Chelsea wawaogesha Man City

Chelsea wamewatandika Manchester City 5-1 kwenye mechi ya kufuzu kwa
robo fainali ya Kombe la Ligi.
Wakicheza nyumbani Stamford Bridge, Chelsea walionekana kuwazidi nguvu
City, ambapo wageni walichezesha kile tunachoweza kusema ni kikosi cha
pili.
Manuel Pellegrini aliwachezesha matineja watano kwa pamoja kwa mara ya
kwanza, na alionya mapema kwamba hangeweka wachezaji nyota.
Hiyo inatokana na ukweli kwamba mechi ilipangwa kuchezwa jioni ya
Jumapili wakati Jumatano wana mechi mbali, Ukraine, kwenye mkondo wa
kwanza wa 16 bora, ikiwa ni mtoano baina yao na
Dynamo Kiev katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Waliopewa nafasi ni pamoja na mlinzi mdogo, Tosin Adarabioyo, viungo
Manu Garcia na Aleix Garcia sambamba na Bersant Celina na David
Faupala, majina mapya masikioni mwa wengi.
Kiungo wa Chelsea aliyeanza vibaya msimu wa 2015/16 kiasi cha kutakiwa
kuuzwa, Eden Hazard, alirejea katika kiwango cha juu na alikuwa
mchezaji bora katika mechi hiyo.
Mabao ya Chelsea yalifungwa na Diego Costa, Willian, Garry Cahil, Eden
Hazard na Traore wakati la Man U lilitiwa kimiani na Faupala.
Wakati City wanasafiri kwa ajili ya mechi hiyo ya UCL, Chelsea
watapumzika hadi Jumamosi kwa ajili ya kukabiliana na Southampton
kwenye mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL).
Jumapili City wana kibarua kingine kigumu, ambapo watapepetana na
Liverpool katika Uwanja wa Wembley, kwenye fainali ya Kombe la Ligi.
Katika mechi nyingine Jumapili hii, Blackburn walipata aibu nyumbani
kwa kucharazwa 5-1 na West Ham wakati Tottenham Hotspur nao walilambwa
1-0 na Crystal Palace.

Comments