Simba yarejea kileleni

Ushindi wa mabao mawili kwa sifuri walioupata Simba Sports Club kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City yamewarejesha Wekundu hao kwenye usukani wa Ligi Kuu Bara.

Simba walilazimika kusubiri dakika za mwishoni kujihakikishia ushindi huo baada ya kushindwa kutumia nafasi kadhaa walizotengeneza kwa zaidi ya saa nzima ya kwanza ya mchezo.

Bao la kwanza la mchezo huo lilifungwa na Daniel Lyanga aliyeingia mwanzoni mwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Brian Majwega.

Lyanga alifunga bao hilo mnamo dakika ya 68 akitumia nafasi iliyopatikana pale golikipa Hannington Kalyesubula alipopangua shuti la Awadh Juma aliyepokea pasi safi ya Ibrahim Ajib.

Ajib aliyeng’ara zaidi kwenye mchezo huo aliihakikishia ushindi timu yake kwa bao safi kwenye dakika ya 90 ya mchezo.

Sasa vijana hao wa Jackson Mayanja wamefikisha jumla ya alama 48 baada ya michezo 21. Wamerejea tena kileleni wakifuatiwa na Yanga na Azam zilizo kwenye nafasi ya pili na ya tatu.

Hata hivyo Azam na Yanga zenye alama 47 kila moja zimecheza michezo 20 pekee, mchezo mmoja pungufu ya michezo ya Simba.

 

Comments