Man United wabanwa

 

Manchester United wamebanwa na Newcastle kwa kulazimishwa suluhu kwenye mechi nzuri iliyopigwa Old Trafford, ambapo ukame wa mabao wa nahodha na mshambuliaji wa kati wa United umeendelea, licha ya kuwa aliahidi mabaoyangeanza kuonekana.

 

Rooney, hata hivyo, alifunga bao lililokataliwa kwa sababu ya kuotea. Newcastle wamepata pointi yao ya pili katika michezo mitatu wakati United wamefikisha saba, kwani walishinda mechi mbili za kwanza, kila moja kwa bao 1-0.

 

Man U walianza vyema, lakini Newcastle wakajibu baadaye kupitia kwa wachezaji wake Aleksandar Mitrovic na kipa Tim Krul aliyefanya kazi nzuri, ikiwa ni pamoja na kumzuia Javier Hernandez kufunga.

 

Kocha Louis van Gaal alisema kikosi chake kilicheza vizuri lakini akasema matokeo hayo hayapendi na kwamba hawakuwa na bahati. Kocha Stev McClaren wa Newcastle alisema walilinda vyema lango lakini bado hawajafikia kiwango ambacho angependa wawe nacho.

 

Katika mechi nyingine Jumamosi hii, Crystal Palace wamewaangusha Aston Villa 2-1, Leicester wakaenda sare ya 1-1 na Tottenham Hotspur kama ilivyokuwa kwa Norwich dhidi ya Stoke na Pia Sunderland dhidi ya Swansea. Bournemouth waliofungwa bao batili na Liverpool na likakubaliwa kwenye mzunguko uliopita, wameonja ushindi wa kwanza Ligi Kuu baada ya kuwapiga West Ham 4-3.

 

Jumapili hii kuna mechi yenye mvuto baina ya West Bromwich Albion wanaowakaribisha Chelsea. Walipokutana mara ya mwisho msimu uliopita Chelsea walioga kichapo cha 3-0. Everton wanawakaribisha Manchester City wakati Watford watakuwa wenyeji wa Southampton.

advertisement
Advertisement

Comments