in

Wenger: Nasoma yanayonisaidia kuwaelewa binadamu

Arsène Wenger

Arsene Wenger – Mfaransa msomi aliyebadilisha kabisa soka ya England mara nyingi amekuwa akijifikirisha atamwambia nini Mungu siku atakapofariki dunia. Kuna msisimko juu ya kujua maswali na majibu yatakuwaje huko kwenye lango la njiapanda ya Mbinguni na Motoni.

Katika maulizo na majibizano hayo, Mungu anamuuliza Wenger kuonesha uhalali wa muda wake alivyoutumia duniani, jinsi alivyoipa zawadi ya Maisha yake maana kwake binafsi na kwa wengine.

“Nilijaribu kushinda mechi za soka!” Wenger ataeleza. Mungu anamwangalia, Wenger anapatwa wasiwasi. “Hiyo tu?” Wenger anaendelea; “kushinda mechi ni ngumu sana. Ukifanya kazi yako vizuri, unawapa raha mamilioni ya watu, vifijo vya aina yake. Usipofanya kazi hiyo vizuri …” hapa Wenger anarudi kwenye uhalisia wa mambo.

“Wakati mwingine najihisi kuogopa kutokana na ukweli kwamba katika Maisha yangu nimefanya soka tu,” anasema Wenger (70) katika mahojiano kutoka Zurich, Uswisi yaliko Makao Makuu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambako Wenger ni ofisa mwandamizi.

“Kwa hiyo, napozungumza na Mungu kuna kuongeza chumvi kidogo. Hiyo ni ikiwa kweli Mungu yupo na ikiwa watataka kuuliza maswali kwa ajili ya kujiridhisha iwapo unakwenda Motoni au Mbinguni. Yaweza kuonekana ujinga kwa kujikita maisha yako yote kwenye kushinda mechi za soka. Na ndiyo maana nikaja na wazo hilo. Wakati mwingine inaweza kuhisiwa kwamba hakuna maana yoyote kutolea maisha yako yote kwa ajili hiyo,” anasema Wenger.

Wenger alizaliwa 1949 na kukulia katika Kijiji cha Alsace, Mashariki mwa Ufaransa na aliweza kutazama kwa mapema sana saikolojia ya wanadamu, akiwatazama madingi waliokuwa wakifika kwenye mgahawa mdogo (bistro) ambao wazazi wake walikuwa wakiendesha.

“Kilevi, kupigana, vurugu, kila kitu ambacho kilikuwa kikitisha na kunitia karaha kama mtoto,” anakumbukia kwenye tawasifu yake mpya aliyoandika ikienda kwa jina la ‘My Life in Red and White’ inayoweza kupewa tafsiri isiyo rasmi; ‘Maisha Yangu ndani ya Nyekundu na Nyeipe’, zikiwa ni jezi za nyumbani kwa Arsenal – Highbury na kisha Emirates.

Alitokea kuja kuwa kiungo mgumu uwanjani, akapanda hadi kuchezea Strasbourg kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa – Ligue 1. Ana kawaida ya kuwa na fikara ya kina sana juu ya gemu ambayo akiwa mwanzoni mwa miaka yake ya 30 alisonga kutoka kucheza na kuwa kocha. Alianzia ukocha Cannes na Nancy za Ufaransa kisha Monacho halafu akaenda Japan alikofundisha Nagoya Grampus Eight.

Ilikuwa mwaka 1996, Wenger, jamaa mmoja mrefu hivi, akiwa amevaa suti yake aligusa fahamu za Waingereza, alipotangazwa na Arsenal kuwa kocha wa nne wa kigeni katika historia ya Ligi Kuu ya England. (watatu wa awali hawakufanya vyema). Alikalia kiti hicho kwa miaka 22 hadi 2018, kipindi ambacho Arsenal walitwaa ubingwa mara tatu na ubingwa wa Kombe l FA mara saba.

Wakati hasimu wake mkubwa katika Manchester United alikuwa Alex Ferguson aliyempokea kwa bezo alipotoka Japan, akisema hakuwa lolote wala kuujua soka, Wenger alithibitisha kwamba Fergie alikosea, kwani alibadili kabisa mfumo wa soka. Kuanzia uwanja wa mazoezi, kwenye mechi, katika vyumba vya kubadilishia nguo hadi mfumo na aina ya vyakula kwa wachezaji wake, washabiki wakampenda hasa.

Akisisitiza nia ya kushinda, lakini zaidi kushinda kwa mtindo wa kuvutia, Wenger anasema kwenye tawasifu yake kwamba kwake soka na Arsenal ni ‘suala la kufa na kupona’ – na hasemi hivyo mara moja, bali mara tatu.

Je, anamaanisha hivyo kweli? “Ningesema kwamba uzoefu wa soka katika ngazi ya juu kabisa ni kama hivyo. Maana, kama si suala la kufa na kupona, basi haimaanishi kuwa kitu kikubwa kwako na hivyo hutakaa kwa muda mrefu kwenye kazi hiyo,” Wenger anajibu.

Kuna wakati ushindani wa Wenger na wenzake ulivuka mipaka, kwanza kukwaruzana na Ferguson kisha Jose Mourinho wa Chelsea wakati wakiwa uwanjani na kwenye mikutano na wanahabari.

Lakini kama kuna mtu alitarajia Wenger awarushie matope na kuwachambua wawili hao, basi amekosea. Humo kuna mahali tu anagusia ‘kuanguka kwa mamlaka ya Fergie’, lakini anakwepa mengine yote hasi yaliyotokea miongoni mwao enzi zao. Mourinho ndio kabisa hatajwi humo.

“Sikutaka kiwe kitabu cha kulipiza kisasi au kuonesha kuchanganyikiwa au udhalimu. Sikutaka kuonesha kwamba ‘ehe, alinifanyia hivi’ – mambo yote haya. Lakini unajua kilichotokea maishani mwako ma unatakiwa juu ya hicho. Nilitaka kiwe juu ya uzoef chanya wa maisha. Huwezi kuwa na maisha niliyokwisha kuwa nayo na bado uwe hasi,” anasema Wenger.

Zaidi ya hapo, kocha huyu anayejulikana kama Profesa wa Soka anataka kuweka bayana wazi kwamba hadi vumbi inatua, kulikuwapo na heshima. “Kila kocha hupitia vipindi vizuri na vibaya. Ni wanadamu. Ni vigumu kupima kiwango cha kazi yetu. Kwa mfano, msimu uliopita, Liverpool walitwaa ubingwa na (Jurgen) Klopp akapongezwa kwa hilo. Nji sawa. Lakini lazima useme kwamba jamaa yule wa Sheffield United (kocha Chris Wilder), ambaye timu yake ilimaliza katika nafasi ya tisa alifanya kazi kubwa na nzuri pia. Nani basi aliyefanya kazi nzuri zaidi? Hujui,” ndiyo mawazo ya Wenger.

Tangu aondoke Arsenal, Wenger hajarudi kwenye ukocha, lakini tangu Novemba mwaka jana amekuwa Mkuu wa Maendeleo ya Soka Duniani katika FIFA. Alitengana na mke wake, Annie Brosterhous mwaka 2015; binti yao Léa anakamilisha masomo katika ngazi ya udaktari katika sayansi ya neva kwenye Chuo Kikuu cha Cambridge.

Anaugawa muda wake kati ya London, Paris na Zurich, mara nyingi akiishi hotelini. Anasema muda mgumu zaidi kwake ulikuwa wakati wa janga la virusi vya Corona pale ligi karibu zote duniani zilipositishwa.

“Sijui kwa nini lakini mechi za soka ndiyo maisha yangu na sidhani kwamba hali hiyo itakaa ibadilike. Kwa hiyo niliikumbuka sana,” anasema.

Wenger anakumbukia mengi akiwa Arsenal, kuanzia walivyokuwa wakicheza uwanjani, mwaka hata mwaka, haja ya kuwianisha fedha kati ya usajili, kulipa mishahara na kujenga uwanja mpya wa Emirates hadi nyakati zake za mwisho ambapo alipata upinzani kutoka kwa baadhi ya washabiki wa Arsenal waliokuwa wakimtaka astaafu mapema, pengine miaka miwili kabla ya 2018.

“Arsenal walikuwa na staili ya kucheza ambayo baadhi walikuwa wakiipinga, lakini ilikuwapo staili. Naweza kuwaelewa wale wanaotaka tu kushinda. Naamini katika kubadil staili na kushinda kimtindo. Shabiki akiamka anawaza tu iwapo timu itashinda, lakini lazima waone pia mchezo mzuri,” anasema.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
cedric kaze

Kocha Wa Yanga Kutua Siku Ya Azam FC

Baadhi ya wachezaji waliohama vilabu

Mambo yalivyo kwenye dili za usajili wa wachezaji