in , ,

ALICHOFANYA BECKHAM 2015: KINADHIHIRISHA UWEZO WA MICHEZO KUINUA JAMII

*Beckham aliamua kucheza mechi saba za mpira, mabara saba, katika siku kumi*

Mwaka 2015 ulikuwa na matukio makubwa na madogo. Shirikisho la Mpira duniani (FIFA) lilisakamwa na kashfa ya wizi wa fedha na viongozi Sepp Blatter na Michel Platini walitiwa mbaroni. Kocha Jose Morinho alitimuliwa na Chelsea. Kabla ya hapo Bw Mourinho alikinzana na mganga wa timu ya klabu hiyo, Dk Eva Carneiro…

Pambano la wanamasumbwi Manny Pacquiao na Flyod Mayweather mwezi Mei lilimalizika kwa utata baada ya Mayweather kutozwa faini ya dola laki mbili alipokwepa malipo ya udhuru wa mapigano hayo ya uzito wa “welterweight”.

Bondia mwingine wa uzito wa juu (heavyweight), Tyson Fury alimnyuka Wladimir Klitschko mwishoni mwishoni mwa 2015. Hata hivyo Mwingereza huyo mwenye kelele na mbwembwe nyingi alizua maneno baada ya kutoa hoja zake binafsi kuhusu anavyowaona wanawake na mashoga. Vyombo vya habari vilimsakama kwamba avuliwe taji lake. Lakini wapambe wengi walimtetea kuwa ni mwanamichezo mzuri na maoni yake binafsi hayana madhara katika ngumi.

Kashfa hizi lakini hazikufua dafu juu ya nia njema ya mchezaji maarufu wa Uingereza David Beckham. Beckham ( 40 ), alijiuzulu kandanda mwaka 2013 baada ya kuchezea timu za Manchester Uinted, Real Madrid, PSG, AC Milan na LA Galaxy kwa kipindi cha miaka 20.

Mwaka 2005 Beckham aliteuliwa kuwa balozi mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya maslahi na elimu ya watoto (UNICEF). Beckham ameishika shughuli hii ya fadhila kwa mikono miwili akitumia jina na umaarufu wake.
Mwezi Novemba Beckham aliamua kucheza mechi saba za mpira, mabara saba, katika siku kumi . Ingawa ilikuwa shughuli ngumu ilikuwa na madhumuni ya kuonesha matatizo ya watoto wadogo duniani na kukusanya fedha za kuwakimu.

Beckham: “ Mwaka 2014 ulikuwa kati miaka mibaya sana kwa ukatili wa watoto , hivyo tunajaribu kurekebisha mambo kwa kusaidia watoto duniani. Hii ni njia nzuri ya kufanikisha hilo.”

Beckham ambaye aliwahi kufanyiwa sinema inayotukuza ufundi wake wa kufunga mabao au kupiga pasi kwa mbali (Bend it Like Beckham) alianza safari visiwa vya Papua Guinea. Baada ya kupokewa kwa shamra shamra, maua na vigelegele, alicheza na timu za vijijini akitumia mpira uliotengenezwa kwa majani makavu. Baadaye alikaa na wenyeji akishangaa namna wanavyokula vibaya ilhali Papua Guinea ina rutuba na mazao mengi.

Wenyeji hula viazi vitamu na vinywaji kama Cocacola na kuuza vyakula vya bora ughaibuni. Matokeo watoto wana utapia mlo. Nchini Nepal bara Asia, David Beckham alioneshwa madhara ya tetemeko la ardhi la mwaka 2015.

Mechi ilihudhuriwa na watu wengi kiasi ambacho ilibidi mwanasoka huyo na wenzake waondoke haraka haraka kupitia milango ya nyuma. Bara Afrika Beckham alicheza na wakimbizi wa Kisomali nchini Djibouti. Alionesha kuvutiwa na namna vijana hao walivyokuwa makini. Alikiri wakipewa nafasi nzuri wataimarika sana. Alielekea Buenos Aires na ukanda wa barafu ya Antarctica.

Ingawa Uingereza na Argentina si marafiki kimpira Beckham hakuzungumzia siasa wala kuonesha kupendelea upande mmoja kuliko mwingine. Alivaa jezi ya Argentina na kupiga picha na wenyeji. Alikaribishwa kinywaji na watu wa kawaida. Aliwasifu watoto wadogo wa klabu ya Boca Juniors jijini Buenos Aires.

Klabu hii ndiyo iliyomtoa mwanasoka maarufu Diego Maradona zamani. Baadaye alikwenda Miami alipocheza na wanawake vijana wasomi . Nchini Marekani soka si mchezo wa wanaume bali unafagiliwa zaidi na wanawake. Beckham alifurahishwa sana na ufundi wa wasichana hawa. Hatimaye aliruka uwanja wa Old Traford, siku kumi kamili akajiunga na timu ya Uingereza dhidi ya timu ya dunia iliyoongozwa na Luis Figo na wenzake wastaafu, Ronaldinho, Cafu, nk.

Wachezaji wengi wastaafu Paul Scholes, Michael Owen, Dwight Yorke na James Caragher walithibitisha bado wangali wakali uzeeni.Bahati mbaya Zinedine Zidane na Patrick Vieira hawakucheza kwa heshima ya janga lililotokea Paris juma hilo la Novemba 14.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Mwaka mpya Arsenal juu

Tanzania Sports

Arsenal bado kileleni