in , ,

Arsenal, Man Utd, moto mkali, Chelsea, City doro

*Timu nne bora zilizozoeleka zajikita kileleni

*Man United yavuna, Liverpool mambo bado

Mzunguko wan ne wa Ligi Kuu ya Uingereza umeshuhudia mwendelezo wa makubwa kadhaa, ukiwamo moto ulioanzishwa na Arsenal.
Timu ‘ndogo’ zilizokuwa zinashika nafasi za juu zimefurushwa, huku nne bora zikirejea zile zilizozoeleka.
Hata kama itakuwa ni kwa muda, lakini Arsenal, Chelsea, Manchester City na Manchester United zimerejea maeneo zinakopenda kuita nyumbani.
Arsenal na United zilirejea baada ya karamu kubwa za mabao, huku Chelsea na City zikitoa sare.
Arsenal iliifunga Southampton mabao 6-1, idadi ambayo ni kubwa kwa Washika Bunduki wa London waliokuwa na mabao mawili tu ya kufunga katika mechi tatu zilizotangulia.
Hata hivyo, Arsenal pia kwa mara ya kwanza msimu huu imeruhusu bao, langoni akiwa amerejea golikipa namba moja, Wojciech Szczesny, aliyeonekana kutotulia vyema langoni kama Vito Mannone aliyedaka mechi mbili zilizopita.
Nyota mpya wa The Gunners, Lukas Podolski alipata bao la pili la msimu, huku Gervais Lombe Yao Kouassi ‘Gervinho’ akifunga mawili na kijana The Walcott naye akipachika bao. Mawili walijifunga Southampton wenyewe.
Swansea walioanza kwa kasi msimu na kukalia uongozi wa ligi, wameanza kufungwa, baada ya kuchambuliwa mabao 2-0 na Aston Vlla ambayo msimu uliopita ilikosa makali.
Huu ni ushindi wa kwanza kwa Aston Villa, waliopata mabao kupitia kwa Matthew Lowton  na mchezaji wake mpya kutoka Genk ya Uholanzi, Christian Benteke, raia wa Ubelgiji na Kongo.
Timu nyingine iliyokuwa ikijidai juu ya msimamo wa ligi ni West Bromwich Albion ambao wamekung’utwa mabao 3-0 na timu ngumu ya Fulham.
Alikuwa ni mkongwe Dimitar Berbatov aliyetokea Manchester United dakika za mwisho za usajili msimu huu aliyewafungia wageni mabao mawili, moja kwa penati. Jingine lilitiwa kimiani na Steve Sidwell, mechi ikikaribia kumalizika.
Ilikuwa siku mbaya kwa Peter Odemwingie wa Fulham, aliyepata kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumkwatua Sascha Riether.
Norwich iliendelea na rekodi yake ya kutoshinda mechi hata moja, baada ya suluhu yake nyumbani dhidi ya West Ham United wanaofundishwa na mkongwe Sam Allardyice.
Mashetani Wekundu waliungana na Arsenal kwa karamu ya mabao, siku hii ambayo mchezaji wa, Paul Scholes  alicheza mechi ya 700.
United walicheza dhidi ya timu isiyotabirika ya Wigan inayofunzwa na Roberto Martinez, ambapo Scholes aliungana na Javier Hernandez; Alexander Büttner na Nick Powell kufunga.
Mfungaji mpya wa United, Robin van Persie hakupata kitu kwenye mechi hiyo, na aliingia dakika ya 71. Pia Hernandez alikosa penati iliyodakwa na kipa Ali Al-Habsi, kama alivyokosa RVP mechi iliyopita dhidi ya Southampton.
Queens Park Rangers (QPR) ilitoshana nguvu na  Chelsea kwa kutoka suluhu, ikidhihirisha maneno kwamba Chelsea licha ya kushinda mechi zilizotangulia, haikuwa imekaa imara sana.
Mechi ilishuhudia mchezaji wa QPR, Anton Ferdinand akikataa kumpa mkono John Terry anayedaiwa kumtukana kibaguzi na Ashley Cole aliyemtetea Terry mahakamani.
Vijana wa Roberto Mancini nao walishindwa kuwabanjua Stoke City, baada ya kutoka nao sare ya bao 1-1.
Stoke walitangulia kufunga kupitia kwa mkongwe Peter Crouch kwa ‘mkono wa mungu’. City walikomboa bao kupitia kwa mchezaji mpya, Javi Garcia.
Michael Owen aliyesajiliwa na Stoke kama mchezaji huru baada ya dirisha la usajili kufungwa, aliingia dakika ya 90 kuchukua nafasi ya Crouch. Bila shaka ataanza siku zijazo.
Ukame wa ushindi umezidi kuiandama Liverpool ya Brendan Rodgers, baada ya kuambulia sare ya bao 1-1 nyumbani kwa Sunderland.Liverpool walitanguliwa kutunguliwa katika dakika ya 29 kupitia mchezaji mpya kutoka Wolverhampton Wanderers, Steven Fletcher, kabla ya Luis Suarez kupunguza majonzi dakika ya 71.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Pre-match handshakes, or the absence of them, overshadowed the eight fixtures in the EPL

Resurgent Prisons, Azam end voodoo