in , , ,

AFCON 2017: SARE ZATAWALA MICHEZO YA UFUNGUZI

Gabon, wenyeji wa Kombe La Mataifa ya Afrika (AFCON 2017), wamelazimishwa sare ya 1-1 na Guinea Bissau kwenye mchezo wa Kundi A. Mchezo huo uliokuwa wa ufunguzi ulipigwa ndani ya dimba la Stade de l’Amitie usiku wa jana Jumamosi.

Nafasi ya kwanza ya bao kwa Gabon ilikuja ndani ya dakika ya 20 kwa Malick Evouna lakini mshambuliaji huyo anayecheza soka huko nchini China alishindwa kuuweka wavuni mpira safi aliopelekewa na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang.

Wenyeji hao waliopewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo hawakuweza kuonesha chochote cha maana ndani ya kipindi cha kwanza ambapo nyota wao kama Aubameyang wa Borussia Dortmund na Mario Lemina wa Juventus walionekana wachezaji wa viwango vya kawaida kabisa.

Guinea Bissau ambao ni kwa mara ya kwanza wanashiriki michuano hii walijitendea haki mno kwenye kipindi hicho cha kwanza hasa kwenye safu ya ulinzi iliyomjumuisha pia Rudinilson Silva ambaye ni mchezaji huru.

Mapema kwenye kipindi cha pili nahodha Pierre-Emerick Aubameyang aliwapatia wenyeji bao la kuongoza ndani ya dakika ya 52 akiunganisha wavuni krosi safi ya chini kutoka kwa Denis Bouanga anayekipiga katika klabu ya Tours FC iliyo ndani ya Ligi Daraja La Pili ya Ufaransa.

Bao hilo lilidumu kwa takribani dakika 40 huku Toni Silva na Frederick Mendy wakikosa nafasi za wazi za kuwasawazishia Guinea Bissau mbaka pale mlinzi Juary Soares alipofunga kwa kichwa ndani ya dakika ya 91 na kuufanya mtanange huo umalizike kwa matokeo ya 1-1.

Kwenye mchezo mwingine wa Kundi A mabingwa mara nne wa mashindano haya, Cameroon pia walishindwa kuvuna alama 3 muhimu walizozihitaji kwenye mchezo huo baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Burkina Faso hiyo jana.
Kiungo Alain Traore wa Kayserispor ya Uturuki alikaribia kuwapatia Burkina Faso bao la kuongoza kabla ya Benjamin Moukandjo kuwaweka mbele Cameroon kwenye kipindi cha kwanza ndani ya dakika ya 35.

Mshambuliaji huyo anayechezea Lorient ya nchini Ufaransa alifunga moja kwa moja kupitia mpira wa adahabu kwa shuti kali lililompita mlinda mlango licha ya kujikunjua vyema akijaribu kulizuia.

Bao hilo la kuongoza lilidumu hadi kufikia mapumziko. Ndani ya kipindi cha pili Cameroon waliendeleza makali yao kwa kutengeneza nafasi kadhaa za mabao lakini hakuna iliyoweza kuwapatia bao la pili ikiwemo ya wazi aliyoipata Clinton N’Jie.

Dakika 15 kabla ya mchezo kumalizika Burkina Faso wakapata bao la kusawazisha kupitia kwa Issoufou Dayo aliyefunga kwa kichwa baada ya mlinda mlango wa Cameroon Fabrice Ondoa kushindwa kuuondosha ndani ya eneo la hatari mpira wa adahabu uliopigwa na Banou Diawara.

Kwa matokeo ya michezo hiyo miwili timu zote nne za kundi hilo ziko na alama sawa, kila moja ikiwa na alama 1, idadi inayofanana ya magoli ya kufunga (1), idadi sawa ya mabao ya kufungwa (1) na pia tofauti sawa ya mabao (0).

Michezo mingine ya kundi hili itapigwa siku ya Jumatano ambapo wenyeji Gabon watajitupa uwanjani kumenyana na Burkina Faso huku Cameroon wakitupa karata yao ya pili dhidi ya Guinea Bissau.

Leo Jumapili kutakuwa na michezo mingine miwili ya Kundi B linalosemwa kuwa kundi gumu zaidi ambapo Algeria watacheza na Zimbabwe huku Tunisia wakivaana na Senegal. Michezo yote hiyo miwili itapigwa ndani ya uwanja wa Stade de Franceville.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

UCHAMBUZI WA MAKUNDI YA AFCON.

Tanzania Sports

Van Gaal astaafu