Carneiro aondoka Chelsea

 

Eva Carneiro, yule daktari wa Chelsea aliyebwatukiwa na kocha Jose Mourinho, ameamua kuacha kazi.

Mourinho alimshambulia daktari huyo, akidai alifanya kazi kana kwamba hana uzoefu wa masuala ya mpira, alipoingia uwanjani na kisha kumtibu Eden Hazard huku timu ikiwa tayari na upungufu wa mtu mwingine mmoja.

Ilikuwa ni katika mechi dhidi ya Swansea wiki sita zilizopita, ambapo walikwenda sare ya 2-2. Carneiro, hata hivyo, aliingia uwanjani baada ya kuitwa na mwamuzi Michael Oliver na tangu hapo Mourinho amepingwa na watu wengi kwa msimamo wake huo.

Baada ya tukio hilo, Mourinho alimshusha hadhi na kumwondosha kwenye benchi la madaktari wa kikosi cha kwanza, ambapo hajampa nafasi tena kuhudumia wachezaji uwanjani. Mourinho alidai kwamba alikuwa na uhakika Hazard hakuwa ameumia.

Carneiro, 42, mzaliwa wa Gibraltar sasa anataka kushughulikia suala hilo kisheria zaidi, kwani inadaiwa kwamba Mourinho alimtusi uwanjani hapo, ikiwa ni pamoja na kutoa madai kwamba ametoka kwenye familia ya waasherati.

Chelsea walimwomba daktari huyo arejee kazini, lakini ameamua kuondoka wakati ambapo Chama cha Soka (FA) kinachunguza malalamiko dhidi ya Mourinho na lugha aliyotumia dhidi ya daktari huyo anayependwa na washabiki.

Klabu imekataa kutoa maoni juu ya uamuzi wa Carneiro, ikisema kwamba huwa haizungumzii masuala ya ndani ya wafanyakazi wake. Hata hivyo, Mjumbe wa Bodiya FA, Heather Rabbatts ameeleza kusikitishwa na kukasirishwa kwake na jinsi Carneiro alivyotendwa.

Rabbats amesema kuondoka kwa Carneiro kuna maana kuna tatizo kubwa zaidi ya inavyofikiriwa, akataka suala hilo limalizwe mapema iwezekanavyo ili aweze kuendelea na kazi katika nafasi za juu kwenye soka.

Amesema hali za wachezaji zinaachwa katika shaka iwapo wale wanaowahudumia wanashambuliwa wanapotekeleza wajibu wake. Rabbatts ndiye mwanamke pekee kwenye Bodi ya FA.

Comments