in

ANAYEMNG’ATA SIKIO AJIB ASHIKE NA KIBOKO, BAADA YA MACHWEO NI GIZA.

Hakuna kitu muhimu katika maisha kama kuyatumikia ipasavyo maisha yako.

Maisha yako huwa yanakuwa mikononi mwako, muda wote huwa unazunguka
nayo kila uendako.

Mikono ya mwanadamu ndiyo imebeba siri kubwa ya mafanikio yake. Na
siri kubwa kuhusu mikono ni kuwa hupenda kushika vitu vizuri siku
zote.

Chochote kibaya kinaposhikwa mkononi maji huitajika kuliko kitu
chochote kusafisha mikono. Hakuna zawadi nzuri utakayoipatia mikono
yako kama pesa nyingi, chakula kizuri ili kiburudishe tumbo lako zuri,
mikono hupiga vigelegele pindi inapokuwa imeshika kiuno cha mwanamke
mzuri barabarani maana ni moja ya kitu kizuri duniani.

Hii ni fahari kubwa ya mikono, hatima ya maisha yetu huwa mikononi
mwetu siku zote, furaha na huzuni ya maisha yetu huwa mikononi mwetu
hapa huja chaguzi na mwanadamu mwenyewe ni ndiye uhusika kuchagua kipi
anakitaka katika maisha yake kati ya furaha na huzuni.

Furaha katika maisha ndiyo huwa chaguo là watu wengi sana duniani
,kila mtu huwa anatamani kuishi na furaha kwenye siku zote za maisha.
Hakuna anayependa matatizo kwenye maisha yake ingawa hayakwepeki.
Matamanio yetu ni furaha siku zote ambayo hufanana kwa kila mwanadamu.

Tunafanana sana kwenye matamanio yetu lakini tunapishana kwa kiasi
kikubwa namna ya kutafuta njia za kuyafikia matamanio yetu.

Njia zetu ni tofauti sana, hata hatua zetu zinatofautiana katika
upigaji. Hii yote inaonesha binadamu wote hawafanani na wanamapungufu
yao.

Mapungufu ambayo yanatupa nafasi ya kushauriana na kuelekezana njia
sahihi za kupita ili kufikia matamanio ya kila mmoja wetu. Waweza
ukawa katika njia sahihi lakini ukawa hupigi hatua sahihi za kuelekea
katika matamanio yako.

Hapo ndipo unapohitaji mtu sahihi wa kukuelekeza namna ya kupiga hatua
sahihi. Ndipo hapo Ajib anapokwama.

Sijajua tatizo liko wapi, ila inavyoonesha mtu anayemshauri siyo
sahihi au anashauriwa na kuupuzia ushauri.

Inauma kila mawio hukutana na Ajib pale Kariakoo, wasiwasi
umeshampotea moyoni mwake hata pale machweo anavyoyashuhudia kwa macho
yake.

Inauma sana kuzeeka ukiwa umeliangalia jua kwani pamoja na kuzeeka
masikini, upofu utakuwa nduguyo.

Mwanga wa uzeeni hutouona, uzee wako utatawaliwa na giza, mwanga kwako
utausikia kwenye hadithi za wajukuu wako watakaokuwa wanaanika mahindi
juani huku wakikuzomea bila ya wewe kuona. Jua litakuwa adhabu kwako
tena uzeeni, halitotumika tena kama mwangaza wako wa kukusaidia kuona
kwa sababu muda huo utakuwa kipofu, kila sekunde kwako giza litakuwa
limetawala mboni za macho yako.

Sijajua kwanini Ajib amefurahia kulitazama jua kuanzia asubuhi mpaka
jioni, nahisi aliyemwambia ule msemo wa mchumia juani hulia kivulini
alifanya kosa kubwa sana kuondoka bila kumpa tafasiri yake.

Ajib amebaki akiwa juani amesimama huku akiamini siku moja atakula
akiwa kivulini, kusimamà peke yake ukiwa unaliangalia jua Ajib
haitoshi. Unatakiwa upigane kwa kulikimbiza jua tena ukiwa juani.

Jua halina utamaduni wa kusimama na kumsubiri mtu, mwanadamu anatakiwa
akimbie kwa kasi ya kuizidi kasi ya jua ili afanikiwe kwa kiasi
kikubwa.

Unatakiwa uende na muda, usiruhusu nyakati zikuache unaweza kujikuta
unalima nyakati za kiangazi.

Nyakati tulizonazo katika mpira wa kisasa ni nyakati za takwimu.
Takwimu ndiyo humuuza mtu mahali popote .

Ule wakati wa mpira sanaa haupo tena umeshaenda na kina Ronaldinho na
Jay Jay Okocha. Hakuna kocha anayeruhusu kutekwa na hisia za mpira
sanaa tena.

Makocha wengi wa sasa sanaa ya mpira haipo kwenye matamanio yao ndiyo
maana wachezaji wa namna hii wanapotea sana.

Ajib ni mshambuliaji anachotakiwa kuwa nacho kwenye akaunti yake ni
idadi kubwa ya magoli na pasi za mwisho za magoli.Hizo chenga
anazopiga hazina msaada kwenye akaunti yake.

Utakuwa kichaa pindi utakapokataa Ajib ni mchezaji mzuri, ana work
rate kubwa ana sanaa kubwa lakini anacheza sana na jukwaa.

Anafanya vitu vingi ambavyo havina msaada mkubwa katika timu kiufundi
ndiyo maana anabaki kuwa mchezaji mzuri na siyo bora.

Kuibeba timu kwa magoli yake ndicho kitu anachohitaji kukifanya muda huu.

Timu haibebwi na yeye kucheza na jukwaa, magoli yake, nafasi za magoli
anazotengeneza ndivyo vitu vinavyohitajika kwenye timu yake pamoja na
kwenye maisha yake ya soka. Bila vitu hivo, jua litachomoza na kuzama
kila siku nakumkuta sehemu ile ile aliyosimamia jana.

Ndipo hapo muda utakuwa umemwacha, na kwenda kwa mwingine anayejua
kuutumikia vizuri.

Hilo kwake kwa muda huu halioni, ndiyo maana pumzi humkata mapema na
hii inaonesha hana mazoezi ya pumzi .Njaa ya mafanikio haipo ndani
yake ndiyo maana suala là pumzi ni tatizo kwake.

Miaka inaenda mbele, hata kule uarabuni wanapohesabu namba kwa kurudi
nyuma hawajawahi kufanikiwa kuzifanya siku zirudi nyuma, hii yote
inaonesha kuwa kila nafasi uliyonayo unatakiwa uitumie ipasavyo maana
ni ngumu kurudisha muda unaopoteza

Ni aibu sana kushiba wakati wa ujana wako na kulia njaa wakati wa uzee
wako. Ajib, Simba haitokupa shibe ya uzeeni.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Huyu ndiyo kiungo mzawa mkabaji anayekosekana pale Yanga

Tanzania Sports

MECHI ZA KIMATAIFA WIKI HII ZIMETUACHA NA DARASA KUBWA SANA