Ngoma aipania Al Ahly

MSHAMBULIAJI wa kutumainiwa wa mabingwa soka wa Tanzania Bara, Yanga, Donald Ngoma amesema itakuwa mara ya kwanza kukutana na Al Ahly katika mchezo wa klabu bingwa Afrika, hivyo amepania kufanya makubwa, ambapo sasa anajifua kwa pambano hilo litakalofanyika Aprili 9 mwaka huu Uwanja wa Taifa.

Ngoma ameonyesha uwezo mkubwa katika kikosi cha Yanga, ambapo kila mara anakuwa shujaa kwa kupambana ili kuihakikishia timu yake inasonga mbele.

Akizungumza jijini Dar jana, nyota huyo raia wa Zimbabwe alisema maandalizi binafsi anayofanya ni kuhakikisha wanaitupa nje ya mashindano klabu hiyo kigogo cha soka kutoka Misri.

“Ni timu yenye uzoefu mkubwa katika michuano hii kwa kufika katika ngazi mbalimbali, hali hiyo tutahakikisha kufuata maelekezo ya kocha ili kujiweka sawa kwa kufanya vyema katika mchezo wetu huo,” alisema.

Alisema kocha wao Hans van Pluijm amefanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mchezo wao dhidi ya APR , hali hiyo atahakikisha kuwa makini ili kuisaidia timu yao kusonga mbele.

Aliongeza kuwa wachezaji wote wapo kwenye ari kubwa na wanahitaji kuonaYanga inaendelea kusonga mbele zaidi katika michuano hiyo hivyo atakuwa makini kufanyia kazi majukumu anayopewa na kocha wao kuhakikisha wanafanya vyema.

Comments