Taifa Stars wavuka

Baada ya kufungwa 1-0 na Malawi ugenini

YAANGUKIA KWA ALGERIA.

Timu ya Taifa ya Tanzania – Taifa Stars – wamevuka kwenda raundi ijayo ya kufuzu kwa fainali za michuano ya Kombe la Dunia 2018.

Stars wamevuka kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya kufungwa 1-0 na Malawi ugenini. Katika mechi ya awali jijini Dar es Salaam, Stars walishinda 2-0.

The Flames wa Malawi walirejea mchezoni jijini Blantyre ambapo walifanya kila namna dimbani kushinda na walipata bao lao kupitia kwa John Banda dakika ya 43 Jumapili hii.

Hata hivyo, kwa kushindwa kupata bao la pili, The Flames walitolewa kwenye mchakato wa kuelekea kwenye fainali hizo.

Hizi ni habari njema kwa Tanzania, na mafanikio kwa kocha mzawa Charles Boniface Mkwasa, ambaye ndio kwanza amepewa mkataba wa kudumu kuwanoa Stars huku akiacha kazi ya ukocha msaidizi Yanga.

Tanzania walipatwa ukame wa mabao, ambapo washambuliaji wake wanaokipigaTP Mazembe nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu hawakuweza kufumania nyavu, tofauti na walivyofanya kwenye mechi ya awali.

Stars wapo katika wakati mgumu kwenye mechi ijayo watakapokabiliana na Algeria kwenye hatua nyingine ya kufuzu kwenda Urusi 2018.

Matokeo hayo yametia shinikizo zaidi kwa kocha wa Malawi, Ernest Mtawali ambaye alipewa kazi hiyo Agosti mwaka huu tu.

Ethiopia wanawakaribisha Sao Tome & Principe, wakisaka kushinda baada ya kuwa walifungwa  bao 1-0 kwenye mechi ya awali. Mshindi atacheza na Kongo Brazzaville kwenye raundi ijayo.

Advertisement
Advertisement

Comments