Mourinho alimwa faini

 

Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amepigwa faini ya pauni 50,000 baada ya kutiwa hatiani na Chama cha Soka (FA) kwa kosa la kutoa maoni potofu dhidi ya waamuzi.

‘The Special One’, kama anavyopenda kujulikana, alidai kwamba waamuzi wamekuwa wakiogopa kuwapa Chelsea penati. Alidai hayo baada ya kufungwa 3-1 na Southampton kwenye mechi iliyopita.

Mwamuzi wa mechi hiyo alikuwa Robert Madley; na FA wanasema kwamba matamshi ya Mourinho yanaonesha kana kwamba waamuzi wamekuwa wakipendelea baadhi ya timu.

Mourinho pia amepewa adhabu ya kukosa mechi moja, ambayo hata hivyo, hatatakiwa kuitekeleza sasa, isipokuwa akirudia matamshi kama hayo ndani ya mwaka mmoja.

Advertisement
Advertisement

Kufungwa kwa Chelsea na Southampton nyumbani Stamford Bridge kulifanya mabingwa hao watetezi kuwa wamepoteza mechi nne kati ya nane za awali katika msimu huu wa Ligi Kuu ya England.

Chelsea wapo pointi 10 nyuma ya vinara wa ligi, Manchester City, lakini pia wapo pointi nne tu juu ya ukingo wa kushuka daraja katika jedwali la msimamo wa ligi yenye timu 20.

Akizungumza baada ya mechi hiyo iliyotoa matokeo machungu kwao, Mourinho alidai kwamba Chelsea walikuwa “siku zote wakiadhibiwa” na makocha kwa sababu “mara nyingi kuna alama ya kuuliza” kutoka kwa vyombo vya habari.

“Ikiwa Chama cha Soka wanataka kuniadhibu basi na wafanye hivyo. Huwa hawaadhibu makocha wengine,” aliongeza Mourinho na kuifedhehesha FA.

Chelsea tayari wameeleza kusikitishwa na adhabu hiyo. Klabu walieleza mapema kwamba bado wanamuunga mkono Mourinho wakati Chelsea wakiwa wameshapoteza mechi tatu za awali na kabla ya kukabiliana na Southampton.

Comments