ya mechi za jana.

Wakati Kocha wa Liverpool, Mjerumani Jurgen Klopp akisema kwamba kupata alama moja na bao moja ni haki na hata Emery anaweza kufurahia, anaongeza kwamba huenda waliwapa mno Arsenal wakati mzuri. Emery anasema anafurahia kwa asilimia 50 maana alitaka washinde. Liver walikwea kileleni kwa sare hiyo, lakini kubaki hapo inategemea matokeo ya leo baina ya Manchester City na Southampton lakini pia mechi baina ya Chelsea na Crystal Palace.

Jose Mourinho walau ametuliza moyo wake baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Bournemouth katika mechi ambayo ilikuwa ngumu na kama si Marcus Rashford dakika za lala salama, basi Mourinho angeondoka ugenini na alama moja tu. Pamoja na ushindi bado Man U wapo mtaa wa saba, yaani wanashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.

Everton wameanza kuamka ambapo walipata ushindi mzuri wa 3-1 dhidi ya Brighton, Newcastle wa Rafa Benitez nao wakijikongoja kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Watford, wakati West Ham wakiwapiga Burnley 4-2.

Mbio za ubingwa wa EPL sasa zinaonekana kuwa kati ya Liverpool, Man City, Chelsea, Spurs, Arsenal na pengine tuwaweke pia Bournemouth na Man United kwa kutazama tofauti ya amana walizonazo – saba kutoka aliye nafasi ya saba hadi ya wa kwanza, kabla ya mechi ya Man City Jumapili hii. Man U wanazo alama 20 wakati Liver wanazo 27.

Lakini kule chini kuna matatizo makubwa, kwa sababu baada ya mechi 10, Huddersfield wamejiokotezea alama tatu tu, Fulham katika mechi kama hizo wana alama tano wakati Cardiff waliopiga mechi 11 wana alama tano pia. Newcastle wanazo alama sita, Saints saba kabla ya mechi ya leo, Burnley nane sawa na Palace kabla ya mechi ya leo. Wote wamo hatarini na makocha wanatakiwa kuwapandisha kwa kasi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Namkumbuka “MAFISANGO” Kila nikimuona “CHAMA”.

Tanzania Sports

Arsenal kwa raha zao wanapeta