Stopilla Sunzu aenda Lille

Mchezaji wa kimataifa wa Zambia, Stopilla Sunzu amejiunga na klabu ya Lille iliyo Ligi Kuu ya Ufaransa kwa mkataba wa mwaka mmoja akitoka China alikokuwa akichezea Shanghai Shenhua.

Sunzu, 26, atakuwa kwa mkopo hapo, ambapo anaungana na kocha wa zamani wa taifa lake aliyefanya naye kazi na kuwapa Zambia ubingwa wa Afrika, Herve Renard , ambapo ni mara ya tatu kuungana naye, kwani walikuwa wote pia Sochaux.

“Hizi ni habari nzuri sana kwangu kujiunga na klabu kubwa kama Lille, nimemjua Herve Renard kwa muda mrefu. Uwapo wake hapa umechangia kwa kiasi kikubwa mie kufikia uamuzi wa kujiunga na Lille, yeye ni kama baba kwangu,” anasema Sunzu.

Wawili hao walipata mafanikio makubwa pale Zambia walipotwaa ubingwa wa Afrika 2012, ambapo Sunzu ndiye alifunga penati ya ushindi walipocheza na Ivory Coast kwenye fainali. Baada ya hapo kocha huyo aliondoka.

Renard aliandika kwenye tovuti ya klabu kwamba Sunzu ni mlinzi mzuri na mwenye kasi na viwango vingi japokuwa wakati mwingine huonesha kwamba hajakomaa na anahitaji chachu zaidi, ambapo atakuwa mzuri akiwa na wachezaji Renato Civelli au Marko Basa.

“Kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2012 alikuwa mwamba wetu. Bila yeye ingekuwa vigumu kupata ushindi kwenye fainali. Kusajili kwake na Lille ni kitu chanya sana kwetu,” akasema Renard.

Katika hatua nyingine mchezaji wa kimataifa wa zamani wa Ivory Coast, Didier Zokora amejiunga na klabu ya Ligi Kuu ya India, FC Pune City. Zakora, 34, ni kiungo aliyethibitisha uhamisho wake kupitia akaunti yake ya Twitter.

Zakora ndiye mchezaji aliyekipiga zaidi na Timu ya Taifa ya Ivory Coast katika historia ya soka nchini humo, kwani amecheza mechi 123 kabla ya kustaafu kwake Septemba mwaka jana. Amechezea klabu saba hadi sasa, ikiwa ni pamoja na St Etienne ya Ufaransa na Tottenham Hotspur ya England.

Comments