in

La Liga bila nyota wakubwa hali itakuwaje, serikali itakwepa lawama?

La Liga

Tusijidanganye kuondoka Cristiano Ronaldo ni wazi kumepunguza thamani ya Ligi Kuu Hispania. Vilevile hatuwezi kujiadanganya kuondoka kwa Neymar Junior hakujapunguza thamani ya La Liga. 

Na sasa kama Lionel Messi ataondoka Barcelona maana yake thamani ya La Liga itazidi kupungua. Wachezaji wenye mvuto wanaopoondoka klabu hupungukiwa mapato na La Liga kwa ujumla ndio maana Bosi wa La Liga Tebbas huwa anahangaika kuhakikisha klabu zinafikia mwafaka kwa wachezaji wao.

Wakati Neymar Junior alipokuwa anaondoka Barcelona tayari alishakwaruzana na serikali Hispania. Wakati mwingine Cristiano Ronaldo amewahi kukwaruzana na serikali kunusiana na suala la kodi. 

Lionel Messi naye alipandishwa kizimbani sababu ya suala la kodi. Kati ya wachezaji watatu hao wakubwa amebaki Lionel Messi peke yake La Liga. 

Ronaldo yupo Seire A kule Italia na kila kukicha anatamani siku moja Lionel Messi aondoke Barcelona na kwenda Juventus. Naymer Junior yuko PSG na kila siku anaongelea matamanio yake kumwona Lionel Messi akijiunga kwa miamba hiyo ya Ufaransa. 

Hapo hapo Pep Guardiola pale Manchester City anamwangalia kwa jicho la pili nyota wake wa zamani na bila shaka atatamani kufanya nae kazi siku moja. Kwahiyo nyota wakubwa kwa miaka ya karibuni wanaondoka La Liga hali ambayo inaonesha wazi ni pigo kwa umaarufu na uimara wa soko la michezo. 

Ninaposikia habari za Sergio Ramos na nyota wengine kuondoka La Liga inarejesha mawazo yalayale kuwa ligi inapungua thamani na kupoteza wachezaji wenye mvuto. Kama sio kufeli mitihani huenda Luis Suarez angeenda Juventus lakini badala yake akaelekea Atletico Madrid. Vivyo hiyo Thomas Partey mmoja wa viungo bora La Liga naye alihama Atletico Madrid msimu uliopita na kwenda Arsenal. Tunaweza kusema Arsenal walifika bei kwa Partey lakini kuondoka kwake La Liga ilikuwa pigo kwa mashabiki wa Afrika wanaofuatilia Ligi hiyo kwa vile alikuwa miongoni kwa nyota wanaovutia zaidi mashabiki kwa bara hili.

Kumbukumbu zangu zinaonesha mastaa kadhaa waliwahi kutimka Serie A ya Italia mara baada ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 kwa sababu za kodi. Ilielezwa mfumo wa kodi ulioletwa na serikali ulikimbiza nyota kadhaa kipindi hicho. Huku ikitajwa kuwa ni miongoni kwa sababu zinachangia wachezaji wakubwa kuzikimbia nchi ikiwa wanakwaruzana na mamlaka hizo kwa namna moja ama nyingine. 

Ndiyo kusema serikali ya Hispania haijajenga uhusiano mzuri na nyota kadhaa wanaokipiga La liga. Zipo kesi mbalimbali za zilizodaiwa ni ukwepaji wa kodi. 

Maoni yangu pengine ingelifaa kuchukua hatua stahiki za kuwawajibisha wachezaji hao bila kuwafikisha mahakamani. Nafikiri serikali ingeweza kuwa na utaratibu wa kuhakikisha nyota wote wanazingatia sheria na wanashughulikia pasipo kuingia viunga vya mahakama hali ambayo inachafua majina yao, ligi yao, klabu yao, wasimakizi wao,mawakala wao, familia zao, na soka la Hispania kwa ujumla wake. 

Pengine ingeweza kushughulikia suala la Ronaldo, Lionel Messi na wengine pasipo kupandishwa kizimbani. Ghadhabu za wachezaji hao ni za wazi kabisa huwezi kukwepa, na wanapoondoka wanasababisha mapato ya serikali kupungua. 

Kwa namna moja au nyingine serikali inachochea kuvuruga La Liga kwa kutoshughulikia kivingine masuala ya wachezaji wakubwa. 

Natambua wataalamu wa sheria watasema kila mtu ni sawa mbele ya sheria na hakuna mkubwa, lakini tunaangalia madhara ya usimamizi wa sheria pasipo busara ya kutatua tatizo. 

Serikali inapodai kodi ni haki, lakini inapotumia rungu la kodi kuwakamua wachezaji wa kigeni kwa namna moja ama nyingine inachochea baadhi yao kuamua kutoendelea kudumu La Liga kwa miaka ya karibuni. 

Nyota wa zamani sio sawa na wa sasa. Nakumbuka kwenye riadha Usain Bolt raia wa Jamaica aliwahi kukataa kushiriki mashindano ya riadha ya Diamond League ya London nchini Uingereza kwa madai kodi kubwa iliyokuwa inatarajiwa kukatwa kwenye malipo yake, hivyo fedha ambayo angepata ni ndogo. 

Kwa mazingira ya namna hii serikali inaweza kutengeneza utaratibu wa pande zote kupata chake cha kuridhisha kuliko kushikilia msimamo wa sheria kisha unakosa fedha zote na wachezaji wenyewe, haikusaidii wala husaidii maendeleo ya michezo.  

Kwahiyo kuvutia nyota wakubwa ni pamoja na namna serikali za nchi husika zinavyoshughulikia mambo ya wachezaji au wanamichezo wake. Hispania imekuwa ikikabiliwa na mambo ya ubaguzi lakini suala la kuwapndisha vizimbani wachezaji limekuwa sugu kiasi kwamba inafifisha nyota kadhaa kwenda huko. 

Wapo watu watasema ukwepaji wa kodi limekuwa jambo sugu ama serikali kuzembea lakini hilo haliwezi kuondoa hoja kwamba lazima uhusiano baina ya nyota wakubwa na mamlaka ya nchi uwekwe bayana. Kuwatingisha tingisha hakujengi soka la Hispania badala yake nyota wengi wakubwa wakiondoka na mapato yanayeyuka. 

Nafikiria pia kama Ramos,Messi na Modric wataondoka basi wataendeleza kupunguza mvuto wa klabu za Hispania. Kwa sababu wachezaji nyota watakuwa wanapungua na hakutakuwa na mvuto wowote vilabuni kwa vile wachezaji watakaobaki ni wale wa kawaida tu. Yaani wanabaki wachezaji wasio na ushawishi wowote ndani nan je ya uwanja.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Mauricio Pochettino

Fahamu mambo yanayomkabili Pochettino PSG

Sven Vandenbroeck

Tusisahau kukisifu kichwa cha Sven Vandenbroeck