Arsenal wanasota

 
Arsenal wamepoteza nafasi ya kufungana pointi na vinara wa Ligi Kuu ya England (EPL), Manchester City baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 walipowatembelea Norwich.

Wageni walianza kupata bao kupitia kwa kiungo Mjerumani, Mesut Ozil anayeng’ara na ambaye alihakikisha pasi zake ni za uhakika kwa zaidi ya asilimia 98 lakini likasawazishwa na Lewis Grabban.

Katika mechi hiyo Arsenal wameongeza orodha ya majeruhi wao, ambapo beki wa kati muhimu Laurent Koscielny aliumia paja mapema kipindi cha kwanza na kisha kile cha pili ikawa zamu ya Alexis Sanchez aliyebanwa na misuli.

Arsenal sasa wana pointi 27, wakiwa pointi mbili nyuma ya vinara wa ligi hiyo, Man City ambapo nafasi ya pili inashikwa na Leicester wanaofungana pointi na City, ya tatu wakiwapo Man United. Huenda kocha Arsene Wenger akalazimika kuboresha kikosi chake Januari ikiwa anataka kweli kupigania ubingwa wa England.

Katika mechi nyingine za Jumapili hii, Tottenham Hotspur walikwenda suluhu na Chelsea, West Ham wakaenda sare ya 1-1 na West BromwichAlbion. Matokeo ya jumla ya wikiendi hii yanafanya Aston Villa kubaki mkiani wakiwa na pointi tano, juu yao wakiwa Newcastle wenye pointi 10 sawa na Bournemouth.

Comments