Klabu zakataa mfumo mpya Kombe la Dunia

TAASISI inayoundwa na klabu kubwa barani Ulaya zimekataa mfumo mpya wa
fainali za Kombe la Dunia.

Mapema mwezi huu, Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA),
Gianni Infantino alipendekeza kwamba timu ziongezwe hadi 48 kwenye
fainali hizo.

Alitaka mashindano hayo makubwa zaidi ya mataifa, yawe na makundi 16
yenye timu tatu kila moja.

Hata hivyo, Chama cha Klabu za Ulaya (ECA) kimesema hakipo tayari
kuona hayo, kwani hivi sasa idadi ya mechi zinazochezwa kwa mwaka ni
nyingi kupita kiasi, hivyo kuwagharimu wachezaji na klabu zao.

“Tunawataka FIFA wasiongeze idadi ya washiriki wa fainali za Kombe la
Dunia,” akasema Mwenyekiti wa ECA, Karl-Heinz Rummenigge.

Hata hivyo, Baraza la FIFA litajadili mapendekezo hayo ya Infantino
Januari 9 mwaka kesho.

Raia huyo wa Uswisi aliyechukua uongozi kutoka kwa raia mwenzake, Sepp
Blatter, alikuwa ameweka ahadi ya kuongeza timu shiriki kama moja ya
ajenda zake kwa ajili ya kampeni za uchaguzi.

Amekuwa akitaka nchi zaidi kupata fursa ya kupambana, wachezaji
wakipeperusha bendera za nchi zao.

Mara ya mwisho kwa nchi kuongezwa kwenye fainali hizo ni 1998, kutoka
nchi 24 hadi 32. Mabadiliko yoyote hayatarajiwi kufanywa kabla ya
fainali za 2026.

Rummenigge anasema kwamba lazima kuangalia vyema kwenye soka kama soka
na kwamba siasa na biashara visipewe kipaumbele kuliko mchezo huo.

ECA inawakilishi klabu zaidi ya 200, zikiwa ni pamoja na Chelsea,
Manchester United, Real Madrid, Barcelona, Juventus na Bayern Munich
anakotoka mwenyekiti huyo.

Comments