ULAYA YATIKISIKA:

 

*Mechi ya Hispania vs Ubelgiji yafutwa*

 

Ulaya inaonekana kutikiswa na mashambulizi ya kigaidi yaliyoua watu 129 jijini Paris, Ufaransa, ambapo mechi ya kimataifa baina ya Ubelgiji na Hispania imefutwa.

Mechi hiyo iliyokuwa ifanyike Jumanne hii sasa imeahirishwa kwa sababu za kiusalama, huku kukiwa na taarifa kwamba mmoja au zaidi ya wahusika wa milipuko hiyo walitoka Ubelgiji.

Mauaji hayo yaliyolaaniwa duniani kote ililenga sehemu za starehe pamoja na eneo la mechi ya kirafiki baina ya Ufaransa na Ujerumani – Stade de France.

Wapelelezi na waendesha mashitaka wa Ubelgiji wanasema kwamba Mbelgiji ndiye alipanga yote hayo na sasa Serikali ya Ubelgiji imeongeza kiwango cha makadirio ya uwezekano wa kutokea hatari kama hiyo nchini humo.

de
Wachezaji wa Ufaransa, wakifanya mazoezi kabla ya mchezo wao na England

Chama cha Soka cha Ubelgiji kimesema kwamba kimechukua uamuzi huo uliokuwa ufanyike katika Uwanja wa King Baudouin jijini Brussels, yalipo makao makuu ya serikali.

Walichukua hatua hiyo baada ya kuwasiliana na wenzao wa Hispania, wakiona kwamba maisha ya wanadamu ni bora kuliko kitu kingine chochote.

 

“Kwa kuzingatia hali isiyo ya kawaida, hatuwezi kuhatarisha maisha ya wachezaji na washabiki wetu. Tunasikitishwa kwa uamuzi huu uliochelewa na tunaelewa jinsi washabiki wanavyosikitishwa kuukosa mchezo,” limesema tamko la FA ya Ubelgiji.

Kocha wa Hispania, Vicente del Bosque amesema kwamba pamoja na kukaa kwa muda mfupi Ubelgiji, hawana woga wowote na wapo salama kwenye hoteli hiyo, hivyo hapakuwapo tatizo lolote.

“Tulifanya mazoezi kwa utulivu, tulihiandaa kwa ajili ya mechi kama ilivyo nyingine zozote, lakini mamlaka zimeona kwamba haziwezi kutuhakikishia usalama kila mmoja wetu, wachezaji na washabiki.

“Matumaini yetu ni kwamba hapatakuwapo tena matukio ya kuahirisha mechi hizi. Tupo hapa kwa ajili ya kufanya michezo na kuburudisha watu,” anasema Del Bosque.

Kocha huyo mkongwe alikuwa akitafuta fursa ya kuonesha umwamba zaidi Ulaya, baada ya kuwafunga England 2-0 Ijumaa iliyopita kwenye mechi ya kirafiki nchini Hispania.

Kwa upande wake, Chama cha Soka cha Ufaransa (FFF) kimeamua kusonga mbele na mechi dhidi ya England kwenye Uwanja wa Wembley jijini London.

Wachezaji wake walionekana wakiingia London wakiwa na hisia kali na uchungu, lakini wanasema watavaa jezi zao na kucheza kwa nguvu na fahari kubwa.

Nahodha wa England, Wayne Rooney ameeleza kwamba watawaonesha magaidi kwamba watu wote wapo dhidi yao.

Advertisement
Advertisement

Comments