De Gea sintofahamu

 

Uhamisho wa kipa namba moja wa Manchester United, David De Gea kwenda Real Madrid ambao ungegharimu pauni milioni 29 unaelekea kukwama.

 

Inaelezwa kwamba nyaraka zilizotakiwa zilichelewa kuwasili Hispania, hivyo kukuta dirisha la usajili limeshafungwa. Katika mpango huo, ilikuwa Madrid wawape United kipa wao, Keylor Navas.

 

Sintofahamu hiyo inaacha wengi wakiwa na maswali, na haijapata kutokea Hispania wakatoa muda wa nyongeza kukamilisha usajili, tofauti na ilivyo England. Baadhi ya wahusika wa Real wanadai kwamba Man U walifanya makusudi kuchelewesha nyaraka hizo.

 

Tayari vibonzo vimeanza kuchorwa kwenye mitandao ya jamii, ikimwonesha Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa United, Ed Woodward anayeshutumiwa kwa kushindwa kuunganisha dili za usajili, akichana karatasi kwenye mashine badala ya kuzituma Madrid.

 

Makao Makuu ya Shirikisho la Soka la Hispania yalitangaza kwamba lazima nyaraka zifike kabla au saa tano kamili, lakini United walizituma kwa mtandao na kufika dakika moja baada ya muda huo. Hata hivyo, United wanadai kwamba wanayo stakabadhi inayoonesha waliwasilisha kwa muda unaotakiwa.

advertisement
Advertisement

 

Kinachosubiriwa sasa ni kuona hatua zitakazochukuliwa na shirikisho ili kuweka sawa jambo hilo au kama Madrid wataamua kukata rufaa kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wenye uamuzi wa mwisho juu ya idhinisho la uhamisho wa kimayaifa.

 

Iwapo Real hawataruhusiwa mtu wao, hawatakata rufaa au wakikata rufaa na kukataliwa, ina maana De Gea atarudi Old Trafford kupigania nafasi yake katika kikosi cha kwanza na makipa wengine waliopo. Tofauti na Madrid, United bado wana nafasi ya kukamilisha taratibu za kumpata kipa Navas.

Comments