Barcelona majanga

LIGI ya Mabingwa Ulaya (UCL) imetoa matokeo ya aina yake, kwa
Barcelona kuambulia kichapo cha mbwa mwizi kutoka kwa Paris
Saint-Germain (PSG).

Barca wanaofundishwa na Luis Enrique walilala kwa mabao 4-0 ugenini
katika mechi ngumu kwao na watatakiwa kujitutumua ili kurudishwa zaidi
ya hayo kama wanataka kuvuka mtoano huu.

Angel di Maria aliyekuwa kwa mahasimu wao, Real Madrid alifunga mabao
mawili mazuri siku ya kuzaliwa kwake, wakati Julian Draxler alifurahi
kupata bao lake la kwanza UCL na la nne liliwekwa kimiani na Edinson
Cavani aliyeshangilia sana kana kwamba wametwaa ubingwa.

Ilikuwa ajabu kwa Barca ugenini, ambapo pacha wake watatu – Lionel
Messi, Luis Suarez na Neymar ni kama vile hawakuwapo uwanjani. Hakuna
cha maana walichofanya hadi dakika saba kabla ya mechi kumalizika,
pale Samuel Umtiti alipogonga mwamba.

Watarudiana na PSG Machi 8 katika uwanja wa Camp Nou nchini Hispania.
Hakuna timu iliyopata kufanikiwa kupindua matokeo ya kufungwa 4-0
kwenye UCL.

Messi ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye UCL msimu huu,
akiwa na mabao 10 katika kundi lao la C, wakishinda mechi tano kati ya
sita za kundi lao.

Walipoteza mechi moja, ikiwa ndiyo yenyewe kupata kukubali kufungwa
mabao matatu kwenye hatua ya makundi; walifungwa 3-1 na Manchester
City. Kibano hicho kilikuwa kwenye Uwanja wa Etihad.

Lakini Jumanne hii katika dimba la Parc des Princes, Paris, Ufaransa,
ulibaki usiku wa kusahau kwa Barca kwa jinsi walivyoshindwa hata
kumiliki mpira, wakipoteza kila mara.

PSG wanakuwa timu ya sita kufunga mabao manne dhidi ya Barcelona,
baada ya Milan, Dynamo Kiev, Valencia, Chelsea na Bayern Munich.
Katika mechi nyingine, Benfica wakicheza kwao Ureno walifanikiwa
kuwashinda Borussia Dortmund 1-0 na ni wazi mechi ijayo itakuwa kali.

Comments