Man United hoi

West Ham wameaga kwenye uwanja wa Upton Park walikocheza kwa miaka 112
kwa ushindi wa kusisimua dhidi ya Manchester United, katika mechi
ambayo kocha Slaven Bilic anasema ilikuwa kama sinema.

United wanaohangaika kupata nafasi nafasi ya nne iwapo mahasimu wao
Manchester City watapoteza mechi ya mwisho huenda wakakosa ushiriki wa
Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), lakini itabidi wasubiri hadi pazia la
Ligi Kuu ya England (EPL) linaposhushwa Jumapili hii.

West Ham walishinda kwa mabao 3-2 kwenye dimba linalojulikana pia kama
Boleyn Ground ambao wamechezea tangu 1904, ikimaanisha kwamba sasa
United wanashika nafasi ya tano wakiwa na pointi 63, mbili nyuma ya
Man City na tano nyuma ya Arsenal.

Vijana hao wa Louis van Gaal watamaliza msimu nyumbani kwa mechi dhidi
ya Bournemouth, ambapo laiti wangeshinda wangejiweka pazuri kuishika
nafasi ya nne, lakini sasa inamaanisha Man City wanaomalizana na
Swansea wanaweza kuchukua nafasi hiyo muhimu.

Leicester ambao ni mabingwa wana uhakika wa ushiriki kwa pointi zao
80, Tottenham Hotspur bado wanasubiri kujua watamaliza nafasi ya ngapi
kwani kwa sasa wanashika ya pili wakiwa na pointi 70, Arsenal wa tatu
wakiwa nazo 68. West Ham ni wa sita kwa pointi zao 62 na Southampton
wa saba baada ya kujikusanyia pointi 60.

Mechi hiyo ya Jumanne ilichelewa kuanza baada ya basi la United, kwa
mara nyingine, kuwasili kwa kuchelewa na basi lao kushambuliwa na
washabiki wa Wagonga Nyundo wa London kwa chupa na kuliharibu kidogo
wakati likiingia uwanjani, hivyo mechi kuchelewa kuanza.
Walioshambulia wamefungiwa maisha na West Ham.

Wenyeji wakishangiliwa vilivyo walianza vyema na kupata bao katika
dakika ya 10 tu kupitia kwa Diafra Sakho, likadumu hadi kipindi cha
pili pale Mfaransa Anthony Martial aliposawazisha dakika ya 51 na
kuongeza la pili dakika ya 72.

Mambo yaliwabadilikia wageni kwani Michail Antonio alitikisa nyavu za
United dakika nne tu baadaya hapo na Mashetani Wekundu wakaanza kuloa
dakika ya 80 pale Winston Reid alipopigilia msumari wa mwisho.

United, kama ilivyozoeleka msimu huu, walishindwa kutumia vyema fursa
za kujipatia mabao zaidi na hata ushindi. Yawezekana kuchelewa kwao
kuliwaathiri, ambapo kama West Ham wangetumia vyema nafasi walizopata,
hadi mapumziko wangekuwa mbele kwa zaidi ya bao moja na pengine
kuibuka na ushindi mkubwa zaidi.

Mechi hiyo ilihudhuriwa na washabiki 34,662 ikiwa ni ya mwisho kwa
West Ham hapo, kwani msimu ujao wanahamia kwenye Uwanja wa Olimpiki
ambao si mbali sana na hapo.

Aston Villa wameshashushwa daraja kwani wana pointi 17 kutokana na
mechi 37. Wanaosubiri kujua hatima yao ligi kuu ni Norwich wenye
pointi 31, Newcastle wenye pointi 34 huku Sunderland wakiwa nazo 35.
Wawili kati yao lazima washuke daraja. Ushukaji utategemea matokeo ya
mechi za leo; Norwich dhidi ya Watford, Sunderland dhidi ya Everton na
zile za mwisho Jumapili ijayo.

Comments