Barcelona ‘out’ Ulaya

*Bayern wapenya kwa tabu

Yametimia. Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya – UCL,
Barcelona wametupwa nje na Wahispania wenzao, Atletico Madrid katika
mechi ngumu ya robo fainali.

Japokuwa waliingia dimbani wakiwa na akiba ya ushindi wa mabao 2-1
waliopata nyumbani kwao Nou Camp, waliduwazwa na Atletico
wanaofundishwa na Diego Simeone, wakakubali kukalishwa chini.

Hapakuwa na yale mazoea ya kuona pasi, mikimbio na mahitimisho ya
kupachika mabao nyavuni kutokana na ushirikiano wa wachezaji Lionel
Messi, Luis Suarez na Neymar, bali ilikuwa kama kivuli cha timu
iliyowika sana msimu uliopita.

Waliduwazwa na mabao mawili ya Antoine Griezman, ambapo Messi sasa
ameshindwa kufunga bao katika mechi tano mfululizo huku Barca
wakipoteza mechi tatu kati ya nne zilizopita kwenye mashindano
mbalimbali.

Bayern wapenya kwa tabu
Bayern wapenya kwa tabu

Kocha Luis Enrique amekubali matokeo na kusema anabeba lawama zote,
kama alivyopokea pongezi msimu uliopita kwa kutwaa ubingwa wa La Liga,
Ulaya na Kombe la Mfalme. Wamepoteza mechi mbili mfululizo katika La
Liga msimu huu, ikiwamo dhidi ya Real Madrid.

Katika mechi nyingine, Bayern Munich walifanikiwa kuvuka, baada ya
kwenda sare ya 2-2 na Benfica. Wameinia nusu fainali kutokana na
kwamba kwenye mechi ya awali walipata ushindi wa bao moja.

Arturo Vidal aliyefunga kwenye mechi hiyo ya Allianz Arena ndiye pia
alifunga bao moja Jumatano hii na jingine likafungwa na Thomas Muller.
Mabao ya Benfica yalifungwa na Jimenez Rodriguez na Souza
Conceição.

Comments