in

Al Ahly ni kibonde wa Simba

Mpambano wa nguvu

Mabingwa wa Ligi kuu Tanzania bara klabu ya Simba wameanza kwa mguu mzuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Kundi A. Simba wamecheza mechi mbili za Kundi A huku wakiendeleza wimbi la ushindi kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya kigogowa soka wa Misri na Afrika klabu ya Al Ahly. Katika mchezo wa pili uliochezwa jumanne wiki hii Simba waliendeleza ubabe mbele ya Al Ahly na kuichakaza bao 1-0. Makala haya yanakuletea mambo adimu ya mchezo wa Simba na Al Ahly.

Simba wamevunja mwiko wa Pitso Mosimane

Katika mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa, klabu ya Simba imefanikiwa kuwafunga mabingwa watetezi kwa bao 1-0 lililofungwana Luis Miquissone raia wa Msumbiji. Simba ni timu ya kwanza kumfunga kocha Pitso Mosimane tangu kuwa kocha wa Al Ahly kutoka barani Afrika. Ni mabingwa wa Ulaya na Dunia pekee Bayern Munich ndiyo timu iliyomfunga Mosimane. Hii ina maana katika bara la Afrika ni klabu ya Simba pekee imefanikiwa kunyanyasa Al Ahly.

Waarabu hawajashinda Dar es salaam ya Simba

Simba wameweka rekodi ya aina yake baada ya kudumisha historia ya kutofungwa na timu za kutoka nchini Misri hapa nchini.

Tanzania Sports
Mchezaji wa Simba

Takwimu ziko hivi; Mwaka 1974 Simba alimchapa Mehala Al Kubra 1-0. Mwaka 1985 Simba walimchapa A Ahaly mabao 2-1. Mwaka 1996 Simba tena wakaifumua Mokawloun mabao 3-1. Mwaka 2001 Simba waliitandika Ismailia bao 1-0.

Mwaka 2003 Simba walitoka suluhu na Ismailia 0-0. Mwaka 2003 Simba waliizaba Zamalek bao 1-0. Mwaka 2010 Simba waliitungua Al Hodoud mabao 2-1. Mwaka 2018 Simba walitoka sare 2-2 na Al Masry. Halafu ukaja mwaka 2019 Simba walifunga bao 1-0 Al Ahly.

Al Ahly  yageuzwa kibonde kwa Simba

Kwenye mpira wa miguu zipo timu ambazo ni kibonde cha mwingine. Katika historia ya soka nchini kati ya timu za Misri na Tanzania, Simba wamefanikiwa kuigeuza A Ahly kuwa kibonde wao.

Simba wamefanikiwa kuichapa Al Ahly mara tatu katika historia yao. Mwaka 1985 Al Ahly walipigwa 2-1 na Simba. Mwaka 2019 Al Ahly walipigwa 1-0 na Simba. Na mwaka 2021 Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi wamepigwa tena bao 1-0 na Simba.

Hii inaonesha namna Al Ahly walivyo vibonde vya Simba. Al Ahly wamefungwa katika karne  mbili. Kwneye karne ya 20 wamechapwa na karena ya 21 wametandikwa hadi sasa hivyo kushindwa kuibuka na ushindi jijini Dar es salaam.

Mabao machache pointi nyingi

Katika mchezo wa kwanza Simba walishinda ugenini dhidi ya timu ngumu ya AS Vita nchini DR Congo 1-0. Mchezo wa pili pia wameshinda kwa bao 1-0 wakiwa dimba la nyumbani jijini Dar es salaam na kuongoza msimamo wa kundi A.

Simba wana pointi 6 na mabao mawili. AS Vita wenye pointi 3 baada ya kuwachapa Al Marreikh ya Sudan mabao 4-1. Al Ahly inashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 3 na mabao manne.

Al Marreikh wanashika mkia katika kundi hilo wakiwa hawana pointi yoyote baada ya kufungwa michezo miwili dhidi ya Al Ahly na AS Vita.

Wachezaji sita wageni,watano wazawa

Tanzaniasports hivi karibuni ilifichua namna wachezaji wa Tanzania waliopo Simba wanavyokabiliwa na changamoto kupenya kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Didier De Gomes.

Katika mchezo dhidi ya AS Vita, kikosi cha kwanza cha Simba kilikuwa na wachezaji 7 wa kigeni, wakati wazawa walikuwa wanne. Wachezaji wa kigeni walikuwa Cletous Chama (Zambia), Larry Bwalya (Zambia), Pascal Wawa (Ivory Coast),Luis Miquissonne (Msumbiji), Tadeo Lwanga (Uganda), Chris Mugalu (DR Congo) na Joas Onyango (Kenya).

Kwenye kikosi cha kwanza wachezaji wazawa walikuwa wanne pekee; golikipa Aishi Manula, nahodha na beki wa kushoto Mohammed Hussein, beki wa kulia Shomari Kapombe na kiungo mkabaji Mzamiru Yassin.

Tukigeukia upande wa wachezaji wa akiba walikuwa Gadiel Michael (Tanzania), Kennedy Juma (Tanzania), Said Ndemla (Tanzania),Meddie Kagere(Rwanda),Bernard Morrison(Ghana), na Francis Kahata (Kenya).

Hiyo ina maana wachezaji wa kitanzania katika benchi la Simba walikuwa watatu pekee. Kati ya wachezaji hao wa akiba ni mtanzania Kennedy Juma, Mnyarwanda Meddie Kagere na Mkenya Francis Kahata ndiyo walipata nafasi ya kuingia dimbani.

Simba dhidi ya Al Ahly kulikuwa na wachezaji watano wazawa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein,Mzamiru Yassin na Hassan Dilunga. Wachezaji wa kigeni walioanza walikuwa sita; Joash Onyango, Pascal Wawa,Cletous Chama,Chris Mugalu na Luis Miquisson.

Wachezaji wa akiba walikuwa Beno Kakolanya(Tanzania), Kennedy Juma (Tanzania), Erasto Nyoni(Tanzania), Larry Bwalya (Zambia), Meddie Kagere(Rwanda),Bernard Morrison (Ghana) na Francis Kahata (Kenya).

Hii ina maana wachezaji wazawa 9 wa Simba walihusika kwenye mchezo dhidi ya Al Ahly, pamoja na wageni 9. Hii inatokana na mabadiliko ya wachezaji watano kwa mujibu wa sheria mpya za CAF ikiwa ni njia ya kukabiliana na tatizo kwa timu inayoweza kukabiliwa na ugonjwa wa corona.

Mshindi wa tatu wa dunia awa uchochoro ‘Kwa Mkapa’

Al Ahly iliwasili nchini Tanzania siku chache baada ya kutoka kwenye mashindano ya klabu Bingwa Duniani. Katika mashindano ya klabu bingwa, Al Ahly ilitolewa katika hatua ya nusu fainali na mabingwa wa Ulaya Bayern Munich kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Robert Lewandowski.

Al Ahly walishika nafasi ya tatu baada ya kuwafunga Palmerais ya Brazil kwa matuta. Lakini kwenye mchezo dhidi ya Simba ni dhahiri Al Ahly walizidiwa maarifa na kugeuzwa uchochoro.

Katika soka timu kubwa kuzidiwa mchezo ni jambo la kawaida, lakini inafurahisha zaidi pale unapoona bingwa mtetezi anateseka kupata matokeo mazuri.

Al Ahly bila shaka wameondoka ‘Kwa Mkapa’ wakiwa wamepata darasa zuri la soka. ndio maana nyota wa zamani wa Al Ahly Wael Gomaa amemlalamikia kocha Pitso Mosimane kuwa chanzo cha timu yao kuambulia kipigo jijini Dar es salaam.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Carlinhos

Carlinhos ni kama mwalimu wa zamu

Ferland Mendy celebrates his strike

Refa ameharibu ushindi wa Real Madrid