Man U wanachekelea

*Jose Mourinho ametwaa kombe la kwanza na klabu yake mpya ya Manchester United*

Wakiwa bado katika nafasi yao waliyozoea ya sita kwenye msimamo wa
Ligi Kuu ya England (EPL), Man U walitwaa Kombe la Ligi – EFL baada ya
kuwafunga Southampton 3-2.
Alikuwa mshambuliaji hatari aliyesajiliwa bila ada, Zlatan
Ibrahimovic, 35, aliyefunga bao la ushindi dakika tatu tu kabla ya
muda wa mchezo kumalizika.
Saints walikuwa makini kwenye Uwanja wa Taifa – Wembley, lakini
walizidiwa dakika za mwisho na kuruhusu bao hilo. Kwa muda mwingi wa
mchezo walikuwa wazuri kuliko Man U.
Walivunjwa moyo pia kukataliwa bao la Manolo Gabbiadini kwa madai ya
mchezaji huyo kuotea, kana kwamba hiyo haitoshi Ibrahimovic
akawamaliza, akifunga bao lake la 26 kwa msimu huu katika mashindano
yote.
United walishafunga mabao mawili ya kuongoza kupitia kwa Ibrahimovic
na Jesse Lingard, lakini Saints wakapambana na kusawazisha kupitia kwa
Gabbiadini, bao moja kila kipindi.
Mourinho alionekana kutofurahia ufanisi wa timu yake kwenye fainali
hii, na atawakazania wachezaji wake zaidi kuongeza umakini kwenye
kazi. Hata hivyo, atafurahi kuweka historia kutwaa kombe na klabu hii
kubwa.
Amekuwa akililenga kombe hili, kwani mwaka 2005 aliwafunga Liverpool
akiwa na Chelsea uwanani japo na 2015 kadhalika, akiwafunga Tottenham
Hotspur.
United watakuwa Old Trafford kwao Jumamosi hii kuwakabili Bournemouth
kwenye EPL mchana wakati Saints watakuwa na kazi ya kupambana na
Watford.

==mwisho==

Comments