Arsenal mbele kwa mbele

Arsenal mbele kwa mbele

 

Arsenal wamewafyatua Liverpool mabao 2-0 na kufanya uongozi wao kwenye ligi kuu kuwa kwa tofauti ya pointi tano.

Wakicheza nyumbani katika uwanja wa Emirates, Arsenal walikuwa na shinikizo baada ya kupoteza mchezo wa Kombe la Ligi dhidi ya Chelsea, lakini walicheza vizuri.

Arsenal walionesha kiwango cha hali ya juu ambapo wauaji walikuwa Santi Cazorla na Aaron Ramsey wakimwacha kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers akishangaa.

Arsenal ni timu pekee iliyofunga goli au magoli katika kila mechi msimu huu katika ligi kuu.

Chelsea waliadhibiwa kwa mshangao wa wengi na Newcastle kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Yoan Gouffran na Loic Remy katikakipindi cha pili.

Jose Mourinho hakuamini macho yake kwa kupigwa na timu ambayo msimu huu haijawa nzuri sana na pia Chelsea walikuwa wameshinda mechi zao sita zilizopita.

Manchester United walifarijika kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fulham na hivyo kumwacha kocha Martin Jol katika wakati mgumu.

Mabao yao yalifungwa na Antonio Valencia, Wayne Rooney na Robin van Persie.

Manchester City kwa upande mwingine walipata ushindi mkubwa zaidi katika ligi kuu kwa kuwafunga Norwich 7-0.

Katika mechi nyingine Hull waliwafunga Sunderland 1-0, Stoke wakaenda sare ya 1-1 na Southampton, West Bromwich Albion wakawafunga Crystal Palace 2-0, West Ham wakaenda suluhu na Aston Villa.

Kwa matokeo hayo, Arsena wanaongoza ligi kwa pointi 25 wakifuatiwa na Chelsea na Liverpool wenye pointi 20.

Man City, Southampton na Tottenham wana pointi 19 kila moja wakati Everton wakiwa na pointi 18.

Manchester Unite licha ya ushindi wao wanabaki katika nafasi ya nane kwa pointi 17 wakifuatiwa na Newcastle, Hull, West Brom, Swansea, Villa, West Ham, Fulham, Stoke na Cardiff.

Comments